Ngoma ikivuma sana hupasuka

09Nov 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ngoma ikivuma sana hupasuka

NGOMA ivumayo sana kutokana na kupigwa huishia kupasuka. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kwamba jambo lolote huharibika hasa linapopita kipimo chake.

Hapana shaka hivi ndivyo ilivyo kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambaye ana makazi yake nchini Ufaransa.

Mkongomani huyu alikuwa anawatumikia "mabwana" watatu kila mmoja akipewa muda wake. Kuna wakati huwa na timu ya DR Congo kwenye michuano ya kimataifa. Pia huitembelea familia yake inayoishi Ufaransa na baada ya hapo huja kibaruani Dar es Salaam kuifunza Yanga.

Wahenga hawakukosea waliposema: “Mshika mbili moja humponyoka.” Kwamba anayevishika vitu viwili lazima ataponyokwa na kimoja. Hutumiwa kumwelimisha mtu mwenye tamaa nyingi na kumkumbusha kuwa hawezi kufanikiwa katika yote ayatakayo.

Kadhalika walisema “Ngoma ikivuma sana hupasuka.” Maana yake ngoma ivumayo sana kutokana na kupigwa huishia kupasuka. Methali hii hutumiwa kutukumbusha kwamba jambo lolote huharibika hasa linapopita kipimo chake.

Nani asiyejua au kukumbuka jinsi Zahera alivyopendwa na mashabiki na wanachama wa Yanga. Alikabidhiwa timu wakati Yanga ilipokuwa katika hali ngumu. Ilishindwa kusajili wachezaji wazuri na hata waliosajiliwa hawakupewa fedha za usajili.

Kwa sababu hiyo Yanga haikuwa na fedha; hivyo ikawa shida kupata wachezaji wazuri. Zahera alipambana na hali hiyo bila kuchoka kwa kuanzisha michango kutoka kwa wanachama na wapenzi wa timu hiyo.

Msimu uliopita timu ya Yanga pamoja na udhaifu wake wa hali na mali, iliweza kucheza mechi 10 bila kupoteza hata mmoja lakini ikafungwa na Mwadui ambayo pia ndio iliyovunja mwiko wa Simba kutofungwa msimu huu kwa kuifunga bao 1-0.

Mh! Mpira unadunda na ni mchezo wa bahati wasemavyo Waingereza kuwa “football is a game of chance.” Timu yaweza kuitawala nyingine kwa muda mrefu mchezoni lakini kosa moja tu likatosha kubadili mwelekeo na kuwashangaza watazamaji!

Nadhani mapenzi ya wanachama na mashabiki wa Yanga yalimvimbisha kichwa Zahera kiasi kwamba yeye ndiye aliyekuwa kila kitu pale Yanga: kocha, msemaji, mchangishaji hela, na taratibu akawa mzungumzaji kuliko viongozi waliomsajili!Sijui mkataba wake ulivyo na kwa nini alisajiliwa ilhali ni kocha msaidizi wa timu ya nchi yake (DRC). Hii ilimpa nafasi ya kwenda kuitumikia timu ya nchi yake kila ilipokuwa kwenye michezo ya kimataifa.

Msimu huu ulipoanza, tena baada ya kusajiliwa wachezaji aliopendekeza, ghafla hali ikawa tata (mwendo wa polepole wa kumatamata kama wa mtoto anayejifunza kwenda; hali ya kutoeleweka). Ikawa hata wachezaji kutoelewana uwanjani!

Timu ilipotoa sare au kufungwa, Zahera alikuwa wa kwanza kulalamika na kwa kiasi kikubwa akiwatupia lawama wachezaji wake kwa “kutofuata maelekezo yake!”

Kadhalika alijitetea akisema baadhi ya viwanja havifai kwa mchezo wa kandanda. Ni kweli viwanja vingi humu nchini si vizuri lakini mbona timu zingine hushinda?

Sasa mahaba ya viongozi, wanachama na mashabiki hayapo kwa achezaji aliopendekeza wasajiliwe.

Kwa mfano anasema hakuona sababu wala umuhimu wa kusajili walinda milango watatu.

wa mara ya kwanza tangu alipotia saini mkataba wa kuitumikia Yanga, alirushiwa chupa za maji na makopo. Kama hiyo haitoshi, akatukanwa na mashabiki wa Yanga jijini Mwanza baada ya Pyramids ya Misri ilipowafunga mabao 2-1.

Ingawa baadhi ya watu walimshauri ajiuzulu, yeye aligoma katakata akisema hawezi kushurutishwa wala kufukuzwa na wanachama ila na viongozi. Pia akasema haogopi mkataba wake kuvunjwa. Akasema wanaoweza kuuvunja mkataba wake ni viongozi wa Yanga lakini apewe stahiki zake.

Hata hivyo alisema hana tatizo kabisa kuondoka Yanga na wala hana shaka na uamuzi wao lakini angesema hali aliyopambana nayo kwenye klabu ya Yanga hata kuwashangaza wanachama na mashabiki!

Mtu akimwona mwingine au wengine wanavunja sheria kisha akaamua kunyamaza, yeye pia anavunja sheria na anastahili lawama na kushitakiwa. Kwa nini sasa Zahera ndio yuko tayari kufichua mambo aliyokutana nayo akiwa Yanga mpaka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo washangae?

Kwa nini hakusema wakati ule ili kuondoa sitafahamu (hali ya watu kutoafikiana kimawazo, kutoelewana au kusikizana juu ya jambo) katika klabu aliyokuwa akiitumikia ila anasema sasa baada ya kufukuzwa?

Wakati viongozi wakiwa kwenye hekaheka ya kupata mwalimu mwingine badala ya Zahera, aliyekuwa mchezaji na baadaye mwalimu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ndiye aliyeteuliwa kuifundisha timu hiyo kwa muda mfupi.

[email protected]

0784 334 096