Mwanamke anatakiwa abaki kuwa mwanamke

10May 2016
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Mwanamke anatakiwa abaki kuwa mwanamke

TAARIFA za utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na kubakwa kwa wasichana na askari wa jeshi la serikali ya Sudani Kusini na baadaye kulazimishwa kuingia kwenye makazi yao na nyumba zikachomwa moto huku wasichana hao wakiwa humo ndani, hai, wakatekea zinagaa kutazamwa kwa makini.

Ni kitendo kinachotakiwa kulaaniwa. Kinahitaji kulaaniwa kwa sababu sio tu kuwa wanawake wanabakwa katika mazingira ya vita, bali hata katika mazingira mengine ili mradi tu wanaume waone kuwa kuna fursa ya kujibadilisha kuwa wanyama.

Wanajeshi hao, walitaka kuficha siri lakini dhambi waliyoifanya ni kubwa sana na Mungu ameifichua. Najiuliza kila siku kwa nini mwili wa mwanamke utumike kama chombo cha kulipiza kisasi.

Kwa nini kubaka kuwa ni sehemu ya mikakati ya vita? Vita mara nyingi huanzishwa na wanaume kwa ajili ya kutetea maslahi yao, dhidi ya wanaume wanzao.

Vita vya waasi iliyoongozwa na Riek Machar dhidi ya Serikali ya Salva Kiir ni baina ya wanaume.

Wanawake na watoto na wanaume wengine raia wa kawaida ambao wengi hawajui vita hivyo vilianzaje na kwa maslahi ya nani ni waathirika tu.

Wanawake katika kipindi cha vita aghalabu huteseka sana na huwa ndio mihimili ya kisaikolojia, ya afya na chakula kwa ajili ya watoto, wanaume na wazee au wengine wasiojiweza kwa namna moja au nyingine.

Huu huwa ni mzigo mkubwa sana kwa wanawake kwa sababu maisha wakati wa vita huwa ni magumu.

Maji huwa shida kupatikana na bei hupanda kwa kila aina ya mahitaji, na fedha nazo wakati wa vita huwa hazipatikani kwa urahisi zaidi. Wanawake hutegemea akiba waliyojiwekea au ubunifu wakati mwingine.

Lakini wanaume, nazungumzia wanajeshi na wasio wanajeshi, wanapoiona hali hii ya wanawake kukosa ulinzi kutoka kwa wanaume wao (wazazi, kaka na ndugu wa karibu) au kwa jamii zao huwa sio karibu na wanawake wakati wa vita na vurugu, wanaume wabakaji huichukulia hiyo kama fursa ya kutekeleza nia zao ovu.

Na wanajeshi wanapofika mahala ambapo hawawezi kupingwa, kinyume na ada za kijamii, kinyume na sheria za nchi na matamko na mikataba ya kimataifa, wanaamua kuwabaka wanawake.

Na wakati mwingine watoto na wasichana ambao hawajafikia hata umri wa kufanya ngono. Ni kitu gani kinawafanya wanajeshi kushusha utu wao kiasi hiki na kuamua kufanya zinaa kinyume na matakwa ya kiutu. Kwa nini wanaume waone kuwa panapotokea wanawake kuwa peke yao na hawana ulinzi, wanachoweza kukifanya ni kulazimisha ngono?.

Imekatazwa katika mikataba ya kimataifa, kwa mfano, mtu akishakamatwa mateka, hata kama ni mwanajeshi, hairuhusiwi kupigwa risasi, anatakiwa kupatiwa matibabu, chakula na kila hitaji la kibinadamu, na anatakiwa hatimaye atangenezewe mazingira ya kurudishwa kwao.

Au afungwe katika jela baada ya kushitakiwa katika mahakama halali, kama hilo ndilo linalohitajika kutegemea na mazingira.

Sasa kama mwanajeshi aliyekuwa akipigana vita na kuua adui anatakiwa kuheshimiwa hivi akikamatwa na wapinzani wake, inakuwaje sasa wasio wanajeshi, na hasa wanawake, wafanyiwe kinyume na mikataba ya kimataifa?.

Ngono haiwezi kuwa silaha ya vita, au mwili wa mwanamke hauwezi kutumika kutoa adhabu kwa niaba ya maadui.

Mwanamke anatakiwa kubaki mwanamke, na sio sehemu ya jeshi la adui wakati wa vita. Wanawake wanapaswa kuachwa huru, na hata kama ni mwanajeshi na amekamatwa kama mateka bado hakuna uhalali wowote wa yeye kubakwa.

Ni kinyume na haki za binadamu na tendo la kuushusha utu wake na wewe unayebaka. Kitendo kilichofanywa huko Sudani Kusini ni lazima kilaumiwe.