Nguvu hizi kupandisha  timu Ligi Kuu zitazamwe

22Jan 2018
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Nguvu hizi kupandisha  timu Ligi Kuu zitazamwe

KUMEKUWA na malalamiko kila kona kwenye mechi za Ligi  Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Baadhi ya viongozi wamekuwa wakilalamika kuwa timu zao zimekuwa zikifanyiwa hila na waamuzi, ili zifungwe kwa manufaa ya timu fulani.

Hii si mara ya kwanza kuwapo kwa malalamiko kwenye Ligi Kuu Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Bado mashabiki wanakumbuka sababu ya Mbao FC kupanda Ligi Kuu. Ni kutokana na sakata la Polisi Tabora, Geita Gold, JKT Oljoro na Kanembwa JKT.

Nilitegemea kuwa huenda msimu huu hali inaweza kuwa nzuri.

Lakini bado hata msimu huu kuna malalamiko kuwapo kwa timu  zinazodaiwa kutumia mbeleko kwa ajili ya kuhakikisha kuwa  zinapanda Ligi Kuu.

Pia kuna nguvu halali ambazo pia nimezisikia za mikoa kadhaa  kuhakikisha kuwa timu zao zinapanda Ligi Kuu na zile ambazo zilishawahi kuwapo na zilishuka zinarejea tena.

Binafsi, napingana na nguvu haramu ambazo zimekuwa zikiripotiwa  kutaka kuzipandisha baadhi ya timu kwa lazima, ili mradi tu zipande Ligi Kuu msimu ujao.

Lakini naunga mkono nguvu halali kama za kuwapa motisha  wachezaji, posho, kambi nzuri na ahadi kemkem ili kuwafanya kujituma na kusababisha wapate ushindi.

Kwa mfano mwaka huu kuna pilikapilika msimu huu kutokana na kuwa na idadi kubwa ya timu zitazotarajiwa kupanda.

Shirikisho la Soka nchini (TFF), limesema kuwa msimu ujao linataka kuwa na idadi ya timu 20 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara,  hivyo zinatakiwa kupanda timu sita msimu huu kwenye Ligi Daraja  la Kwanza, huku mbili za Ligi Kuu zikishuka.

Idadi hiyo ndiyo zinawatia wazimu viongozi mbalimbali vya vyama vya soka na serikali mikoani, na mashabiki wa timu hizo kuhakikisha timu zao zinakuwa miongoni mwa zitakazopanda.

Sina tatizo na zitakazopanda kwa njia halali, lakini kuna kitu  ambacho siku zote huwa kinanitatiza.

Hivi kwa nini baadhi ya viongozi wa klabu, vyama vya soka, serikali  mikoani, na mashabiki hutumia nguvu nyingi halali na haramu  kupandisha timu kwenye Ligi Kuu halafu zikishapanda  huzitelekeza?

Tumeshawahi kuona huko nyuma baadhi ya timu zikipanda, zikiwa  na hamasa kubwa, lakini zikishafika Ligi Kuu zinakuwa na ukata  wa kutisha.

Zingine huungana na kuwa kitu kimoja zikiwa chini, lakini zikipanda Ligi Kuu tayari migogoro huanza na kuifanya timu  kutofanya vizuri.

Mfano mzuri ni Coastal Union ya Tanga. Timu hii imeshuka na kupanda mara mbili hivi kwa kipindi cha hivi karibuni, lakini umoja huwa wakati wa kuipandisha, ila ikishafika Ligi Kuu, viongozi wao wanaanza migogoro na kuifanya timu kuwa nyanya na hatimaye kushuka. Hata African Sports ilipanda na kushuka kwa staili hiyo hiyo.

Kwa kuwa zinatakiwa timu 20 msimu ujao, basi angalau ziwe  zimepanda kwa uwezo wao wenyewe na si kubebwa ili kuwe na Ligi  Kuu bora Tanzania kama ambavyo angalau tumeanza kuona msimu huu.

Hatutarajii kuziona timu zilizopanda kwa kubebwa ili ziwe timu za kuchukulia pointi kirahisi na kuifanya ligi kuwa dhaifu.

Wito wangu pia ni kwa nguvu halali zinazotumiwa kuzipandisha timu ziendelee pia timu zinapokuwa Ligi Kuu na si kutumika wakati  wa kuzipandisha tu na kuzitelekeza.

Lengo ni kuifanya Ligi Kuu kuwa na idadi ya timu 20 ambazo zote zitakuwa na uwezo wa kupambana uwanjani, lakini pia zikiwa na  uwezo wa kiuchumi ili kuleta ushindani na kuinua soka la Tanzania.