Mwanafunzi wa leo anakumbushwa kujiandalia ratiba nyumbani, shuleni

11May 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mwanafunzi wa leo anakumbushwa kujiandalia ratiba nyumbani, shuleni

KUTENGA muda wa kujisomea ni miongoni mwa njia zinazoweza kumsaidia mwanafunzi kujiandaa na kufanya vizuri katika masomo na mitihani yake bila kujali anasoma katika kiwango gani.

Ili kufanikisha hilo, ratiba hiyo inatakiwa kuandaa utaratibu na mikakati ya kujisomea kuanzia nyumbani hadi shuleni na hata wakati wa mapumziko na likizo za mihula.

Kimsingi, ratiba ina nafasi kubwa ya kumsaidia mwanafunzi kufikia malengo yake ya kufaulu, hivyo ni vyema aipange ili kujisomea huku akifuata ratiba yake ya darasani.

Kwa ujumla kupanga ratiba ni muhimu na ni utaratibu unaotakiwa kufuatwa na mwanafunzi, wazazi na walezi ili waweze kuitekeleza inavyotakiwa, kwa lengo la kumsaidia kutimiza malengo yake.

Iwapo kila mwanafunzi atajiwekea ratiba ya kujisomea nyumbani huku wazazi nao hawapi kazi nyingi au majukumu mengine, itakuwa rahisi kufanya vizuri darasani, kwa kuwa atakuwa ameshafanya mapitio mengi.

Kwa kujali umuhimu huo wa kutenga muda wa kujisomea, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, anawaomba wazazi na walezi kuwapunguzia kazi watoto wao wanaojiandaa na mitihani ili waweze kujisomea.

Mtaka anatoa rai kwa wazazi na walezi wenye watoto walio katika madarasa ya mitihani ya taifa kuwapunguzia kazi ili wanafunzi hao waweze kupata muda wa kujiandaa na akizungumza wiki iliyopita mjini Bariadi wakati wa futari maalum iliyoandaliwa na ofisi yake kwa ajili ya Waislamu waliofunga Ramadhani.

Matarajio ya mkuu huyo wa mkoa ni kuhakikisha Simiyu inabaki kuwa miongoni mwa mikoa mitano inayofanya vizuri katika elimu nchini, huku malengo ya mwaka huu ikiwa ni kuona wanatoka kwenye nafasi ya tano.

Wanatamani kuwa nafasi ya tatu na kufikia nafasi ya kwanza, hivyo anawaomba wazazi na walezi wote wa mkoa wa Simiyu wenye watoto wa madarasa ya mitihani wawapunguzie kazi ili wapate muda wa kujisomea na kufanya matayarisho ya mitihani yao ya taifa.

Anawataka wazazi kutowaruhusu wanafunzi kwenda katika minada kufanya biashara badala yake wahakikishe wanafunzi wote wanahudhuria masomo, ili kuendelea kuinua mkoa huo kielimu.

Kinachofanywa na mkoa huo, ni mfano wa kuigwa ili kusaidia kuongeza ufaulu, hasa kwa kutambua kuwa si rahisi mwanafunzi kufanya vizuri darasani au katika mitihani bila kupata muda wa kutosha wa kujisomea.

Wanafunzi wanawajibu wa kusaidia kufanya shughuli za nyumbani, lakini shughuli hizo zisiwabane hadi wakose nafasi ya kujisomea, bali wapunguziwe kazi ili iwe rahisi kuwa na ratiba ya kujisomea.

Suala hilo liko ndani ya uwezo wa wazazi na walezi na ndiyo maana mkuu wa mkoa amewaomba kuzingatia hilo, hasa kwa kuzingatia kwamba mitihani ya taifa iko karibu kuanza kufanyika, hasa kwa wanafunzi wa darasa la saba.

Lakini, pamoja na hayo kuwa na ratiba ya kujisomea isiwe kwa wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani tu bali uwe ni utaratibu wa kawaida kwa lengo la kuwajengea uelewa zaidi wa masomo mbalimbali.

Njia hiyo pia inamwezesha mwanafunzi kuwa na uwezo wa kuuliza maswali mbalimbali yanayohusu mada zilizopita pale mwalimu akifika darasani wakati akikumbushia yale yaliyofundishwa kwenye vipindi vilivyotangulia au iwapo akiuliza kuna mtu hakuelewa somo lililopita mwenye ratiba na anayeifuatilia anapata nafasi ya kuuliza aliyoyabaini.

Hivyo, mwanafunzi kuwa na ratiba ya kujisomea nyumbani ni muhimu, lakini itakuwa matokeo mazuri kama ataheshimiwa na wote kuanzia wazazi na walezi pamoja na mhusika.

Ikumbukwe yote hayo yatafanikiwa kama walezi na wazazi wataacha kumpa majukumu mengi yanayomkosesha muda wa kujisomea.