Mwendo kasi chanzo cha ajali barabarani?

20Dec 2016
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Mwendo kasi chanzo cha ajali barabarani?

NINATAKA Mtanzania yeyote aliye mkweli ajitokeze kwamba yuko tayari kufanya safari ya kwenda Mbeya, Mwanza, au Arusha na kufika saa sita usiku au siku ya pili kwa mwendo wa taratibu ambao hautasababisha ajali.

Ninaomba ajitokeze! Tusipende kuzungumza vitu ambavyo havitekelezeki.

Kwa sisi ambao tumekuwa tunaendesha magari, tujiulize, kuendesha basi kwa spidi ya kilomita 90 au 80 kwa saa ndio mwendo kasi? Hiyo ni spidi ya wastani kwa madereva wengi.

Nieleze , ukiwa dereva unaweza kuendesha umbali wa kilomita 1,100 kutoka Dar-es-Salaam hadi Mwanza kwa kilomita 60 kwa saa? Unajua kiasi gani cha mafuta kitatumika ukilinganisha na wenzako watakaokwenda kwa mwendo wa wastani wa kilomita 90 kwa saa?

Na tutahitaji madereva wanne wa kupokezana.Kuna tajiri anayeweza kumudu gharama hizo? Inawezekana maswali yangu ni ya upuuzi, lakini tujaribu kujiuliza.

Najiuliza ni nani anayetaka kwenda kwa taratibu siku hizi? Wafanyabiashara wengi wanatamani kufanya safari ambayo angeweza kwenda na kurudi siku hiyohiyo. Wafanyakazi wengi wanaowahi mikutano angetamani aende siku hiyohiyo na kuwahi mkutano badala ya kutoka jana yake.

Muda ni mali, na ndio maana shirika lililowezesha wafanyabiashara kusafiri kwa bei rahisi na kwa kasi linapata wateja wengi. Huu ni wakati wa spidi. Wakati wa kwenda kasi. Ndio msingi wa utajiri na ubepari.

Kasi hupunguza gharama, na huo ndio ukweli. Sasa tujiulize kama hakuna sababu zingine zaidi ya mwendo kasi zinazosababisha ajali?

Magari ya siku hizi yanayosafirisha abiria ni makubwa na yenye nguvu sana. Mabasi ni marefu ukilinganisha na yale ya Albioni na Fiat. Je barabara zetu zimejengwa kufanana na urefu na kasi ya magari haya?

Unakuta mara nyingi gari linapokata kona, ni lazima likope sehemu kutoka upande mwingine wa barabara? Huenda utasema kwa sababu ya kasi ya gari, lakini endesha gari lako kwenye mwendo wa staha na kuogopa ajali kama watu watakuja kupanda?

Aidha madereva wanaendesha saa ngapi kwa siku na saa ngapi kwa wiki? Unakuta wiki nzima mfanyakazi wa basi yuko kwenye gari isipokuwa linapoharibika. Unadhani tunaweza kuepuka ajali kama polisi wenyewe waliosema kuwa, madereva wapokezane kila baada ya saa nane wanashindwa kulinda sheria yao ikatekelezwa?.

Dereva anafika Dar-es-Salaam saa tatu usiku kutoka Mwanza. Analala saa nne, saa kumi na moja analileta gari tena kituoni kuanza safari ya kurudi Mwanza.

Hana devera wa kumpokea, wiki nzima iko hivyo, sielewi uwezo wa binadamu katika hili linaishia saa ngapi kwa siku. Wenzetu huko Ulaya dereva wa lori au basi linalofanya safari ndefu, anapofika saa nane, anashuka, mwingine anapokea.

Aliyeshuka anakwenda kulala hotelini akisubiri kesho kumpokea mwenzake atakayekuja kesho. Hapa kwetu dereva wa lori anaendesha basi kwa saa 100 hadi mia tano kwa wiki kutoka Dar-es-Saalaam,Kigali, au Dar-es-Salaam hadi Lubumbashi.

Hata kama wako wawili wakisaidiana hakuna binadamu anayeweza kufanya hivyo bila kufanya makosa. Na kwenye mabasi huyu akipokelewa analala hapohapo kwenye boneti ya injini. Baada ya saa nne anaamshwa tena kuendelea na kazi.

Kuna wakati wanaoendesha ni utingo ambao hatujui kama ni wazoefu, maana pale Ubungo amesainishiwa mwingine, lakini anayepokea njiani hatujui kama ana uwezo wa kutosha.

Ni polisi wanaosababisha haya kwa sababu wanashindwa kutimiza wajibu wao wa kusimamia sheria, na wanashindwa kutumia teknolojia ya kisasa kudhibiti mambo mengine ambayo ndio visababishi vya ajali.