Muhimu kuwapo sheria inayobana watoto wasiolea wazazi makusudi

14May 2021
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Muhimu kuwapo sheria inayobana watoto wasiolea wazazi makusudi

KILA anayeletwa duniani, ni zao la wazazi wawili. Hivyo, hao waliochangia uzazi huo, wana wajibu wa msingi kuwalea kwa nafasi yote.

Hata hivyo, kumekuwapo baadhi ya watu wasiokuwa tayari kutimiza hilo la malezi, katika sura ya pili pale wazazi wanapofika hatua sasa nao wamechoka kiafya, hawamudu tena badala ya kubeba jukumu kuwachukua na kuwasaidia kuwahudumia, eti wanathubutu kuwapeleka katika kambi ya malezi.

Kutokana na watu kushindwa kuwalea wazazi wao ambao wameshakuwa wazee sasa, wanaomba sheria zitungwe, ili wachukuliwe hatua watoto wao wenye uwezo wa kuhudumia wazazi, lakini wanawatekeleza.

Walesi Mwakikalo ni Mwenyekiti wa Wazee Kinondoni, anasema kuwa wao kutunzwa katika kambi ni kosa na haifai bali wanatakiwa kutunzwa na hata kujengewa nyumba au kulelewa na familia zao.

Anasema, tabia ya kubeba utamaduni wa kuwaweka wazee kambini na kuwaacha walelewa huko, si njema sana.

Anasema wazee wanaoishi kambini wanakuwa mara nyingi wanasumbuliwa na maradhi kama ya ukoma, upofu na matende.

Pia cha ajabu ni kwamba, kuna watu wanawapeleka hata wazee wasiokuwa na matatizo ya kiafya, katika makazi yao, eti kisa wamezeeka wakasaidiwe huko. Hiyo siyo sahihi hata kidogo.

Anasema, hadi sasa inafaa sheria zitungwe na ikiwezekana kuwapo namna ya kushinikiza watoto kugharamia matunzo ya wazazi, hata kupitia mishahara yao hao walioko kazini.

Ni mtazamo chanya kuungana mkono na Mzee Walesi, anayemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kukutana nao na kujenga hoja chanya ya kuwasaidia.

Msingi mara zote, chanzo cha watoto kushindwa kufuatilia mmomonyoko wa maadili na hata wasiwasaidie wazee wao waliowazaaa, kuwasomesha, lakini bado kunachosikitisha mzazi asipompeleka mtoto shule, anachukuliwa hatua.

Mtoto akishindwa kumlea mzee, naye hachukuliwi hatua na hakuna sheria stahiki inayosimamia hilo kokote. Tujiulize, kama mzazi asipompeleka mtoto shule anachukuliwa hatua gani? Inajulikana kote, hatua kali huwa zinafuata.

Niliwasikia wazee hao katika siku yao kwa hatua kubwa wakiishukuru serikali kuwajali, hata wanapoenda hospitali wanapata matibabu stahiki, ingawa katika sura ya pili kunashuhudiwa hasa katika kupatikana vipimo na dawa pasipo pesa wanakwama.

Pia namkumbuka Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Sakumu Matibwa, anasema kuwa jamii wajibu wao ni kuleta fadhila kwa wazazi.

Anasema, mmomonyoko wa maadili umechangia vijana kutokea wazee wanalalamika kutekelezwa na watoto wao, akifafanua: "Nchi za Ulaya Wazee kuishi kambini ni sawa lakini sio Tanzania."

Matibwa anaongeza makambi yanatakiwa yawahudumie wazee ambao hawajabahatika kuoa wa kuwa na watoto na sio, katika kambi anapelekwa mtu aliye na watoto.

Anasema, wapo baadhi ya vijana wanawatelekeza wazazi wao kutokana na kuishi mataifa ya Ulaya na kuoa huko na kushindwa kurudi kuwasaidia wazazi wao.

Matibwa anasema wazee wana sifa kuu tatu kusinzia, unafahamu na gadhabu, sasa wakiyafanya hayo wasilaumiwe na kushindwa kuwasaidia wazazi.

Wazee wanaathirika, pale alipokuwa na kazi na akistaafu anapewa mafao na kuoa nyumba ndogo, hapo unakuta changamoto inatokea na watoto kumchukia baba.

"Watoto wanatakiwa kuwa karibu na wazazi, hata anapopata kiinua mgongo, anasaidia utunzaji fedha na ikiwezekana anajengewa nyumba ili imsaidie," anasema.

Msingi wa hoja ni kwamba, watoto wanapowatunza wazazi wao, inasaidia hata serikali kupunguza gharama za kuwalea wazee na kuwajengea nyumba za kuwatunza.

Ushauri mkuu ni wazee watunzwe nyumbani kwao, kwa kuwa ni hatua yenye faida yake, mojawapo akiitaja kuwa ni mzee huyo kuwa mlezi wa familia na hata mjukuu wake atakuwa anamwangalia vyema, kwa msaada wa ushirikiano wa dada wa kazi au vinginevyo.