Muhimu kwa wacheza kandanda

15Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Muhimu kwa wacheza kandanda

MPIRA ni kitu cha mviringo kilichotengenezwa kwa mpira kwa ajili ya michezo; mchezo unaotumia kifaa kilichotengenezwa kwa mpira. Mpira wa miguu una majina mengi; kandanda, kabumbu, soka.

 

 

 

Mingine ni mpira wa pete, mpira wa wavu na mpira wa magongo.

     Zamani, kandanda ulikuwa mchezo wa kuwapa mazoezi wachezaji na wakati huo huo kuwaburudisha watazamaji. Wachezaji hawakulipwa hela kwani watazamaji waliingia viwanjani bure kufurahia mchezo huo.

     Sasa mambo ni tofauti kwani mchezo wa kabumbu ni kazi kama zingine na wachezaji hulipwa mishahara, tena mikubwa kuliko hata wanaofanya kazi walizozisomea! Naam, “kila zama na kitabu chake.”   

Kuna methali isemayo “Kipendacho moyo ni dawa” kwamba kitu anachokipenda mtu au inachokipenda roho ya mtu huwa ni kama dawa yake. Methali hii hutumiwa kumpigia mfano mtu anayeelekea kukipenda kitu fulani sana ingawa wengine wanakiona kuwa cha kawaida au kibaya.

     Hata kwenye kabumbu kuna baadhi ya wachezaji mahiri wanaovipenda mno vilabu vyao kiasi cha kutotaka kujitafutia hela zaidi kwenye vilabu vingine, ndani au nnje ya nchi. Labda baadhi yao huogopa kwenda nnje ya nchi kwa kutojua lugha ngeni. Hawapaswi kuogopa kwani tatizo hilo waiachie miguu yao ndiyo itakayozungumza.

     “Maendeleo” kwa muktadha ninaoujadili ni tendo la kutoka kwenye kiwango kidogo cha ufanisi na kufika kwenye kiwango kikubwa. Pia ni ongezeko la ubora katika huduma za kijamii kama vile elimu, uchumi, afya bora, mawasiliano n.k.

     Hakuna asiyejua kuwa fedha, (pesa, hela au fulusi) ni sarafu inayotumika kulipia huduma mbalimbali zinazohusu maisha ya binadamu. Ndivyo wanavyotakiwa kujua baadhi ya wachezaji wetu wa kandanda wanaong’ang’ania kwenye vilabu vya nchini kwa kuvipenda mno badala ya kufikiria maisha ya kesho.

     Mikataba ya wachezaji isiwe na upendeleo unaoegemea upande mmoja tu, yaani vilabu wanavyojiunga navyo au kuongeza mikataba baada ya awali kufikia ukomo. Wachezaji wanapaswa kuwa na wanasheria wa kutafsiri maana ya mikataba yao ili wasipunjwe masilahi yao au kubanwa na vilabu wanavyojiunga navyo.

     Masilahi hayo ni mishahara itakayokubaliwa na pande zote mbili, kulipwa kwa wakati kwa kuwekewa kwenye akaunti zao za benki bila ubabaishaji kama ilivyo sasa. Ili kutimiza masharti hayo, wachezaji wawe na chama chao kitakachoendeshwa na wachezaji wastaafu kwani ndiwo wanaojua matatizo na stahiki za wachezaji. Kuwe na mwanasheria atakayesimamia mikataba ya wachezaji na vilabu.

     Katika mikataba hiyo kuwe na kigezo (kielelezo, kipimo maalumu cha kufuatwa; sheria inayoongoza kutolewa uamuzi) kinachowapa wachezaji uhuru kujiunga na vilabu vingine vitakavyowapa masilahi mazuri zaidi. Mchezaji atakayeitumikia klabu yake kwa bidii, nidhamu na mafanikio apewe tuzo ya aina fulani na ikiwezekana aongezwe mshahara.

     Aidha, vilabu viwekewe masharti ya matumizi ya fedha kwamba kila kinachonunuliwa kiwe na risiti inayothibitisha manunuzi. Kwa ufupi ni kwamba kila hela inayotoka klabuni iwe kwenye maandishi na ukaguzi ufanywe na wakaguzi wasiokuwa na tamaa ya hela ili wafanye kaguzi zao kwa haki bila ghiliba (udanganyifu wenye nia ya kujinufaisha).

     Imebidi nitahadharishe mapema kwani baadhi ya viongozi hugombea nafasi hizo ili kujinufaisha kwa fedha za vilabu. Mfano mzuri ni kesi zilizo mahakamani inayowahusu waliokuwa viongozi wa chama kile kikuu kama ilivyo klabu fulani (nimesahau majina yao)!

Habari zisizo rasmi zaeleza kuwa kuna baadhi ya viongozi waliojenga nyumba kwa fedha za chama au vilabu vya mpira wanavyoviongoza. Ndio maana ‘huwanunua’ watu wa kuwafanyia kampeni kabla ya uchaguzi!

Hao wanaofanya hivyo, watafakari kwa kusoma methali hii: “Penye urembo ndipo penye ulimbo.” Mahali penye urembo huwa pana mtego unaoweza kukunasa. Methali hii hutumiwa kumnasihi mtu asikiendee kitu fulani kwa pupa kwa kuwa kinamvutia kwa sababu huenda kikawa na madhara fulani baadaye. Hutukumbusha umuhimu wa kuvichunguza vitu kwanza.

Vilevile vilabu vyapaswa kuwakumbuka wachezaji wao waliostaafu wanapopata maradhi hata kutoweza kujitibu. Kuna wachezaji wengi wa vilabu vikubwa nchini, hasa vya Simba na Yanga walioviletea vilabu hivyo sifa kubwa ndani na nje ya nchi, lakini sasa hawathaminiwi wala kukumbukwa! Au ndio yale yasemwayo “yaliyopita yamepita?”

“Asante tupu haijazi chungu.” Shukrani au asante isiyo na kitu haijazi chungu. Tuwafariji waliofikwa na maafa fulani kwa vitendo wala sio maneno matupu tu.

[email protected]

0784  334 096