Naibu Spika Dk Tulia busara itaepusha mpasuko bungeni

10Jun 2016
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Mjadala
Naibu Spika Dk Tulia busara itaepusha mpasuko bungeni

TANGU kuanza kwa Bunge la 11 mjini Dodoma Watanzania wameshuhudia baadhi ya kauli za kutishiana na kuoneshana ubabe baina ya kiti cha Spika na wabunge wa vyama vya upinzani.

Kauli hizo za ubabe zilikuwa ziliibuka pale wabunge wa upinzani walipokuwa wanaomba mwongozo ama taarifa kwa Naibu Spika, Spika ama Mwenyekiti wa Bunge.

Msuguano huo uliendelea kwa muda mrefu hadi ukafikia hatua mbaya, ya wabunge wa vyama vya upinzani kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia kwa kile kinachodaiwa kwamba amekuwa akiwaonea, kuwanyanyasa na kuwaburuza.

Uhasama huo, baina ya Wabunge hao na Naibu Spika umezidi kukua siku hadi siku hata hivi karibuni wabunge hao walitoka ndani ya ukumbi wa Pius Msekwa uliopo nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kiongozi huyo kupewa nafasi ya kufungua semina ya wabunge kuhusu Malengo Endelevu ya Dunia.

Mwenendo huo siyo dalili nzuri hata kidogo kwa chombo hicho cha kutunga sheria.Uhasama ambao haijulikana hatma yake ni nini kati ya wabunge wa wapinzani na Naibu Spika, Dk. Tulia.

Kwa watu wanaoutamia mema mhimili huo ili ujiendeshe kwa manufaa ya watanzania, wanamuomba Mungu ili uhasama huo uishie katika masuala ya siasa tu na usiendelee katika shughuli nyingine za kijamii.

Ni imani yangu kuwa, Naibu Spika Dk. Tulia ni mbobezi wa sheria tofauti ikilinganishwa na Spika wa Bunge aliyetangulia Anne Makinda ambaye fani yake haikuwa sheria,lakini alijitajidi kutumia ujuzi, maarifa, busara,usikivu na kuangalia upepo unavyokwenda na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa jahazi haliendi mrama.

Kwa Dk Tulia ambaye anaijua sheria vizuri kwani kabla ya kushika nafasi hiyo alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tunatarajia makubwa zaidi kutoka kwake.

Busara na hekima yake ikitumika kikamilifu itasaidia sana kuwawezesha wabunge wa vyama vyote kujiridhisha kuwa haki inatendeka bila ya ubaguzi na kwa manufaa ya wananchi waliowachagua wanaowatarajia wawatumikie.

Ukweli ni kwamba kiti cha Spika kina nguvu kubwa za kisheria katika kuliongoza Bunge kwa kuzingatia kanuni mbalimbali.

Pamoja na mazingira hayo,lakini bila ya kuwapo busara na hekima inaweza kusababisha Bunge hilo ‘kupasuka’ kama lilivyoanza kuonesha dalili.

Kwa sasa baadhi ya wabunge wa upinzani ni kama hawataki kuona wanaongozwa na Naibu Spika. Hawapo tayari kuingia katika kikao chochote kitakachoongozwa na kiongozi huyo hata kama ni wasilisho la Bajeti kuu.

Ni vyema Naibu Spika Dk. Tulia akatafuta ushauri kutoka kwa wazee waliowahi kuliongoza bunge hilo, kama vile Samuel Sitta, Pius Msekwa na Anna Makinda kwa namna gani walifanikiwa kuwaongoza wabunge wapinzani ambao kuna nyakati huona kuwa wanaonewa.

Kama alivyowahi kusema Mzee Pius Msekwa, Bunge ni taasisi ya utungaji wa sheria za nchi, wabunge nao, bila kujali jinsia zao wala umri walionao, wanawajibika kufuata kanuni na sheria zinazotawala Bunge, mbunge anapokiuka kanuni na taratibu zilizopo, anawajibika kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Matarajio ya wananchi siyo kuona huo ushindani, bali kuona mambo ya msingi yanajadiliwa kwa kina na kutafutiwa ufumbuzi ambao utawanufaisha Watanzania wanaounga mkono chama tawala, vyama vyaupinzani na wasio na itikadi zozote.

Tunaamini wabunge kama ilivyo kwa binadamu wengine, wanatofautiana katika maono na mitazamo ya mambo mbalimbali.

Wanatofautiana katika uwasilishaji wa hoja, katika kujadili, kufanya maamuzi na hata katika utekelezaji. Wabunge wengine wanamitazamo hasi kwa kila kinachojitokeza, katika hali kama hii, Naibu Spika anatakiwa awe mpole, mvumilivu na bustara zaidi katika kukabiliana na wabunge wa aina hiyo.

Anne Makinda aliyeamua kustaafu baada ya kuwa mtumishi kwa nafasi mbalimbali ndani ya chama na serikalini kwa miaka 40, aliwahi kueleza kuwa, Spika anayetakiwa ni lazima akubali kujifunza tabia za wabunge wake na awe na uwezo wa kukabiliana na hali halisi ya bungeni.

Makinda aliwahi kueleza pia kuwa Spika lazima awe mvumilivu na anayeweza kuzuia hasira, na badala yake atumie muda mwingi kujifunza kanuni za Bunge na kuwa mwepesi kupokea hoja za wabunge bila kubagua ili aweze kuzifanyia kazi.

Dk. Tulia ni mama na mwanamke ambaye anatakiwa kusimama kidete katika kutetea haki za wanawake wenzanke popote.

Mathalani kuna kauli tata zilizotolewa bungeni na mbunge mmoja kwamba wabunge wanawake wa kambi ya upoinzani hawapati nafasi hizo hadi waitwe ‘baby’.

Yalilenga kuwadhalilisha wanawake wabunge wa viti maalum. Naibu Spika aliinyamazia hata kusababisha hali kuibua malumbano na zogo bungeni, huku kiti cha Spika kilikuwa kinaangalia tu bila kuchukua hatua yoyote.

Kwa namna yoyote ile , busara ya Naibu Spika itasaidia sana kuliepusha Bunge na mitafaruku isiyo na tija kwa nchi na kufanya kazi yake ya kuwakilisha wananchi katika kuisimamia Serikali kwa ufanisi zaidi.

Tumeshuhudia katika Bunge hili la 11 wabunge saba wote wa upinzani wameadhibiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge wasihudhurie vikao vyote vya Bunge hilo na vijavyo kwa kile kilichoelezwa kuwa vinara wa vurugu mbalimbali zilizotokea bungeni.

Swali ninalojiuliza, kwa nini adhabu kama hizo kali hazikuwahi kutolewa katika Bunge lililopita? Kwa nini sasa? Kwa nini wabunge wa upinzani wamgomee Naibu Spika peke yake na siyo viongozi wengine wa Bunge? Majibu ya maswali hayo yote ni busara na hekima itumike ndani ya Bunge kuliko nguvu, sheria, itikadi za vyama na mengineyo ambayo yanatishia kulifanya Bunge lisifanye kazi zake kwa ufanisi.

Wote tunajenga nyumba moja ambayo ni Tanzania ya maendeleo hivyo hakuna haja ya kunyang’anyana fito na mwiko.