Ndivyo unavyodai fidia kutokana na madhara

09Nov 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Ndivyo unavyodai fidia kutokana na madhara

MADHARA ni matokeo hasi yanayompata mara nyingi mtu au kitu na wakati mwingine mali kutokana na kitendo kilichofanywa na mtu mwingine au kilichotokea kutokana na mtu flani kushindwa kutimiza wajibu.

Kutokana na madhara hayo mtu aliyeumizwa anastahili kupata fidia.

Ili kupata fidia, inampasa mtu aliyepata madhara hayo kufungua shauri la madai katika mahakama yenye mamlaka ili ipime madhara yaliyotokea na kuamuru kulipwa fidia au kutolipwa na ya namna gani.

Ili kufanikiwa katika shauri la kudai fidia kutokana na madhara yaliyosababishwa na mwingine au mwingine kushindwa kutimiza wajibu wake mambo yafuatayo inabidi yathibitishwe mbele ya mahakama.

Mosi kuwe na wajibu wa kujali au wajibu wa kisheria upande wa mdaiwa fidia.

Wajibu huo uwe umevunjwa na mdaiwa fidia na uvunjwaji wa wajibu huo usiwe umechangiwa na anayedai fidia. Aidha, kuwe na madhara yanayotokana na uvunjwaji wa wajibu upande wa mdai fidia.

Mojawapo ya sheria zinazosimamia madhara inatoka katika Sura ya 310 ya Sheria za Tanzania kama ilivyorejewa mwaka 2002 (The Law Reforms (Fatal Accidents and Miscellaneous Provisions) Act).

Kuna namna mbalimbali ambazo mtu akishindwa kutimiza wajibu wake anaweza kusababisha madhara kwa wengine na kupelekea muathirika kufidiwa. Namna hizo ni kama wajibu wa mwenyeji kuhakikisha kuwa wanaoingia na kutoka kwenye eneo lake kwa halali hawadhuriki.

Mwenyeji ana wajibu wa kuhakikisha kuwa wote wanaoingia na kutoka katika eneo lake kihalali hawapati madhara.

Akishidwa kutimiza wajibu huo na madhara yakatokea, mtu aliyeumia anaweza kudai fidia. Baadhi ya mifano ya mambo yanayoweza kupelekea madhara kutokea na mtu kudai fidia chini ya wajibu huu ni pale ambapo aliyekwenda kwenye nyumba ya mtu au taasisi na kukuta sakafu inateleza kutokana na kupiga deki au asili ya sakafu bila kuwa na ilani (tahadhari) kuhusiana na hali ya sakafu hiyo na mtu akateleza au akaanguka na kuumia.

Inaweza kutokea endapo mtu amepanda gari la mtu mwingine na gari hilo likawa na viti vibovu na kupelekea abiria huyu kuumia au kupata ajali kutokana ubovu wa gari hilo.

Wajibu wa mtu kulinda hadhi na heshima ya mwingine chini ya wajibu huu, kila mtu ana wajibu wa kulinda hadhi na heshima ya mwenzie.

Iwapo atafanya lolote na kusababisha hadhi ya mwenzie kushuka, aliyefanyiwa hayo anaweza kudai fidia. Mfano wa uvunjifu wa wajibu huu ni pale A amefanya tendo au amesema maneno ambayo si maoni halali juu ya mtu B mbele ya watu wengine na kwa maoni ya hao watu wengine tendo lile au maneno yale yanashusha hadhi au yanamdhalilisha mtu B. Kisheria B anaweza kwenda kudai fidia.

Halikadhalika wajibu wa mtu kutoharibu raha na furaha ya mwingine, wajibu huu unamaanisha kwamba mtu hatakiwi kuwasumbua wengine walioko jirani naye.

Mfano wa uvunjifu wa wajibu huu ni pale ambapo mtu anasababisha karaha kwa kufungua mziki kwa sauti ya juu bila kibali au bila kuzingatia masharti ya kibali.

Jingine ni kusababisha harufu

mbaya kiasi cha kuwakosesha raha au kuwasumbua wengine. Wajibu mwingine ni wa mwenye mali au mwajiri kuhakikisha kuwa mawakala au wafanyakazi wanatimiza wajibu wao kwenye kazi au ajira haiwasababishii madhara kwao na kwa wengine.

Wajibu huu unamaanisha kwamba, mwajiri au mwenye mali ana wajibu wa kuhakikisha kuwa mawakala au waajiriwa wake hawasababishi madhara kwa wengine wakati wanatimiza majukumu yao ya kazi.

Mfano wa uvujifu wa wajibu huu ni pale ambapo mfanyakazi au mwajiriwa binafsi au kwenye taasisi au wakala akifanya kitu chenye kuleta madhara kwa mtu mwingie au juu ya mali ya mwingine wakati anatimiza majukumu yake. Hili likitokea aliyepata madhara, au mali yake anaweza kudai fidia kutoka kwa mwajiri au mwenye mali.

Mfano, mwingine ni pale ambapo mtu amepanda basi gari na akapata ajali au kuumia akiwa kwenye basi hilo na kapata madhara anaweza kudai fidia kutoka kwa dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo pamoja na mmiliki wa gari au basi hilo.

Mara nyingi hii ni pale ambapo basi au gari lilikuwa ni la biashara mfano mabasi yanayosafirisha abiria.

Wajibu wa watawala na viongozi kuhakikisha hawafanyi vitendo ambavyo vitawaathiri wananchi wao.

Chini ya wajibu huu, viongozi au watawala wanapaswa kujali na kufanya mambo ambayo hayaleti madhara kwa wananchi wanaowaongoza.

Mfano kiongozi anaruhusu takataka zitupwe kwenye eneo fulani ambalo lipo kwenye makazi watu. Cha kuzingatia ni kila mtu ana wajibu wa kujali na kuhakikisha kuwa kitendo chochote anachofanya hakisababishi madhara hasi kwa mwenzake.