Mwongozo ukoje pale mteja anaposhindwa kurejesha Mkopo?

20Jul 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Mwongozo ukoje pale mteja anaposhindwa kurejesha Mkopo?

MASUALA ya kuweka mali rehani ili kupata mkopo hapa nchini yanaongozwa na sheria kuu mbili nazo ni Sheria namba 4 ya Ardhi ya mwaka 1999 sura ya 113, pamoja na sheria namba 17 ya rehani ya mwaka 2008.

Kifungu cha 127 (1) cha Sheria ya Ardhi, kinatambua habari ya mhusika kushindwa kurejesha mkopo. Kinaielezea hatua hiyo kama miongoni mwa mambo ambayo yanakiuka masharti ya mkataba wa mkopo.

Wiki iliyopita tulianza sehemu ya kwanza ya makala hii na sasa tumalizie vipengele muhimu vya kuzingatia kwenye masuala ya rehani.

Ukiukaji wa masharti ya mkopo kutumia mali iliyowekwa reheni inaweza kuwa ni pamoja na kuweka mali hiyo reheni kwa taasisi au mkopeshaji zaidi ya mmoja.

Aidha, kuuza, kupangisha bila ya hata mhusika kutoa taarifa au kuomba ridhaa kwanza kutoka kwa mtoa mkopo nao ni ukiukaji.

Hata hivyo haya na mambo mengine yanayofanana na hayo yatachukuliwa kama kukiuka masharti ya mkopo ikiwa yamekatazwa, wazi wazi, katika kupitia mkataba baina au kati ya taasisi ya fedha na mteja wake.

Pia kwa mujibu wa sheria mteja kushindwa kurejesha mkopo kunajumuisha pesa kamili aliyoiweka kama mkopo, riba, pamoja na makato mengine ambayo na yenyewe yanafanya sehemu ya mkopo huo.

NOTISI SIKU 60

Notisi ni ya lazima kabla nyumba au kiwanja cha mteja hakijauzwa. Bado siyo tu lazima mhusika kupatiwa mapema, bali pia ni matakwa ya kisheria kutoa muda wa siku zisizopungua 60.

Hivyo basi, mtindo wa kutoa au kuwapatia wahusika notisi ya siku 14 tu au wakati mwingine chini hizo ni kukiuka taratibu za kisheria zilizowekwa.

Kifungu cha 127(1) (a) cha Sheria ya Ardhi kinaeleza kuwa pale mkopaji anapokuwa ameshindwa kurejesha mkopo kwa wakati au kwa mujibu wa makubaliano ya awali, basi taasisi ya fedha itampatia mkopaji, au mteja wake taarifa ya siku 60 juu ya nia yake ya kuuza mali.

Siku hizo zikiisha kabla mkopaji hajalipa moja kwa moja taasisi hiyo itaweza kuendelea na hatua za kuuza ikiwa tu itaamua kufanya hivyo. Kimsingi, ni lazima mteja apatiwe taarifa ya siku 60 kabla.

Siku hizo zinaanza au zitaanza kuhesabika kutokea siku taarifa ilipopokelewa au kumfikia mteja. Kinyume chake itakuwa ni kosa kwa mujibu wa sheria.

MUHIMU

Notisi haishii kuhusika tu pale mteja anaposhindwa, atakaposhindwa kufanya malipo kwa mujibu wa makubaliano.

Bali pia kufuatia ukiukwaji wa sharti lolote lile la haki katika mkataba wa mkopo, ambalo taasisi ya fedha inadai mteja wake amelikiuka.

Hapo pia, katika mazingira kama hayo, itabidi mteja husika kuchukuliwa hatua kisha taratibu nyingine baada ya hiyo zitafuatia.

UKIUKAJI NOTISI

Awali ya yote, kama nyumba au kiwanja bado hakijauzwa nenda mahakamani ili kuweka zuio (Caveat); na piliendapo mali imeshauzwa bado mhusika anaweza kufungua shauri mahakamani kubatilisha mauzo hayo batili kwa msingi wa  kukiukwa kwa taratibu nzima za mauzo, na kurejeshewa mali yake.

ANGALIZO

Kwa mujibu wa Sehemu ya (iii)-Kanuni ya 7(1), Kanuni mpya za Sheria ya Ardhi kupitia tangazo la Serikali namba 345 la Aprili 2019.

Inaelekeza, mwenye kiwanja au shamba ambalo (kwa namna moja au nyingine) halijaendelezwa au lenye maendelezo hafifu ikiwa ataomba mkopo na kuweka rehani ardhi hiyo, atatakiwa ndani ya miezi sita kutokea siku alipoweka rehani, apeleke taarifa kwa kamishna wa ardhi kuonyesha ni namna gani pesa yote au sehemu ya pesa alizokopa zimetumika katika kuendeleza ardhi hiyo.

Hili ni kwa ardhi zilizopimwa pekee, majanga kwa wamiliki wasio rasmi. Mfano kama taasisi ya fedha (benki) itaamua kukupatia mkopo kwa ‘sharti kuu’ la kuliendeleza eneo husika basi ndani ya miezi sita tokea mteja apokee mkopo ni lazima atawajibika kutimiza takwa la kutii kupeleka au kuwasilisha ‘taarifa maalum' kwa Kamishna wa Ardhi.

Ataonyesha ni kwa namna au jinsi gani mkopo huo umetumika kuendeleza ardhi ambayo imetajwa kama rehani, hata kama mkopo husika unatoka kwa mafungu (installments).

Aidha hata kama hizo fedha zinakopwa maalum kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza biashara fulani, kununua gari ni lazima kiasi fulani kitengwe kwa ajili ya kuiendeleza ardhi inayohusika.

Na taarifa ya namna pesa ilivyotumika kuendeleza eneo itatakiwa kutolewa katika fomu maalum ambayo imeanzishwa na Sheria ya Ardhi fomu namba 551.

Zaidi, udanganyifu wowote katika mchakato mzima ni jinai inayoweza kupelekea mhusika (yeyote) kwenda jela kwa kifungo kisichozidi miaka miwili au faini, ama vyote viwili kwa pamoja, kwa mujibu wa kanuni ya 9 ya sheria ya reheni.