Neema mpya ya madereva wetu kujihami na corona

28May 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Neema mpya ya madereva wetu kujihami na corona

HIVI karibuni serikali iliwataka madereva wa malori nchini kuchukua tahadhari dhidi ya mambukizo ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakula vyakula vitakavyolinda kinga zao za mwili.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW), Ummy Mwalimu, wakati akizungumza na baadhi ya madereva wa kampuni mbalimbali za malori zinazosafirisha mizigo nje ya nchi waliofika katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, iliyoko Mabibo jijini Dar es Salam, kwa ajili ya kupima kama wana maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona au la.

Waziri Ummy anasema ugonjwa wa corona bado upo, ingawa ukweli wa upande wa pili ni kwamba maambukizo yamepungua.

Jambo muhimu hapo ni kwa wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya. Hiyo inajumuisha kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na majisafi yanayotiririka, kuvaa barakoa, pia kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mwingine.

“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa kwa ajili ya kupima virusi vya corona, kama mtakutwa hamna maambukizo ya ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwamo machungwa, mananasi, malimau, mboga za majani na tangawizi.

“Hii itawasaidia kinga zenu za mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga nyungu,” anasema Waziri Ummy.

Kaimu Mkurugenzi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, Ambele Mwafulango, anasema pamoja na kupima vipimo vya wagonjwa wengine kwa upande wa madereva walioko jijini Dar es Salaam, kwa siku wanawapima madereva 200 walioko mikoani na kuna utaratibu maalum wa kuchukuliwa sampuli zinazotumwa Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo.

Majibu ya vipimo hivyo yanatoka baada ya saa 48 kama madereva hao watakutwa hawana maambukizo na watapewa vyeti vinavyotumika kwa siku 14, itakayowasaidia kwenda kupeleka mizigo nje ya nchi, bila ya kupimwa tena katika nchi wanazokwenda.

Mwafulango anasema kabla madereva hao hawajafanyiwa vipimo vya corona, wanapimwa joto la mwili na wale ambao watakutwa na joto la juu la mwili watapewa huduma ya haraka zaidi ukilinganisha na wale ambao joto lao la mwili liko sawa.

“Madereva ambao tunawakuta hawana maambukizo ya ugonjwa wa corona tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wanapokuwa safarini siku zote.

“Katika maabara hii ya Mabibo, tuna mashine mpya tano ambazo ndani ya saa 24 zinapima vipimo 1,800 hii imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR jijini Dar es Salaam.

“Tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo 300 hadi 400, jambo lililokuwa linachelewesha utendaji wetu wa kazi,” alisema Mwafulango.

Serikali imetenga utaratibu maalum kwa ajili ya madereva wa malori wanaosafirisha mizigo nje ya nchi ambao wanafanyiwa vipimo vya ugonjwa wa corona kabla ya kusafiri, ili kuhakikisha hawana maambukizo na kuwaepusha kupata usumbufu ambao utajitokeza wanapokuwa safarini.