Mwanzo mtamu, mwisho mchungu

01Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mwanzo mtamu, mwisho mchungu

‘MUA’ ni mmea wenye tindi (kifundo) na majani marefu yenye wage (vumbi linalotokana na mimea au nafaka linalowasha mwilini) na kigogo (sehemu ya mti inayotoa matawi; kipande kinene cha mti kilichokatwa kisichokuwa na majani) chenye maji matamu.

Yasemwa kandanda ni mchezo wa bahati. Kama ni kweli au ni maneno ya mitaani, utaamua mwenyewe msomaji. Nijuacho ni kwamba bidii (ari katika kufanya jambo; idili, juhudi, jitihada) ni muhimu katika utendaji wa jambo lolote ili kupata mafanikio.

 

          Sehemu nyingi za Afrika ‘nyeusi’ timu za kandanda hutawaliwa na imani za kishirikina kuliko kumtumaini Mwenyezi Mungu aliyeumba Mbingu na nchi na vyote vilivyomo, vinavyoonekana na visivyoonekana.

          “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako. Nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, ‘usiogope, mimi nitakusaidia’.” (Isaya 41: 10,13).

          Hata pamoja na ahadi hii nzuri yenye matumaini, binadamu twashindwa kumwamini Mwenyezi Mungu, ndipo anaposema:

“Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, hataona yatakapotokea mema. Bali atakaa jangwani palipo ukame, katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.

“Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto; hautaona hofu wakati wa hari ujapo, bali jani lake litakuwa bichi; wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda.

Natamani kama timu za Afrika zingesoma maandiko hayo na kukataa katakata mambo ya ushirikina. Muhimu ni wachezaji kufanya mazoezi kwa bidii, kufuata maelekezo ya walimu na kukataa katakata (tanakali sauti inayoashiria msisitizo wa tendo la kukataa jambo) ushirikina na kutokuwa watovu wa nidhamu ndani na nnje ya uwanja. Waache pombe, sigara, bangi na dawa za kutia nguvu miili yao.

Yanga ilianza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa utamu na imemaliza mechi ya mwisho mzunguko wa pili kwa uchungu ilipofungwa mabao 2-0 na Azam ambayo mzunguko wa kwanza wachezaji wa Azam FC ndiwo waliotoka uwanjani vichwa chini kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga. Naam, kutesa kwa zamu, chambilecho/chambacho (kama wasemavyo) vijana wa Dar es Salaam.

Wachezaji wengi huanza ligi kwa bidii lakini huharibika baada ya kupewa sifa na mashabiki wa timu zao pamoja na magazeti yanayowasifu kupita kiasi. Ukisoma habari za magazeti yetu ya michezo, mara moja utagundua mwelekeo wa waandishi wetu kwa timu za Simba na Yanga. Huo ni uandishi wa ovyo kabisa unaowapotosha wasomaji.

Mtoto anaposifiwa kwa jambo la kijinga huvimba kichwa akidhani alichofanya ni kizuri kumbe sivyo. Mweleze ukweli wa mambo na kumkosoa kila afanyapo vitendo visivyo vya kiungwana. Kwa kufanya hivyo utakuwa unamfundisha kujua mema na mabaya.

Ukimdekeza mtoto utamharibu na mwishowe aweza kukufedhehesha mbele za watu. Ndo maana wahenga walisema “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.”

Kwa kawaida mtoto hukua jinsi alivyolelewa; akilelewa vibaya ataishia kuwa na tabia mbaya. Methali hii hutumiwa kuwanasihi wazazi wawalee watoto wao vizuri ndipo wainukie kuwa na tabia nzuri na wawe watu waVilevile wachezaji wanaposifiwa sana hufura vichwa kwa dhana kuwa wao ni wao kumbe wanaifanya Tanzania kutokuwa na wachezaji mahiri.

Badala yake twategemea wachezaji kutoka nchi za nnje ambao wengi wao hawapati nafasi kwenye timu za mataifa yao hivyo huamua kuja ‘kuganga njaa’ Tanzania.

  Wakati huu wa usajili, mengi yasemwa na yataendelea kusemwa na wanachama na mashabiki wa timu mbalimbali. Viongozi wa Simba na Yanga wanasema kwa mbwembwe na majivuno (hali ya kujiona bora zaidi kuliko wengine) kuwa watawasajili wachezaji kutoka klabu yoyote na popote. Nisomapo habari hizo ambazo nyingine ni za ubabaishaji, huwa najiuliza: “Kwa nini timu hizo kongwe hazisajili kwa siri na utulivu?”

Kwa upande mwingine, timu zote za Ligi Kuu ya Bara zapaswa kutangaza mapema majina ya wachezaji watakaoachwa ili wajitafutie timu watakazojiunga nazo msimu mpya. Huu mpango wa kuwatangaza mwishoni mwishoni ni kuwanyima riziki na nafasi zao kwa timu zingine.

Kwani ni lazima kutangaza kabla ya mchezaji kutia saini ya kujiunga na klabu husika? Tabia hii hufanywa sana na watu wasiokuwa wasemaji wa vilabu vya Simba na Yanga! Kwa nini hawaachi habari hizo zitangazwe na wasemaji wa vilabu? Wana sababu gani kuingilia kazi za wasemaji wa vilabu walioajiriwa maalum kufanya kazi kama hizo?    

          Waandishi waache kuchukua habari za mitaani kuhusu mambo ya vilabu kwani mashabiki huweza kusema lolote kuhusu vilabu vyao liwe baya au zuri. Wasiojua umuhimu wao katika uandishi hukimbilia kuandika wakidhani ni kile kiitwacho ‘scoop’ yaani habari inayotangazwa mara na gazeti moja kabla ya mengine.

[email protected]

0784  334 096