Namna nzuri ya kufanya biashara yenye mafanikio

17Mar 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Namna nzuri ya kufanya biashara yenye mafanikio

KARIBUNI wasomaji wa safu hii ya Mtazamo Kibiashara, na kwa leo nimeona tuangazie namna nzuri ya kufanya biashara yenye mafanikio kwa mfanyabiashara wa ngazi yeyote.

Kimsingi inaweza ikawa rahisi kuanzisha biashara yoyote, kwani kuna fursa za kutosha za kuanzisha biashara kulingana na mtaji na maarifa aliyonayo mtu ya kufanya biashara.

Lakini, ugumu huwa ni ule wa kuifanya biashara uliyoianzisha kuwa ya mafanikio.

Hata hivyo, kufanya biashara yenye mafanikio huanza na hatua ya awali ya kupanga aina ya biashara anayotaka mtu kuifanya. Aidha kama mfanyabiashara atataka kuajiri mtu, basi anapaswa afikirie aina ya mtu wa kumuajiri na jinsi atakavyodhibiti mapato yake, kwani vyote hivyo ni muhimu sana ili biashara iwe ya mafanikio.

Sasa kuna mambo ya kuzingatia ikiwa unataka kuanzisha biashara itakayokuwa na mafanikio. Baadhi ni mambo hayo ni haya yafuatayo:-

CHAGUA BIASHARA SAHIHI

Mafanikio yako katika biashara yanaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja ya jinsi utakavyochagua biashara ya kufanya. Kimsingi, unapaswa kuchagua biashara itakayotumia ujuzi na kipaji chako vizuri. Kwa mfano kama una mkono wa biashara ya duka, fanya hivyo, kama una mkono wa biashara ya genge fanya hivyo, kama una mkono wa biashara ya mkaa, mazao, nguo, upishi na kadhalika, basi anzisha biashara hiyo.

Hata hivyo ni muhimu sana kuzingatia namna biashara unayotaka kuianzisha unavyohitajika na watu, yaani wingi wa wateja wa biashara unayotaka kuianzisha. Kwa maana nyingine, ni vyema ukatilia maanani uwepo wa biashara zingine za aina hiyo unayotaka kuanzisha kwenye eneo husika, ili usijikute unaanzisha kutokana na mkumbo tu, kwamba maadam wengine wameanzisha, ngoja na wewe uanzishe. Hakikisha kwamba biashara unayoianzisha,kuna wateja tayari.

CHAGUA ENEO SAHIHI KWA BIASHARA YAKO

Hii ni hatua muhimu sana iwapo utataka biashara unayoianzisha iwe na mafanikio. Kwa mfano kama utataka kuanzisha biashara ya kuuza vocha za simu ama kuwa wakala wa kutuma fedha kwenye mitandao, basi hakikisha eneo unaloweka biashara yako liko barabarani, sehemu inayofikiwa na watu wengi. Vivyo hivyo kwa biashara zingine, uchaguzi wa eneo la kuweka biashara yako ni la msingi sana.

KUWA NA MALENGO KATIKA BIASHARA YAKO

Maana rahisi ya kuwa na malengo ya biashara yako, ni ile ya kupanga kwamba, baada ya kipindi fulani cha kufanya biashara yako unataka iwe imepanuka kwa kiwango fulani. Kwamba pengine kama ulianza na biashara ya duka kwa mtaji wa shilingi 100,000 kwa mfano, basi baada ya miezi sita, mtaji uwe imefikia walau Sh.130,000 au Sh.150,000.

Pia ni muhimu katika hatua hii ukawa unatunza kumbukumbu za biashara yako, yaani mapato, matumizi na faida unayotengenezeza. Hii itakusaidia hata pale utakapotaka kuomba mkopo wa kupanua biashara yako siku za usoni.

KUWA NA LESENI AU KIBALI CHA BIASHARA

Kuwa na leseni au kibali cha biashara ni kitu cha msingi kwa mfanyabiashara. Sasa kama biashara yako inahitaji uwe na leseni, basi hakikisha unakuwa na leseni halali, au kama inahitaji ulipie ushuru fanya hivyo. Ni vizuri uhakikishe unafanya biashara isiyo na mazonge ya aina yoyote ile.

ITAENDELEA