Natabiri Watanzania watachagua sera

27Sep 2020
Nkwazi Mhango
Nipashe
FIKRA MBADALA
Natabiri Watanzania watachagua sera

KABLA ya kuzama kwenye mada, lazima niseme wazi. Natabiri kuwa Watanzania watachagua sera na si sura; uzoefu na si uanagezi; uhalisia na si hekaya za Abunuwas; ustaarabu na si matusi; ukweli, si uongo, uhalisia, si uchochezi na matendo na si nadharia.

Kwani urais si nafasi ya majaribio wala tambo bali serious business kwa kisambaa. Mnajua ninachomaanisha hata kama naongea kilevi. Kwa taarifa yenu, walevi wengi ni wasomi na watu wasio wanafiki. Ukimkosea mlevi, kabla hajawa mbwi, atakugwaya. Akishaweka vitu vyake, jiandae kufurumushiwa ukweli unaouma na kuchukiza kinoma. Hivyo, nisemayo leo, ni matokeo ya kanywaji. Waliozoea vitu vilivyotulia na kwenda shule, leo watanshangaa wakidhani sina akili nzuri wasijue mie ni bonge la daktari tena wa falsafa zote. KTY (kwa taarifa yako), hakuna watu wakatili kwenye kutovumilia ghilba kama walevi. Ukitaka kumdanganya mlevi, mnyime kanywaji. Ukitaka ukweli wengi wanaokuficha, mpe mlevi kanywaji.

 

Nizame kwenye mada sasa. Kuna mchambuzi mmoja kwenye mitandao, amekuwa akisema kuwa uchaguzi huu unaweza kuwa wa aina yake kwa vile wapiga kura watapiga kwa huruma badala ya hekima. Nakubaliana naye kuwa uchaguzi huu ni wa aina yake kwa vile umejaa wabangaizaji hata wachochezi wanaojua kuwa watapoteza, lakini watapata kiki.

Kwanza kwa wanaojua maana ya kufaa katika kutumikia watu, wapiga kura huangalia mambo mengi na si kumuonea huruma mgombea. Wapiga kura si mama au baba huruma.

Pili, kutumia uzoefu wa Nelson Mandela, rais wa kwanza mzalendo wa Bondeni alivyochaguliwa kwa vile alikuwa amefungwa na serikali ya kikaburu kwa jumla ya miaka 27. Ni kushindwa kuelewa kuwa serikali ya kikaburu ilikuwa haramu. Ni kushindwa kuelewa kuwa mateso yatokanayo na kupigania umma. Mandela alipigania uhuru. Siasa za Afrika Kusini na za kipindi kile ni tofauti na za sasa za Bongo ambapo lazima utumie bongo na si bango, sera na si sura, matokeo halisi na si matarajio.

Tatu, kwa kuzingatia kile Watanzania karibu wote wanahitaji wataangalia utendaji wenye mashiko. Katika yote, maendeleo yatachukua kiti cha mbele kwenye vipaumbele ambayo Watanzania wanavyo. Afya, amani, barabara, elimu, miundombinu, nishati, na usalama vitakuwa ni tunu wanazotaka anayetaka kuwaongoza awe na uwezo wa kuwahakikishia ima kutokana dira na ilani yake au mambo ambayo ameishayafanya. Hawatakubali kugeuzwa mabunga wala sehemu ya siasa za majaribio. Huu ni ukweli ambao unaweza kuuapia hata bila kupata kanywaji. We are now going practical as opposed to theoretical. Kwa kimakonde ni kwamba sasa tunaangalia vitendo na si ngonjera na mashairi. Kwa kijita ni chikerebe, cha kwa akina Pius Msekwa, ni kwamba kapira bwacha sugu si salamu bali kanuni ya sayansi.

Amini usiamini. Watanzania wa sasa si wa jana. Wanataka mambo yanayowezekana na si hadithi za Paukwa Pakawa. Siasa siyo hadithi ya mapenzi. Ni uwanja ya maslahi tena mapana na mengi. Ukitekeleza nilichokutuma na ulichoahidi, nani akuondoe? Waliokuwa wakitaka maji wakayapata watamchagua aliyewezesha; kadhalika kwa barabara, umeme na mengine. Waliochukia ufisadi watachagua aliyeuangamiza; ukwepaji kodi na wizi wa rasilimali zao watachagua aliyekomesha kadhia hii. Mwenye macho haambiwi tazama; mwenye masikio sikia. Kila kitu kiko wazi kama usiku na mchana. Nani ni usiku na nani mchana? Usiku ni kiza kitupu. Hujui wala kuona uelekeako zaidi ya kelele za wadudu na vyura. Mchana, kila kitu kiko wazi. Hata ukifumba macho utaona tu.

Ikifika siku ya uchaguzi, chagua uwezekano na si matarajio na ahadi za urongo zisizo na rekodi yoyote ya utendaji. Chagua maendeleo na si maneno matupu. Kwani maneno matupu yanaliwa? Narudia. Mwenye macho haambwi tazama; na mwenye maninga haambiwi tazama. See you.