Ndemla bidisha 'guu' usirudi soka la Bongo

21Jan 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ndemla bidisha 'guu' usirudi soka la Bongo

HUU ni zaidi ya mwaka wa nne sasa huwa nasikia kiungo wa Simba, Said Ndemla, anatakiwa na timu za Ulaya.

Lakini cha ajabu ni kwamba mchezaji huo aliyetoka kwenye kikosi cha pili cha Simba, ameendelea kubaki hapa hapa, licha ya kila msimu kuwa na habari za kutakiwa kwenda kucheza soka nje ya nchi.

Ndemla mwenye umri wa miaka 22, Novemba mwaka juzi, alikwenda nchini humo kufanya majaribio kwenye klabu ya AFC Eskilstuna, lakini hakuna majibu yenye kueleweka yaliyowekwa wazi, matokeo yake alirejea na kuendelea kuitumikia Simba, tena kwa kusaini mkataba mpya.

Wakati kila shabiki wa soka akiwa amechoshwa na stori hizo za kila msimu, kiungo huo mwenye mashuti makali ya mbali yupo nchini Sweden akifanya majaribio mafupi katika klabu ile ile ya AFC Eskilstuna ya Ligi Kuu ya Sweden.

Kwa mujibu wa Meneja wa mchezaji huyo, Said Suleiman Sharrif, tayari kiungo huyo akiwa ameongozana na mshambuliaji mwingine chipukizi wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, Rashid Chambo wa JKT Ruvu, wameshaanza majaribio.

Kocha Mkuu wa klabu hiyo Nemanja Miljanovic, amesema hii ni nafasi nyingine ya mchezaji huyo kujiridhisha juu ya uwezo wake kwa majaribio mafupi tu wiki hii.

Baada ya muda mrefu, mimi naiona kama hii ndiyo nafasi pekee ya mwisho kwa Ndemla kudhihirisha ubora wake ili abakie Ulaya na kuanza maisha mapya.

Mashabiki wengi wa soka walikuwa wakimtabiria kuwa hatomaliza soka lake kabla hajacheza nje ya nchi.

Anachotakiwa kufanya ni kutowaangusha mashabiki wake kwa kufanya vema kwenye majaribio hayo.

Nadhani Ndemla atakuwa ametoka kambini kwenye klabu ya Simba na kwenda huko, na kama ni hivyo hilo litamsaidia sana kwenye majaribio yake, kwa kuwa wachezaji wengi wa Kibongo wamekuwa wakishindwa majaribio siyo kwa sababu hawana vipaji, bali uwezo wa kuhimili mazoezi magumu ndiyo tatizo.

Wengi wanakwenda kwenye majaribio wakiwa wametokea majumbani, wakiwa wamekaa wiki nzima kwenye maisha ya mtaani, hivyo kwenda huko mwili ukiwa umechoka, hawana nguvu wala stamina, hivyo kuonekana hawawezi kumudu mikikimikiki ya huko.

Kiungo huyo anatakiwa kufanya juhudi zote, ufundi wote na kuonyesha kipaji alichojaliwa nacho kwa sababu kama akifeli hapo, sidhani kama anaweza tena kupata nafasi adhimu kama hiyo.

Kwa sasa anaonekana kupoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba ambacho kina viungo kama Claotus Chama, Haruna Niyonzima na Hassan Dilunga, hivyo anatakiwa kutotaka tena kurejea nchini ili kukaa benchi.

Tumeona baadhi ya wachezaji wanaofeli majaribio na kurejea, baadaye wanashindwa kuendelea hata na zile timu walizokuwa nazo na kwenda kwenye klabu za chini yake.

Ndemla aepuke kurejea nchini na baadaye kwenda klabu za Mtibwa, Kagera Sugar, au Ndanda kama baadhi ya wachezaji huko nyuma, bali miguu yake ifanye kazi ya kumshawishi kocha ili amkubali na uwezo huo anao. Huu ndiyo wakati wake sasa wa kucheza Ligi Kuu Ulaya baada ya matarajio ya muda mrefu. Kila la kheri Ndemla.