Ndugu zangu wauza mafuta Mwanza, mteja ni mfalme

21Nov 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ndugu zangu wauza mafuta Mwanza, mteja ni mfalme

‘MTEJA ni mfalme’ ni usemi unaobeba nafasi fulani yenye ukweli katika jamii. Ni kauli inayotumika sana katika masuala ya uhusiano kibiashara, hasa kati ya mnunuzi na muuzaji.

Kimazingira, mteja ana nafasi kubwa ya kusikilizwa, pia kuhudumiwa kwa mengi, ajione ana haki kubwa mahali hapo.

Pamoja na kufika katika biashara zao, kunatakiwa mteja aheshimiwe katika nafasi muhimu, kuzingatia uamuzi wa kuja kupata huduma mahali hapo.

Kunaelezwa, iwapo mtu hataona umuhimu wa wateja katika biashara zako, basi wajue wako mbioni kuporomoka kibiashara.

Inaelezwa, nafasi ya kushuka biashara mara nyingi inaanzia katika kukosekana kauli au matendo mazuri kutoka upande wa muuzaji, kwenda kwa mnunuzi.

Mhusika wa mauzo anapotakiwa kuboresha biashara na mapokezi ya ombi hilo kutoka kwa muuzaji ikawa ubabaishaji, kunachangia wateja kukimbia.

Nirejee tena, neno ‘mteja ni mfalme’ lina maana kubwa kwa matendo na utawala wa kifikra, katika kujenga uhusiano wa pande hizo mbili husika na jamii kwa jumla.

Kuwapo biashara, iwe kubwa au hata ndogo, wamiliki wanatakiwa kuwa na watumishi waliosomea au kunadaliwa, kuhusu dhana nzima ya mapokezi bora, kwa ajili ya kuwakaribisha wateja wao, ikiwamo na kumuelewesha mteja wake. Ina maana kubwa sana.

Pia, mfanyakazi asipokuwa na lugha nzuri kwa wateja, ajue anaweza kuisababishia hasara sehemu anayofanya kazi, akiponzwa na kauli zake.

Jiulize nini mvuto hata mteja akapiga hatua hadu penye biashara,akachukua pesa zake na kufanya ununuzi, Iko wazi kuna sababu inayoambatana na msukumo.

Kwanini namtaka hayo? Nimejaribu kueleza kidogo umuhimu huo, kutokana na ushuhuda wetu katika jamii; uhusiano wa muuzaji bidhaa na huduma, pia mnunuzi wake.

Mwanzo ni kwamba, wafanyabiashara wanaingia gharama kubwa katika kutangaza bidhaa zao, ili zitambulike kwa jamii wanakopatikana wateja.

Hilo hufanyika, huku katika baadhi ya biashara zinaumizwa na sehemu ya watendaji wake wasio na lugha nzuri kwa jamii kwa jumla. Hatima ni hasara, baadhi ya biashara zinatumbukia shimoni kwa bidhaa ‘kudoda’

Katika hilo hapo nina ushuhuda hasa ulionifanya kuwasilisha hoja hii. Nakumbuka siku ya wiki moja iliyopita mwaka huu majira ya jioni, katika kituo kimojawapo cha mafuta, jirani na hospitali kubwa ya jijini Mwanza, niliwashuhudia vijana wawili wanaotoa huduma ya biashara hiyo.

Cha kushangaza ni pale nilipowaona vijana hao wauza mafuta,walitoa kauli isiyofanana na ufanisi wa biashara.

Mteja alipofika, akitaka kuwekewa mafuta na ana pesa kubwa inayohitaji chenji, alikatizwa katika lugha fupi ‘haiwezekani’ na akatakiwa aende mjini ndiko kwenye chenji.

Hilo halikuwa kwa mteja mmoja, bali wengi. Ilinisikitisha sana, kwani nilishuhudia malalamiko mengi kutoka kwa wateja hata nao walishangaa hayo.

Mimi nikiwa mmoja wao, kinachoshangaza ni kituo hicho cha mafuta kinashindwa kutafuta mbadala wa kukabili hali hiyo, kwenda benki inashindwa kuchukua pesa benki zitakazowasaidia kurudisha chenji na wateja wao kunufaika kibiashara kwa ufasaha.

Vivyo hivyo, inapendeza dhana ya huduma kwa wateja kutawala, ili kuwapo kauli bora na yenye busara zaidi.

Mnapowaambia wateja waende mjini kuchukuwa mafuta, je, mnategemea kwa lugha hiyo, kesho wataendelea kushiriki biashara zenu?

Kwa mara mwisho niwatamkie tena tamathali ‘Mteja ni Mfalme’ ndugu zangu wa vituo vya mafuta.