Mzizi wa mimba kwa wanafunzi uko huku

31Oct 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mzizi wa mimba kwa wanafunzi uko huku

LICHA ya serikali kuweka adhabu kali kwa wanaowasababishia ujauzito kwa wanafunzi na watoto chini ya umri wa miaka 18, bado tatizo la mimba za utotoni limeendelea kuwapo na kukatisha ndoto zao.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - Tamisemi), Mwita Waitara, anataja chanzo ni mila na desturi, kwa vile zipo ambazo mabinti wanapofikia umri fulani, wanapewa chumba chao.

Kwa mujibu wa Waitara kupitia kauli yake jijini Dodoma kwenye maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani, tatizo hilo ni kubwa kwa shule zote; msingi na sekondari.

Waitara anasema, asilimia 29 ya tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mila na desturi na kuleta walakini hata katika utekelezaji wa mashtaka na uendweshaji wa kesi zinazohusu ngono na mimba kwa wanafunzi.

"Uendeshaji kesi hizi mpaka kumtia mtu hatiani bado ni changamoto, kwa kuwa wanaofanya vitendo hivyo, wengine ni watu wa karibu na familia na wengine wanarubuni ndugu na kumalizana kimya kimya,” anasema Waitara.

Anafafanua kwamba, uelewa wa watoto bado ni mdogo, huku mimba nyingi zinazoripotiwa zikiishia hewani bila ya kujua mwisho wa kesi.

Naibu Waziri anasema, serikali kila mara imekuwa ikifanya vikao na wazazi kuondokana na tatizo hilo, lakini bado mwitikio ni mdogo katika kudhibiti vitendo hivyo.

Mbali na hayo, anasema bado kuna changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi na kwamba kati ya vizazi hai 100,000 vya watu waliopo, 556 wanaripotiwa kufariki dunia kwa sababu mbalimbali, ikiwamo mimba za utotoni.

Mjadala huo naamini una haja ya kuchukuliwa hatua za makusudi, ili kumaliza tatizo. Hiyo ni pamoja na kuwaelimisha wazazi, ambao ni wazito kuelewa umuhimu wa elimu.

Inasikitisha kuona serikali inawashirikisha wazazi katika kumaliza tatizo hilo, halafu baadhi yao wanakuwa wazito kutoa ushirikiano. Inawezekana hao ndiyo wanaoendekeza mila na desturi zisizo sahihi.

Ni vyema juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kwa lengo la kuhakikisha mtoto wa kike anakamilisha elimu yake bila ya kikwazo ziheshimiwe na watu wote.

Hebu fikiria, eti kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, wanafunzi 142 wameshakatisha masomo kwa sababu ya mimba, mkoani Lindi.

Taarifa iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na Ofisa Elimu (Taaluma), Hatibu Tuki, inaonyesha idadi hiyo walipata ujauzito kuanzia mwezi Januari hadi tarehe 30 iliyopita.

Hivi hali kama hii ikiwa kwenye mikoa yote nchini kutakuwa na wanafunzi wangapi wenye mimba? Ni vyema wazazi na walezi wabadilike na kushiriki kikamilifu katika vita ya kuzuia mimba hizo.

Tabia hii chafu ya kuwapa mimba wanafunzi haijawaacha nyuma baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari, kwani nao wamekuwa wakitajwa katika vitendo hivyo, ambavyo ni kinyume na maadili.

Katika kukabiliana na tatizo hilo la mimba, mwaka 2016 serikali ilifanyia marekebisho Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, ikisimama katika marufuku ya mapenzi na mwanafunzi.

Sheria ya Makosa ya Kujamiiana inaenda mbali, kwa kutangaza adhabu nzito inayoangukia miaka 30 hadi kifungo maisha.

Kwa bahati mbaya, pamoja na kuwapo sheria hizo, bado tatizo la mimba limeendelea kusikika na kuthibitishwa katika maeneo mbalimbali nchini, hali ambayo ni hatari kwa maendeleo ya elimu ya mtoto wa kike.

Mjadala huu unaamini kwamba, ushirikiano wa wazazi na walezi na serikali katika kutatua tatizo hili na muhimu kusaidia kuwabana wanafunzi na ‘mafataki’ wanaosababisha kuendelea kuwapo mimba hizo.

Wasichana wana haki ya kupata elimu, hivyo wanatakiwa kulindwa, ili kukomesha mtindo huo wa baadhi ya watu wasio na ‘mshipa wa aibu’ kwa kuendekeza ngono.

Kukomesha uwapo kwa mimba kwa wanafunzi inawezekana, iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake ikiwamo malezi bora na pia kutoa ushirikiano na vyombo vya dola ili kuwanasa ‘mafataki’ hawa.