Muhimu kwa wacheza kandanda

29Feb 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Muhimu kwa wacheza kandanda

MPIRA ni kitu cha mviringo kilichotengenezwa kwa ngozi kwa ajili ya michezo; mchezo unaotumia kifaa kilichotengenezwa kwa mpira. Mpira wa miguu una majina mengi: kandanda, kabumbu, soka. Mingine ni  mpira wa pete, mpira wa wavu na mpira wa magongo.

Maana ya pili ya ‘mpira’ ni mti mkubwa kiasi wenye majani mapana yaliyogawanyika unaotoa utomvu unaotengeneza vitu vya mpira.

     Zamani, kandanda ulikuwa mchezo wa kuwapa mazoezi wachezaji na wakati huohuo kuwaburudisha watazamaji. Wachezaji hawakulipwa hela kwani watazamaji waliingia viwanjani bure kufurahia mchezo huo.

     Sasa mambo ni tofauti kwani mchezo wa kabumbu ni kazi na wachezaji hulipwa mishahara, tena mikubwa kuliko hata wanaofanya kazi walizosomea! Naam, “kila zama na kitabu chake,” chambilecho wazungu.

     Kuna methali isemayo “Kipendacho moyo ni dawa” kwamba kitu anachokipenda mtu au inachokipenda roho ya mtu huwa ni kama dawa yake. Methali hii hutumiwa kumpigia mfano mtu anayeelekea kukipenda kitu fulani sana ingawa wengine wanakiona kuwa cha kawaida au kibaya.

     Hata kwenye kabumbu kuna baadhi ya wachezaji mahiri wanaovipenda mno vilabu vyao kiasi cha kutotaka kujitafutia hela zaidi kwenye vilabu vingine, ndani au nje ya nchi. Labda baadhi yao huogopa kwenda nje ya nchi kwa kutojua lugha ngeni. Hawapaswi kuogopa kwani tatizo hilo waiachie miguu yao ndiyo itakayozungumza.

     Masilahi hayo ni mishahara itakayokubaliwa na pande zote mbili, kulipwa kwa wakati kwa kuwekewa kwenye akaunti zao za benki bila ubabaishaji kama ilivyo sasa. Ili kutimiza masharti hayo, wachezaji wawe na chama chao kitakachoendeshwa na wachezaji wastaafu kwani ndiwo wanaojua matatizo na stahiki za wachezaji. Kuwe na mwanasheria atakayesimamia mikataba ya wachezaji na vilabu.

     Katika mikataba hiyo kuwe na kigezo (kielelezo, kipimo maalumu cha kufuatwa; sheria inayoongoza kutolewa uamuzi) kinachowapa wachezaji uhuru wa kujiunga na vilabu vingine vitakavyowapa masilahi mazuri zaidi. Mchezaji atakayeitumikia klabu yake kwa bidii, nidhamu na mafanikio apewe tuzo ya aina fulani na ikiwezekana aongezwe mshahara.

     Atakayefanya kinyume, kama kutokuwa na nidhamu uwanjani kwa kuoneshwa kadi iwe ya njano au nyekundu mara kwa mara, ama nje ya uwanja kwa kushiriki ulevi, uvutaji sigara, dawa za kuongeza nguvu, uasherati n.k. apewe onyo la kwanza na akiendelea apewe la pili na la tatu afukuzwe na kulipwa masilahi yake yote.

     Kadhalika mchezaji asilazimishwe kushiriki vitendo vya ushirikina iwe ndani, nnje au viwanjani. Kama hataki kwa sababu ya kumwamini Mungu wake, asichukiwe wala kuadhibiwa kwa kukomolewa (kumfanyia tendo la kumsumbua au kumuumiza) kwa namna moja au nyingine. Awe huru kukubali au kukataa, kwa mujibu wa imani yake.

     Aidha vilabu viwekewe masharti ya matumizi ya fedha kwamba kila kinachonunuliwa kiwe na risiti inayothibitisha ununuzi. Kwa ufupi, kila hela inayotoka klabuni iwe kwenye maandishi na ukaguzi ufanywe na wakaguzi wasiokuwa na tamaa ya hela ili wafanye kazi yao kwa haki bila ghiliba (udanganyifu wenye nia ya kujinufaisha).

     Wahenga hunishangaza sana kwa methali zao. Kwa mfano walisema: “Mtaka cha mvunguni sharti ainame.” Maana yake anayekitaka kitu kilicho mvunguni mwa kitanda lazima ainame ndipo aweze kukichukua. Hii ni methali ya kutukumbusha kwamba tukitakapo kitu lazima tuwe tayari kukifanyia kazi au kukisumbukia. Kumbe ndo maana chaguzi zote husumbukiwa kwa hali na mali usiku na mchana!

Vilevile vilabu vyapaswa kuwakumbuka wachezaji wao waliostaafu wanapopata maradhi hata kutoweza kujitibu. Kuna wachezaji wengi wa vilabu vikubwa nchini, hasa vya Simba na Yanga walioviletea vilabu hivyo sifa kubwa ndani na nnje ya nchi lakini sasa hawathaminiwi wala kukumbukwa! Au ndio kile kisemwacho “Yaliyopita si ndwele ganga yajayo”?

“Asante tupu haijazi chungu.” Shukrani au asante isiyo na kitu haijazi chungu. Tuwafariji waliofikwa na maafa fulani kwa vitendo wala sio maneno matupu tu.

[email protected]

0784  334 096