Mtazamo wangu kauli ya Mbunge Gwajima

28Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mtazamo wangu kauli ya Mbunge Gwajima

CCM imeahidi kufuatilia kwa makini mienendo na kauli za baadhi ya wanachama wake ambao imedai wanapotosha umma na kwenda kinyume na maelekezo ya Mwenyekiti Rais Samia Suluhu Hassan, na pia maadili ya chama chao.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, anaeleza kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya wanaotumia nafasi hiyo kusukuma ajenda binafsi.

Anatoa kauli hiyo baada ya mbunge wa Kawe (CCM) na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kudai daktari atakaye ‘shadadia’ chanjo ya corona bila kufanya utafiti wa kina kujua madhara ya muda mrefu na mfupi atakufa.

Ni katika ibada ya Jumapili iliyopita wakati akihubiri kanisani hapo ndipo alipoonyesha mashaka kuwa chanjo za corona zinaweza kuwa hatari kwa maisha.

Pengine si sahihi kama mbunge wa CCM kupingana na serikali yake hali ambayo inaweza kusababisha watu kukosa upande wa kusimamia kuhusu chanjo.

Askofu Gwajima ana ushawishi kwenye kanisa na jamii pia, hivyo kauli yake inaweza kuchukuliwa kwa uzito na pengine kusababisha wengi kutowaamini na kuwa na hofu na wanaopigia chapuo dawa hizo wakiwamo wakuu wa serikali.

Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa ndiye aliyekubali chanjo ya corona iletwe nchini, hivyo kusema kuwa wanaopigia chapuo dawa hizo wamepewa pesa, ni kama kumgombanisha na wananchi.

Huenda mbunge na Askofu Gwajima, akawa ameteleza kidogo kwa kauli hiyo, ambayo inapingana na juhudi za serikali za kukabiliana na corona.

Hata hivyo suala la COVID-19, limeibua mambo mengi na hasa taarifa feki, kujenga hofu na kuogopesha watu kuhusu chanjo yake.

Ndiyo maana Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema tangu kuzuka maradhi hayo, wanapambana na maadui wawili, taarifa feki pamoja na mlipuko wa COVID-19.

Anasema kumekuwapo na elimu nyingi zisizotokana na wataalamu wa afya ambazo dunia (wakiwamo Watanzania) wamekuwa wakipokea zinazidi kuwaweka njiapanda washindwe kujua ukweli au uongo uko wapi.

Pengine pia Gwajima ametumia maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM, alipohutubia bunge na kuwataka wakosoe serikali na kuleta mambo chanya na mbadala kwa maendeleo.

Hata hivyo, katika vita hiyo vya corona ni vyema Rais, Wizara ya Afya na CCM wakatoa mwongozo unaohusu namna bora ya kutoa taarifa ili kuepusha uwezekano wa kuwa na maelekezo yanayokinzana na yenye kuwachanganya wananchi.

Kwenye suala la chanjo ya corona, busara itumika zaidi kwani wananchi wanaona ni jambo jipya, lakini kuna taarifa nyingi zinazotolewa na pia madhara yake yameelezwa kuwa ni pamoja na damu kuganda, kubadilisha mifumo ya nasaba (DNA) inayohusisha kinga na kwamba unaweza kuchanjwa lakini ukaumwa tena COVID-19 hata kupoteza maisha.

Waziri wa Afya wa Uingereza, Sajid Javid, alithibitisha kuambukizwa corona licha ya kuchanja mara mbili, lakini anaamini kuwa imesaidia kupunguza makali ya ugonjwa huo na sasa yuko salama, yote hayo ni mambo yanayoongeza tafakari ya chanjo.

Hivyo CCM badala ya kusema inafuatilia kauli za viongozi wake, ingependeza iwapo angeitwa na kusikilizwa, kwani inawezekana kupata maelezo mengine zaidi na serikali ikawa katika nafasi nzuri ya kuyafanyia ufafanuzi.

Pamoja na hayo ni vyema kiongozi huyo wa kiroho atumie muda mwingi kuhamasisha wananchi na waumini wake kuzingatia mwongozo wa Wizara ya Afya wa kujikinga na COVID-19.

Wizara imetoa mwongozo mpya wa karibuni unaelekeza mambo mbalimbali kama kuvaa barakoa kwenye mikusanyiko, kunawa na kutumia vitakasa mikono.