Mvua hizi, kanuni zake kujihami nazo hizi hapa

02Jan 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mvua hizi, kanuni zake kujihami nazo hizi hapa

NI msimu wa mvua ambao mikoa mbalimbali nchini, zinanyesha na kusababisha aina mbalimbali ya mafuriko, japo sura ya pili ina neema zake. Sote tunajua ‘maji ni uhai.’

Ushahidi wa jumla ni kwamba, katika maeneo mbalimbali mtu anakopita anakutana na adha za mvua mito kupanuka, majengo kuathiriwa na athari hizo.

Kunaponyesha mvua, baadhi ya watu katika jamii wanashindwa kutumia ustaarabu kukabili mvua hizo na mvua hizo hutumika kutiririsha maji machafu.

Shida mojawapo inayojitokeza ni baadhi ya watu hugeuza mvua na maji yake mbadala wa kushughulikia athari zao, wakitiririsha maji machafu ya vyooni kupitia maji yaliyojaa.

Hapo ndipo shida inaanza, kwani maji machafu yanatiririka katika makazi ya umma jirani. Kuna sehemu yanaingia kwenye bustani za mboga zinazodhaniwa kuwa mlo wa umma.

Simulizi inayofuata baada ya hapo, ni kushuhudia magonjwa ya milipuko, kwani maji machafu yana mengi. Mtu anapoyakanyaga tu, anaweza kupata magonjwa ya kuambukiza kama vile fangasi na ndio mwanzo wa matatizo kama maradhi ya ngozi.

Hivyo basi, jamii inatakiwa kuwa makini kupitia mvua hizo kijihami kuzingatia suala la afya ya umma.

Hivi karibuni imeelezwa kuwa Watanzania hususani wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wamehimizwa kuzingatia kanuni za afya na usafi wa mazingira, hasa katika kipindi kilichopo cha msimu wa mvua za masika, waepuke magonjwa mbalimbali.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi, anasema Watanzania wanatakiwa kujua hiki kilichopo ni msimu wa mvua kubwa, katika maeneo mbalimbali kitaifa.

Ingawaje ni neema, lakini wakati mwingine inakuwa adha, inapoangaliwa katika mtazamo wa kiafya, mwenyewe akitamka: "Tunakuwa na maji mengi, tunakuwa na mafuriko, kwa hiyo tuendelee kuzingatia kanuni za afya katika maeneo yetu."

Anatoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam, kwamba lilikumbwa na mlipuko wa homa ya dengue na serikali ikachukua hatua ya kuidhibiti kwa nguvu zote, hivyo madhara ya mvua nayo yanapaswa kudhibitiwa, mosi kwa kuizingatia kanuni zilizopo za afya.

Dk. Subi anaongeza kuwa eneo wanaoliona limezungukwa na maji, wanapaswa kuendelea kutumia dawa, kulala kwa kutumia vyandarua, kufukia madimbwi ya maji na kuondoa vifuu vya nazi, tena bila ya kuruhusu uwepo wa mazalia ya mbu.

Anashauri sheria zichukuliwe, kwa wote watakaobainika kutiririsha maji katika kipindi cha mvua zinaponyesha na kwa wananchi kuhakikisha matumizi ya maji yawe ya kunywa, kunawa mikono au kuoshea vyombo ni yaliyochemshwa, lengo ni kuhakikisha wadudu waenezao magonjwa wanakufa.

"Hivyo, pamoja na kwamba upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam umeimarika hadi kufikia asilimia 85, bado kuna ile asilimia 15," anasema.

Anashauri jamii kuendelea kuhakikisha wanatumia maji safi na salama, muhimu wachemshe maji ya kunywa, wakiona hawawezi basi watumie dawa aina ya ‘chlorine’ na ‘water guard’ ambazo ni nzuri katika maeneo yao, huku wakinawa mikono hasa kabla ya kula chakula.

"Hizi ni baadhi ya kanuni za afya ambazo tunahimiza wananchi waendelee kuzizingatia, tuna uwezo kabisa wa kupambana na maradhi. Tumetolewa pia wito kama unakaa kwenye mabonde hama, serikali imetoa wito kwa wananchi wote.

“Wale ambao wanakaa kwenye maeneo hatarishi kuhama, kwa sababu ni hatarishi kwa afya lakini pia ni hatarishi kwa maisha yao na familia zao," anasema kiongozi huyo wa afya .

Mwisho, anatoa rai kwa jamii kuwalinda watoto, walemavu na wagonjwa ambao wanataabika, katika suala la usafi wa ndani ya nyumba, kwa kupuliza dawa za mbu ili kujikinga.