Mwisho wa malalamiko ya Ligi Kuu?

09May 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mwisho wa malalamiko ya Ligi Kuu?

ENDAPO kusudio la Rais John Pombe Magufuli litatekelezwa baada ya mawasiliano ya hapa na pale, bila shaka timu 19 za Ligi Kuu ya msimu huu wenye utata wa corona, zitafurahia isipokuwa moja ndio itakayosononeka kwa kucheleweshewa kombe lao.

Hiyo ni timu ya Simba, maarufu ‘Wekundu wa Msimbazi.’ Sipendi kuiita ‘mnyama’ kama walivyozoea waandishi wa michezo, kwani ‘mnyama’ ni hayawani yaani mnyama wa miguu minne ilhali wachezaji wa Simba ni binadamu kama wengine wenye miguu miwili.

Napata ukakasi wa kutumia jina hilo kwa wachezaji wa klabu ya Simba kwani maana nyingine ya mnyama ni tamko la kumtusi mtu.

Nasisitiza kuwa ni ‘watani wetu wa jadi’ kwa maneno lakini si kwa vitendo. Watani hawadhuriani bali husaidiana kwa kila hali lakini si kwa Simba na Yanga! Kila moja inaiombea nyingine mabaya. Huo si ‘utani wa jadi’ bali ni ‘chuki za jadi!’

Mpaka Ligi Kuu iliposimamishwa kutokana na ugonjwa mpya unaoitwa corona ukiendelea kuitikisa dunia, bingwa mtetezi, Simba ilikuwa ikiongoza kwa alama 71 baada ya kucheza mechi 28 ikifuatiwa na Azam FC pia iliyocheza mechi 28 lakini ikiwa na alama 54 na Yanga ikiwa nafasi ya tatu kutoka juu imecheza mechi 27 na kuambulia alama 51.

Tukirudi chini, timu ya mwisho inayolemewa kwa uzito wa kuzibeba timu 19 zilizo juu yake, ni Singida United yenye alama 15 baada ya michezo 29 ikiwa na mabao 16 ya kufunga na kufungwa 49. Ni timu pekee iliyofungwa mabao mengi zaidi ya zingine. Juu ya kichwa chake ni timu ya Mbao yenye alama 22 kwa kukubali kufungwa mabao 33.

Kwa mwenendo huo huo wa kwenda juu, kuna timu ya Alliance FC yenye alama 29 na kufungwa mabao 36 ilhali Mbeya City ikiwa kichwani mwa Alliance kwa alama 30 na kuambulia mabao 35 ya kufunga. Timu zote hizi zipo hatarini kushushwa daraja endapo hazitapanda juu kama ligi ikiendelea.

Ikumbukwe pia kwamba wakati mwingine kandanda ni mchezo unaoshangaza kwani umdhaniaye siye aweza kuwa ndiye na adhaniwaye ndiye akawa siye!

Katika hali hii, kila timu itacheza kwa bidii ili zile zinazoifuatia Simba, yaani Azam, Yanga, Namungo na Coastal Union zisishuke chini ya hapo zilipo bali zisalie kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuna manung’uniko ya chini kwa chini yanayotolewa na wapenzi, mashabiki na hata viongozi wa Simba wakitaka wakabidhiwe kombe kwani hata ligi ikiendelea haiwezi kukosa kombe iwe jua iwe mvua. Maana yake ni kwamba hakuna timu itakayofikia idadi ya alama ilizo nazo.

Ni kweli kwamba timu zilizo chini ya Simba hakuna itakayoweza kuipiku kwani ipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya zingine. Husemwa kandanda ni mchezo wa bahati. Sawa, lakini mpaka Ligi iliposimamishwa, Simba ilikuwa na alama nyingi (71) zaidi na mabao 63 ikifungwa mabao 15. Pia imetoka sare mara mbili na kupoteza michezo mitatu.

Wakati Azam FC iliyo nafasi ya pili ikiwa na mabao 37 ya kufunga na kufungwa 20, imecheza michezo 28 kama Simba lakini meshinda michezo 16 na kupoteza 6. Yanga nayo imecheza michezo 27, imeshinda 14, imetoka sare mara 9, kufungwa mara 4 ikiwa na mabao 31 na kufungwa 20.

Namungo imecheza mechi 28 ikishinda mechi 14 kama Yanga, sare mara 8 na kupoteza michezo 6, mabao 34 ya kufunga na kufungwa mabao 25. Coastal Union ambayo ipo kwenye hatari ya kumpoteza mchezaji wao Bakari Mwamnyeto kusajiliwa na Azam, Simba au Yanga msimu ujao imecheza mechi 28, imeshinda mara 13, imepata sare 7 na kupoteza mechi 8 na kupata mabao 27, dhidi ya mabao 19 waliyofungwa na kupata alama 46.

Husemwa kandanda ni mchezo usiotabirika lakini kwa hali yoyote itakavyokuwa kwa Ligi ya mwaka huu, itakuwa ni ajabu Simba kupoteza mechi nyingi zitakazoifanya ipokonywe kombe ililotwaa mara mbili mfululizo misimu miwili iliyopita hata ishindwe kulitwaa moja kwa moja mwaka huu.

Kama Ligi itasimamishwa na Simba kupewa ushindi, italeta shida kwa timu zinazowania nafasi za pili, tatu na nne na mbaya zaidi timu zitakazojitahidi kuepuka kushuka daraja kwa sababu nazo zitalalamika kwa kutopewa nafasi ya kukwepa kadhia hiyo.

Kwa maana hiyo, viongozi wa Simba wanapaswa kuwa waungwana kwa kukubali Ligi Kuu iendelee badala ya kukabidhiwa kombe ilhali ligi hiyo haijamalizika. Sisemi wachezaji wa Simba waingie uwanjani kwa dharau, La hasha. Wanatakiwa kudhihirisha ubingwa wao wa mara ya tatu mfululizo, vinginevyo watapoteza heshima yao kama watacheza kwa dharau na kusababisha wakose kombe!

[email protected]

0784 334 096