Nafasi tatu Ligi Kuu ziwe za kimataifa msimu ujao

27May 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Nafasi tatu Ligi Kuu ziwe za kimataifa msimu ujao

FAIDA ambayo Tanzania imeipata msimu huu kwenye nyanja za michezo ni timu ya Taifa, Taifa Stars kutinga Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), na vile vile timu ya Simba kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imesababisha Tanzania kupata nafasi nne za uwakilishi mechi za kimataifa msimu wa 2020/2021. Na washindi hao watapatikana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia msimu ujao wa 2019/2020.

Timu mbili zinatakiwa zicheze Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine mbili Kombe la Shirikisho Barani Afrika (Caf).

Hata hivyo, itategemea na Shirikisho la Soka nchini (TFF), itatumia mfumo gani kuwapata wawakilishi hao wanne.  Rais wa TFF, Wallace Karia, alikaririwa akisema kuwa hadi sasa hawajakaa kuangalia ni vipi watatengeneza mfumo wa kupata timu nne ambazo zitaiwakilisha Tanzania kwenye mechi za kimataifa.

Kwa sasa mfumo uliopo ni kwamba bingwa ndiye anaiwakilisha Bongo kwenye Ligi ya Mabingwa na Mshindi au bingwa wa Kombe la Shirikisho nchini (TFF), maarufu kama Kombe la FA, ndiye anayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (Caf).

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Tanzania inapeleka timu mbili tu, yaani moja Ligi ya Mabingwa na moja Shirikisho.

Kwenye mjadala huu natoa ushauri kwa TFF kutokaa na kuumiza kichwa sana jinsi gani ya kuwapata wawakilishi wanne, badala yake waipe thamani Ligi Kuu Tanzania Bara itoe wawakilishi watatu kwenda kwenye mechi za kimataifa.

Nina maana kuwa Bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa pili waiwakilishe Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na mshindi wa tatu moja kwa moja aiwakilishe nchi kwenye Kombe la Shirikisho, aungane na Bingwa wa Kombe la FA naye acheze Shirikisho.

Hapa tayari nchi itakuwa imepata wawakilishi wake wanne kwenye michuano hiyo.

TFF isitafute michuano mingine au kutengeneza vitu ambavyo vitazidi kuifanya ligi isiwe na mvuto wala thamani.

Kwa sasa Ligi Kuu ina timu 20 ambazo ni nyingi, lakini anayetafutwa ni bingwa mmoja tu na tumeona timu moja au mbili zikishakuwa na pointi nyingi kuliko zingine, msisimko unapotea.

Kwa maana hiyo, zikitafutwa nafasi tatu kati ya timu 20 zinazocheza Ligi Kuu, nadhani itakuwa na mvuto wa hali ya juu kwani hata kama kuna timu ambayo itakuwa na pointi nyingi na kukaribia ubingwa, bado kutakuwa na timu zinapambana ili kupata nafasi ya pili na ya tatu kwa ajili ya kuiwakilisha nchi, hivyo ligi kuendelea kuwa ngumu na bora zaidi.

Hapo hata timu inayosaka ubingwa inaweza kuwa na wakati mgumu ikipambana na timu ambayo inatafuta nafasi angalau ya tatu kwa ajili ya kucheza Kombe la Shirikisho.

Mifano tunaona kwenye Ligi Kuu ya England ambapo mbali na vita ya ubingwa, lakini kuna nyingine ya nne bora maarufu kama 'top four' na hiyo inaifanya kuwa ngumu na isiyotabirika.

Kuanzia msimu ujao ambapo zitaanza kutafutwa timu nne, nashauri Ligi Kuu sasa iwe ya 'top three', yaani timu tatu za juu ziende kucheza mechi za kimataifa, mbili Ligi ya Mabingwa na moja Shirikisho, hapo hata TFF yenyewe itaona jinsi gani ligi itakavyokuwa ya ushindani, na inaweza kabisa kusababisha hata kupata wadhamini na klabu zikaanza kunufaika.