Ndivyo Nyerere anavyoishi mioyoni mwa Watanzania

13Oct 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ndivyo Nyerere anavyoishi mioyoni mwa Watanzania

NYERERE amepumzika miaka 22 sasa, lakini ndoto zake na baadhi ya mambo aliyoyaasisi yanaendelezwa mojawapo ni ujenzi wa bwawa kubwa la umeme la Stigler’s Gorge, litakalozalisha kilowati 2,115 za umeme.

Baba wa Taifa katika uhai wake, alitamani kuwa na bwawa hilo, lakini hakufanikisha azma hiyo.

Huduma muhimu za jamii zinazohusisha kujenga kituo cha afya kwenye kila kata na zahanati kwenye vijiji vyote, kuongeza shule za msingi na sekondari na vyumba vya madarasa ya awali bila kusahau kujenga sekondari maalumu za sayansi kila mkoa kwa ajili ya wasichana ni miongoni mwa maono aliyoliachia taifa.

Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, mara nyingi wamekuwa wakieleza kuwa huduma za msingi za elimu, afya na maji zitawafikia Watanzania wote Bara na Visiwani.

Viongozi hao wanaamini kuwa kufanikisha miradi hiyo ya huduma za kijamii ni njia ya kuwanasua Watanzania kutoka dimbwi la ujinga, umaskini na maradhi, maadui wakuu wa taifa, walioatangazwa kwa mara ya kwanza na Mwalimu Nyerere baada ya uhuru.

Tukirejea kwenye umeme licha ya kazi ya ujenzi wa Bwawa la Nyerere kuanzishwa na hayati John Magufuli, miaka takribani 15 baada ya kifo cha Nyerere, Rais Samia Suluhu Hassan, anaahidi kuwa kazi zote za miradi ya umeme zitakamilishwa kama ilivyopangwa, wakati wa kipindi cha uongozi wa awamu ya tano. Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambalo hadi sasa limefikia kwenye hatua za kujengewa njia ya kusafirisha umeme na kuuingiza kwenye gridi ya taifa.

Kinachoendelea sasa ni TANESCO kupewa jukumu la kuanza ujenzi wa mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere hadi Chalinze yenye kilometa 167 ikibeba msongo wa kilovolti 400.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati anazungumzia kazi zilizoacha alama zinazofanywa na serikali, anasema mojawapo ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuvifikishia umeme takribani vijiji vyote.

Anasema vijiji 9,112 ilipofika Aprili 2020 vilikuwa vinawaka umeme na gharama iliyotumika ni Shilingi trilioni 2.27. Hivyo kazi iliyobakia ni kukamilisha kuvipa nishati hiyo vijiji vingine takribani 2000 kazi anayoahidiwa kuwa itafanywa kabla ya 2025.

Katika awamu hii serikali inatangaza kuendeleza mpango wa kujenga miradi miwili itakayozalisha megawati 580 za umeme wa maji ambazo ni Ruhudji na Mradi wa Rumakali iliyoko mkoani Njombe.

Ruhudji inatazamiwa kuzalisha megawati 358 wakati megawati 222 zitatoka kwenye mradi wa Ruamakali kazi iliyoanza mwaka jana ikitarajiwa kukamilika 2024 na kuongeza megawati 580 katika gridi ya taifa. Kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na umeme ni ndoto ya Mwalimu inayoishi, ikitaka Watanzania waondoke gizani.

Licha ya kufariki dunia miaka 22 iliyopita fikra na kazi zake zinaendelea kufanyiwa kazi na wadau hasa wana mapinduzi ndani ya CCM Tanzania pamoja na vyama vya ukombozi wanaojenga Chuo cha Uongozi cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere.

Taasisi hiyo ya kitaaluma inacholenga  kutoa mafunzo ya itikadi na uongozi kuendeleza fikra za uzalendo na umajumuni wa Afrika.

 Kazi ya kujenga chuo hicho inahusisha vyama sita vya ukombozi barani Afrika vya CCM ya Tanzania,  FRELIMO cha Msumbiji, ANC cha Afrika Kusini, SWAPO  kutoka Namibia, wakati Zimbabwe  ZANU-PF inashirika pamoja na  MPLA  chama kilicholeta uhuru wa Angola.

Licha ya kwamba ujenzi wa  Chuo cha Uongozi cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere, unaendelea wadau wa kisiasa wakiwamo viongozi wanapokitembelea na kukagua maendeleo wanatoa maoni mbalimbali yanayosifu kazi za Mwalimu na jinsi alivyokuwa muumini wa uzalendo, mpenda Afrika, mwanamapinduzi na gwiji la fikra zinazoishi na zitakazoendelea kudumu.