Mvua hizi zitufunze jambo

16May 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mvua hizi zitufunze jambo

SOTE tunakubaliana kuwa mvua ni baraka kwetu sote na kila inaponyesha, wapo wengi wanaofurahi kutokana kupata maji, ambayo yana matumizi mengi kupita kiasi; nyumbani, shambani na sehemu za uzalishaji kama vile viwandani.

Mvua hiyo inaponyesha, baadhi ya watu wanaifafanua kiimani zaidi, zaidi ya mtazamo wa kiikolojia iliyozoeleka, wakitamka: “Ni Baraka Kutoka kwa Mwenyezi Mungu.”

 

Ni ufafanuzi unaoenda mbali katika lugha ya ushuhuda kwamba, kila mvua zinapogoma au kuchelewa kunyesha, viongozi wa dini hushirikishwa kupitia nguvu ya maombi yao, ili mvua zinyeshe na kufakikisha kupunguza joto, upatikanaji maji na mazao yanusurike.

 

Mvua zinapopatikana, mara moja neema zinazoambatana nazo hushuhudiwa. Lakini, katika upande wa pili wa shilingi ambao kidole changu kinaelekeza, kuna tabia zisizofaa kutokana na mvua hizo. 

 

Hapo ninajielekeza mijini, tena nikisonga kule kunakojulikana ‘Uswahilini.’ Hapo ndipo kunapotokea ushuhuda wa yasiyo ya kistaarabu, kwa maana ya maji machafu kutoka katika yaliyo na vinyesi.

 

Pia tumeona, mvua hizi ziliponyesha katika baadhi ya mikoa. Zimeleta changamoto kuanzia uharibifu wa miundombinu ya umma, makazi na adha kubwa kwa jamii.

 

Nikiamua kuwa mahsusi kwa jiji la Dar es Salaam, nako kuna adha yake kubwa. Mvua imeleta changamoto kubwa kwa wakazi wake.

 

Sote tulioko jijini tumeona namna baadhi ya miundombinu ya barabara imekuwa haipitiki na kukatika kwa mawasiliano kuingia upande mwingine.

 

Katika barabara ya Morogoro ambayo ni kubwa na muhimu ndani ya jiji, tumeona mawasiliano ya kuingia mjini, yaani katika maeneo kama Posta, Mnazi Mmoja na Kariakoo.

 

Hali haikuwa nafuu hata kidogo, magari kutoka nje ya mji, yalikuwa yanaishia Magomeni Mapipa na hapo abiria kia mmoja kwa mikakati yake binafsi, alilazimka kujipanga namna atavyofika aendako huko mjini.

 

Ndipo inakuja simulizi ya baadhi ya watu kulazimika kupada usafiri wa baiskeli za magurudumu matatu, maarufu Gutta wavushwe kwa kwenye maji mengi kwa tozo la nauli kati ya Sh. 500 hadi 1000, wakielekea kama Posta, Kariakoo na kwingineko, baadhi wakiwa na safari ya mbali zaidi kufikia maeneo kama Kigamboni.

 

Hapo mabasi ya huduma za Mwendokasi, yanayotegemewa sana na wakazi wa Barabara ya Morogoro kati ya Mbezi na Mjini na Barabara ya Bibi Titi, kati ya eneo la Kinondoni Morocco na Magomeni, huduma hiyo kwao ilisitishwa.

 

Sababu iko wazi, miundombinu na hasa iliko daraja la Jangwani, kulifurika maji na athari zisambaaa, zikiwamo shule kufunga kwa muda.

 

Kuna shule nazo ziliguswa moja kwa moja, baadhi ya madarasa yalijaa maji, walimu na wanafunzi wakashindwa kuhudhuria vipindi, kwa mujibu wa taratibu na ratiba zao.

 

Kimsingi, mvua hizo zinaponyesha tumeona hata baadhi ya watu wanazibua majitaka, pasipo kujali afya za watoto wanaocheza, wapita njia, wakazi jirani na wengine ambao kwa njia moja au nyingine ni wahusika.

 

Katika kipindi hicho cha mvua, tumeona magari madogo yanazimika, pindi yanapopita katika madimbwi ya maji hayo, hapo inazuka kero ya foleni barabarani.

 

Sasa, kutoka na mvua hizi ambazo hazijaisha, jamii tunatakiwa kujifunza kitu.Wahusika wasimamizi wa miundombinu husika, wanapaswa kuzitumia changamoto hizo kwa kuboresha miundombinu, ili kuwapunguzia kero kutoka kwa wananchi.

 

Kwa sasa, barabara za mitaani hazipitiki. Mashimo yamekuwa mengi, pia baadhi ya masoko kwa sasa yamejaa tope na hata watu kuingia sokoni, unatakiwa kuvaa mabuti kutokana na kuwapo na tope jingi na uchafu wa kila namna.