NEC imeweka wazi, kazi kwa wanasiasa

05Aug 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
NEC imeweka wazi, kazi kwa wanasiasa

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inawakumbusha wanasiasa kuwa makini wakati huu ambao hatua mbalimbali zinachukuliwa, kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Katika mkutano wake na wadau wa siasa wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa uliofanyika wiki iliyopita, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, anawataka wanasiasa kuwa makini ili baadaye wasije kulalamika.

Umakini huo unaoelekezwa kwa vyama vya siasa ni pamoja na kuchagua watu makini, ili kuepusha migogoro baina yao na NEC pale wanatakapotakiwa kukamilisha mchakato wa kupitisha majina ya wagombea.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, uteuzi huo unahusu wagombea urais na ubunge, hivyo wahusika wanatakiwa kujaza fomu za tume hiyo kwa usahihi bila dosari ili wasije kukosa sifa za uteuzi na kuanza kulalamika.

Katika hilo, mwenyekiti huyo anatoa angalizo kwamba, malalamiko yote ya wanasiasa yasiwekwe kwenye mitandao, bali yapelekwe katika tume, kwa kuwa haijihusishi na mitandao.

Hatua hiyo ya tume inaonyesha wazi kwamba inataka mchakato huo uwe huru na wa haki na hata hadi kufikia kwenye uchaguzi mkuu wenyewe, ili kila mwanasiasa avune alichopanda.

Kwa maana hiyo ni wajibu wa vyama vya siasa kuzingatia kile ambacho kimeelekezwa na chombo hicho cha kusimamia uchaguzi ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima, bali kila mmoja ashindwe au ashinde kihalali.

Tayari NEC imeshakutana na wadau hao kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo na ni wazi kwamba kila mmoja ametoa dukuduku lake kwa lengo la kufanikisha mchakato na kuona kuwa kila kitu kinakwenda sawa.

Hivyo kinachofuata sasa ni wanasiasa wenyewe kuzingatia maelekezo ya mwenyekiti huyo kwa kuyafanyia kazi kwa usahihi aliyowaeleza ili asiwepo mtu wa kulalamikia kwenye mitandao ya kijamii.

Kama tayari tume imewapa nafasi ya kutoa dukuduku na kuelekeza jinsi ya kutoa malalamiko pale linapojitokeza kosa au dosari, inatarajia kwamba wahusika watazingatia kila hatua.

Baadhi ya wadau wamekuwa wakiilalamikia NEC wakiwa vyama vikuu vya upinzani kila mwaka wa uchaguzi kuhusu uwezo wake wa kiutendaji, huku vikidai kwamba, havina imani nayo.

Vinadai kwamba tume hiyo inashindwa kutekeleza matakwa ya kidemokrasia kwa vyama vya siasa na wananchi na katika uendeshaji wa uchaguzi na daftari la kudumu la wapigakura.

Chombo hicho kimekuwa kikitupiwa lawama nyingi ikiwamo utendaji wake na wapinzani mara zote wamekuwa wakilalamika na kutaka kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi isiyoegemea upande mmoja.

NEC imeshatoa ratiba ya uchaguzi huo utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, 2020 huku kampeni zikitarajia kuanza mwezi huu (Agosti 16) hadi 27 Oktoba 2020 na uchaguzi mkuu kufanyika Jumatano.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kwa kuzingatia ibara ya 41 kifungu cha nne cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 pamoja na marekebisho yake, ikiambatana na vifungu kadhaa katika Sheria ya Uchaguzi na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya 292, inatoa kibali kwa tume hiyo kutangaza ratiba ya uchaguzi.

Ni katika muktadha huo Jumatano Oktoba 28, 2020 Watanzania watafanya uchaguzi mkuu kwa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge pamoja na madiwani.

Kwa mara ya kwanza, taifa litaondokana na mazoea ya kufanya uchaguzi mkuu Jumapili ya mwisho wa mwezi Oktoba. Hatua, ambayo inapokelewa na Watanzania wengi kwa sababu itatoa fursa kwa watu wengi kushiriki pamoja na kuendelea kuheshimu uhuru wa kuabudu.