Mwanzo msimu korosho, RC Pwani atutia moyo

01Nov 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mwanzo msimu korosho, RC Pwani atutia moyo

KOROSHO ni zao linalouongezea mapato mkoa wa Pwani. Ili serikali na wakulima wanufaike nako, kuna kila haja ya hatua kuchukuliwa, kuhakikisha serikali na wakulima wananufaika.

Pamoja na kuonekana mkombozi kwa wakulima na serikali, kuna baadhi ya watu wamekuwa wakilalamikiwa kwamba si waaminifu katika kufanikisha matakwa ya zao hilo na hususan mchakato wa mauzo.

Hiyo ni kwamba, wanakuwa si waaminifu hata kusababisha serikali kujipanga kwa kulisimamia zao hilo, ili iweze kumkomboa mkulima ajiongezee kipato.

Kuna historia ndefu ya kuzalisha zao hilo. Moja ya maeneo ni kuwapo baadhi ya watu kutokuwa waaminifu na kuwafanyia wakulima hujuma nyingi.

Haikuwa jambo jema hata kidogo, katika baadhi ya maeneo kuna wakulima waliopatwa na madhila hata wakaamua kuacha kulima, wakahamia mazao mengine.

Kwetu Pwani, sasa ni mwezi huu wa kuuza korosho. Mtazamo bayana utumike kuliletea taifa mapato, ikiwamo kuwanufaisha wakulima kupitia zao hilo.

Wakulima wamekuwa wakilima korosho na wanapouza wanatarajia kunufaika na zao hilo, mbali ya wakulima kunufaika, pia serikali inatarajia panapouzwa korosho wananufaika kutokana na fedha zinazopatikana kupitia zao hilo.

Hivyo basi, serikali imekuwa ikiwawezesha wakulima pembejeo ili waweze kunufaika na kilimo hicho.

Katika mkoa wa Pwani, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, ameziagiza kamati zote za ulinzi na usalama za wilaya kuwachukulia hatua watu wote watakaogundulika kufanya ubadhirifu kwa wakulima wa korosho.

Anazitaka kamati hizo kumpa taarifa za utekelezaji huo ndani ya siku saba. Ni kauli yake, alipofungua mkutano wa wadau wa korosho Mkoa wa Pwani, uliofanyika wilayani Mkuranga. Jambo zuri sana kwetu wakulima.

Ndikilo anazitaka taasisi zote za fedha zilizoshiriki katika kufanya malipo kwa wakulima wa korosho, kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya ulinzi na usalama za wilaya, ili kubaini kasoro zinazochangia wakulima kutopata fedha zao

Aidha, anaipongeza serikali kufanya malipo kwa wakulima wa korosho kiasi cha Sh. bilioni 47.7 na imebaki Sh. bilioni 18.1, ambazo wakulima hawajalipwa.

Mhandisi Ndikilo, amewahakikishia wakulima wa korosho wa Pwani, kwamba korosho zilizokusanywa na serikali zimeshauzwa na anawataka wawe na subira, wakati serikali inamalizia uhakiki, ili kila mkulima apate fedha zake.

Ni jambo linalochukua sura hiyo mkoani, huku Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga, anasisitiza kwamba hatovifumbia macho vyama vya msingi au viongozi wa vyama watakaoshiriki kufanya ubadhirifu na kurudisha fedha

"Tunataka wakulima wanufaike na zao hilo, yeyote atakayefanya ubadhirifu atachukuliwa hatua kali za kisheria," anasema.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, anasema wao wanaahidi kutoa mafunzo kila kijiji cha mkoa wa Pwani katika zao la korosho, ili kulifanya zao hilo mkoani Pwani linakuwa na ubora kama ilivyo mikoa mingine.

Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Pwani (CORECU), chenyewe kimetakiwa kuandaa magunia mapema kwa ajili ya kujiandaa na msimu unaoanza na wakulima wakitakiwa kutochanganya korosho na michanga au taka zingine.