Nani ataibuka na ushindi leo?

04Jan 2020
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Nani ataibuka na ushindi leo?

“LIANDIKWALO ndilo liwalo.” Jambo lililoandikwa na Mungu ndilo linalokuwa. Yaani jambo ajaliwalo mtu ndilo limjialo, liwe baya au zuri.

Tunaambiwa “Kinywa ni jumba la maneno.” Maana yake kinywa cha binadamu ni kama jumba la maneno. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kuwa binadamu ana uwezo wa kusema maneno yoyote yawe mazuri au mabaya.

“Hauchi hauchi unakucha.” Mtu husema usiku hauchi, hauchi, lakini hatimaye jua huchomoza na usiku ukatoweka. Methali hii hutumiwa kumtia mtu moyo anapokabiliana na hali ngumu kumshajiisha* kuwa lazima atauona mwisho wa hali hiyo.

*Shajiisha ni kitendo cha mtu kumhamasisha mwingine kuwa na ari ya kufanya jambo. ‘Shajiika’ ni kitendo cha mtu kuingia hamu ya kufanya jambo; hamasika.

Simba na Yanga kila moja ina hamu ya kuishinda nyingine; si leo tu, bali kila zikutanapo. Timu hizi zaweza kushindwa na timu zingine zote hata za madaraja ya chini lakini hazisononeshwi (kitendo cha kusababisha kuwa na huzuni kubwa moyoni) sana, endapo mojawapo ikishindwa na nyingine!

‘Watani’ ni watu aghalabu (kwa kawaida; mara nyingi) wa kabila tofauti au rafiki mkubwa ambaye ameruhusiwa kumdhihaki mwingine kwa mujibu wa mila zao bila ya aliyetaniwa kukasirika.

Eti Simba na Yanga zaitwa “watani wa jadi.” Watani ni watu wanaosaidiana wakati wa dhiki (usumbufu unaosababishwa na matatizo; shida, mashaka). Kwa hali hiyo husaidiana kumaliza matatizo yao.

Kwa Simba na Yanga, ‘utani’ umegeuzwa kuwa ‘chuki’ (hisia ya kutopenda kitu au jambo) kwani ni wachache sana wa pande zote mbili wanaokubali kushindwa ilhali robo tatu ya wanachama na mashabiki wao hawakubali kushindwa! Hawajui maana ya ushindani kuwa kuna kushinda na kushindwa!

Kama Simba na Yanga ni ‘watani wa jadi’ wanaoishi jiji moja liitwalo Bandari ya Salama ambalo ndiyo Dar es Salaam ya sasa, kwa nini ziwekeane shonde (hali ya watu kutozungumza pamoja) ilhali wote ni wa aina moja na sampuli moja?

Yashangaza kusikia eti timu hizi zilikuwa moja zilipoanzishwa mwaka 1935 kabla ya kufarakana mwaka uliofuatia (1936) na kuundwa Sunderland enzi zile ambayo sasa ndio yaitwa Simba SC au ‘Wekundu wa Msimbazi.’

Eti sasa timu hizo zaitwa ‘watani wa jadi’ ilhali zaombeana mabaya kila uchao! Ni utani wa aina gani kumbe zachukiana kama walivyo Waarabu na Waisraeli?

Timu yoyote ngeni inayokuja Tanzania kucheza na hizi kongwe ziitwazo ‘watani wa jadi’ hushangiliwa na ‘mtani wa jadi’ aliye nnje ya uwanja. Mwenzao akipigwa na mgeni, ‘mtani wa jadi’ hushangilia utadhani mwenyeji ndiye aliyeshinda.

Mbona twajidharaulisha kiasi hiki hata twaonekana majuha (watu wenye uwezo mdogo wa kufikiri au kuelewa mambo; wapumbavu, wajinga, mabwege)?

Nduguyo anapigwa na mgeni wewe washangilia kipigo chake? Nchi yako yavamiwa na kushambuliwa na maadui wewe wapiga ngoma kuwapongeza wavamizi wanavyoshambulia na kuisambaratisha nchi yako? Kwa hali yoyote iwayo, unapaswa kupimwa akili yako.

Tutoke huko turudi kwenye mechi ya leo kati ya Simba wakiwa wenyeji na Yanga wakiwa wageni kwenye mzunguko huu wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Hapana shaka kuna mengi waliyoambiwa wachezaji wa timu zote mbili ikiwamo kuahidiwa zawadi za fedha, vyombo vya moto n.k. kwa timu itakayoshinda. Ahadi hizi ni hatari kwa timu kwani wachezaji wasiotumia akili hucheza bila kufuata kanuni za mchezo.

Ahadi hizo husababisha wachezaji wasio na hekima kucheza rafu mara kwa mara. Matokeo yake ni kuonyeshwa kadi za njano au kutolewa nnje ya uwanja kwa kuonyeshwa kadi nyekundu. Inapokuwa hivyo, wanaotolewa hukosa michezo mitatu na hivyo kudhoofisha uwezo wa timu husika.

Mwamuzi na wasaidizi wake (washika vibendera) wanapaswa kuchezesha kwa haki bila upendeleo kwani kufanya hivyo ni hatua moja mbele itakayowafanya wachaguliwe kuchezesha mechi za kimataifa.

Idadi kubwa ya watu wanaopenda mchezo wa kandanda wana timu wanazozipenda. Kwa hali hiyo waamuzi wanapaswa kuwa makini na kuchezesha kwa haki hata kama timu wazipendazo zikifungwa na wapinzani wao.

Watambue kwenye mashindano ya kandanda kuna mambo matatu au manne: kushinda, sare (kufungana idadi sawa ya mabao), suluhu (kutofungana) au kushindwa (kufungwa idadi yoyote ya mabao).

Mashabiki nao wanapaswa kutambua kuwa huo ni mchezo, yaani jambo linalofanywa kwa nia ya kuburudisha badala ya kuchukizana, kutukanana na mwishowe kupigana! Kwa nini tugombee gozi la ng’ombe ilhali hatujui nyama kala nani?

Hebu (tamko la kumtaka mtu akusikilize) kwa mara ya kwanza tuoneshe uungwana (hali ya kuwa tayari kumfanyia mtu wema na insafu; utu) ili iwe fundisho kwa wenzetu walio mikoani.

[email protected]
0784 334 096