Muda wa usajili laini simu uangaliwe upya

17Jan 2020
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Muda wa usajili laini simu uangaliwe upya

KWENYE maeneo mengi nchini kwa sasa wananchi wanahangaika kupata namba za vitambulisho vya Taifa ili waweze kusajili laini zao kabla ya Januari 20, mwaka huu.

Tayari Mamlaka ya MawasilianoTanzania (TCRA), imetoa tangazo kusisitiza kuwa ifikapo Januari 20, laini zote ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole zitafungwa na wahusika wataendelea kusajiliwa ndipo zitafunguka.

Usajili wa laini hauna kikwazo chochote kwa kuwa hakuna foleni na kampuni za simu zimejipanga ipasavyo, kwa kuwa kuna mashine ndogo zinazotumiwa na vijana wanaotembea hadi kwenye makazi ya watu kusajili laini za simu.

Kwa takribani miezi sita sasa changamoto kubwa imekuwa ni kupata namba ya utaifa kabla ya kitambulisho chenyewe, na wengi wanalilia kupata namba namba hizo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Wengi wameshajiandikisha na kupeleka viambatanisho muhimu, lakini wameambiwa wasubiri wiki tatu hadi nne ili kupata namba.

Yapo maeneo ambayo wananchi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma huyo, mathalani wananchi wanaoishi Ugweno mkoani Kilimanjaro, wanatakiwa kusafiri hadi Mwanga kujiandikisha kwa ajili ya kupata namba.

Kuna wakati Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) walikwenda Ugweno wakaandikisha watu na kuwataka kufuatilia namba, lakini hadi sasa hawajazipata, na wametakiwa kujiandikisha upya kwa kwenda wilayani.

Maana yake ni kuwa mwananchi anatakiwa kuwa na nauli na muda wa siku nzima kujiandikisha kwa ajili ya kupata namba itakayomwezesha kupata kitambulisho.

Takwimu za mara ya mwisho zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zilionyesha kuwa zaidi ya watu milioni 22, hawajajiandikisha, ambayo ni kubwa na inatoa sura halisi ya hali itakavyokuwa hadi kufika Jumatatu ambayo ndiyo mwisho.

Hakuna ubishi kuwa wapo waliokuwa na vitambulisho vya zamani na namba ambao walitakiwa kuvibadilisha, hivyo kuanza mchakato upya, lakini uhaba wa vifaa kwa Nida umekuwa changamoto kubwa.
Mathalani, katika kituo cha Kawe jijini Dar es Salaam, kuna msongamano mkubwa wa watu na vifaa vilivyopo kwenye kupiga picha na kuchukua alama ni vya watu watano pekee kwa wakati mmoja.

Iwapo wengi wataachwa bila kujiandikisha maana yake ni harasa kwa serikali, taasisi za fedha, kampuni za simu na mtu mmoja mmoja kwa kuwa hawataweza kufanya miamala kwa njia ya kielektroniki.

Kila dakika kuna miamala ya simu inayotumwa na kupokelewa na watumiaji ambao hutuma fedha kwa simu, simu kwenda benki, kutoka benki kwenda kwenye simu, kuhamisha akaunti moja kwenda nyingine, au kulipa malipo ya serikali.

Kote huko serikali inapata fedha ambazo ni kodi mbalimbali, sasa kwa watu milioni 22 kuachwa nje maana yake kuna hasara itakayopatikana kwa muda ambao watu watakuwa wanasubiri vitambulisho vya Taifa.

Kwa msingi huo, upo umuhimu wa kufanyika tathmini ya hadi Jumatatu kisha kufanya uamuzi wa kuongeza muda wa mwisho kwa Nida kuharakisha upatikanaji wa namba za utaifa ili watu wajisajili.

Kimsingi, hakuna tatizo kwenye kusajili laini kwa kuwa haichukui hata dakika tatu kukamilika, lakini tatizo lipo kwenye kupata namba za utaifa ambazo watu wanazisotea kuanzia asubuhi hadi jioni na bado hawafanikiwi.

Naamini mamlaka zikiwasiliana vizuri na kujiridhisha na taarifa za wahusika, wataweza kutoa namba haraka, ikiwamo kuwa na mfumo wa kutuma ujumbe mfupi kwa wahusika ili waende wakachukue namba zao.

Faida za kiuchumi ni nyingi zaidi kwa kuwa athari zitajitokeza kwa watu binafsi, taasisi binafsi na serikali yenyewe kutokana na ukuaji wa kasi wa sekta ya fedha kwa njia yakielektroniki.