Ni halali kujadiliana na DDP, kufutiwa kesi

16Nov 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Ni halali kujadiliana na DDP, kufutiwa kesi

ZAMA hizi si tatizo tena kuanza kuwaza kuwa hivi inawezekana au sheria za Tanzania zinaruhusu washukiwa au washitakiwa kujadiliana na Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na kufikia makubaliano ya kumaliza kesi nje ya mahakama na hata kesi kufutwa?

Kimsingi, swali hilo limejibiwa na hata kama linaendelea kuwasumbua wachache ni jukumu lao kujua kuwa hakuna kikwazo na yote sasa yanawezekana.

Msingi wa makala hii ni hatua za hivi karibuni zilizofanyika nchini kufuatia ushauri wa serikali kwa washtakiwa wa makosa ya uhujumu uchumi kushauriwa kuomba radhi na kutubu mashtaka yao.

Serikali iliwaagiza wahusika kuandika barua kuamba radhi, kukiri makosa na kukubali kurejesha kiasi cha fedha wanachodaiwa. Kauli au ushauri huo wa Rais, John Magufuli,

Rais aliitoa Jumapili Septemba 22, 2019 akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, akimshauri Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasikiliza mahabusi wanaoshtakiwa kwa kesi za uhujumu uchumi.

Aidha, alitangaza kuwa wale watakaokiri, kuomba radhi na kukubali kurudisha fedha wanazodaiwa wasamehewe na kufutiwa mashtaka.

Alisema katika baadhi ya kauli zake:"Najua wanateseka. Unaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli. Inatia huruma na inaumiza. Najua wengine wanataka kuomba msamaha...wale ambao watakaoshindwa kuomba msamaha, waendelee kubanwa hata kama kesi zao zitachukua miaka 20."

MATOKEO

Baada ya ushauri huo matokeo ya utekelezaji wake yamekwenda kama ambavyo taarifa zimekuwa zikitolewa.

Itakumbukwa kuwa , Septemba 5 mwaka huu Bunge la Tanzania lilipitisha muswada wa maboresho ya sheria mbalimbali ikiwamo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo mapatano baina ya watuhumiwa na Mwendesha Mashtaka (plea bargain) yalipitishwa.

Kwa mabadiliko hayo yeyote kati ya mtuhumiwa, wakili wake ama mwendesha mashtaka anaweza kuanzisha mapatano hayo kwa kuifahamisha mahakama juu ya suala au nia hiyo ya kufanya majadiliano nje ya kizimba.

Kisha kuanzia hapo mahakama kwa upande wake haitahusika tena na makubaliano hayo.

Katika makubaliano hayo , mshukiwa au mshitakiwa anaweza kukiri tuhuma au sehemu ya tuhuma dhidi yake ili kupata afueni fulani ikiwamo kufutiwa mashitaka au kuondolewa baadhi ya mashtaka na hata kupunguziwa muda wa kutumikia adhabu au aina ya adhabu.

Halikadhakika, anaweza kutakiwa kulipa fidia ama kurejesha fedha ambazo zinahusishwa na kesi anayoshitakiwa nayo, kama ambavyo Rais alitangulia kushauri.

MUSWADA

Ni muhimu kusema kwa mujibu wa muswada huo, makubaliano hayo yakishafikiwa, yatapelekwa au kuwasilishwa mahakamani ili kutambuliwa rasmi, lengo ni mahakama katika hatua ya awali, ijiridhishe kuwa hayakuingiwa kwa shuruti.

Bado, mshukiwa atatakiwa kula kiapo cha kukubaliana na makubaliano hayo, pamoja na mhusika kusomewa haki zake za msingi ikiwamo “kumuondoshea haki ya kukata rufaa” isipokuwa kuhusu kurefusha muda au kipindi au uhalali wa hukumu atakayopatiwa.

MUHIMU

Makubaliano hayo kwa mujibu wa muswada hayatafanyika kwa watuhumiwa wa makosa kama udhalilishaji wa kingono ambayo adhabu yake inazidi kifungo cha miaka mitano ama inahusisha walalamikaji wa chini ya miaka 18.

Mengine ni mashtaka ya uhaini, kumiliki ama kusafirisha dawa za kulevya ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh. milioni 10, ugaidi, kukutwa na nyara za serikali ambazo thamani yake ni zaidi ya milioni 10 bila kibali maalumu cha maandishi cha DPP.

Isitoshe, ni mshitakiwa pekee ndiye atatakiwa kuiandikia Barua Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka wa Serikali kwa kupitia Mkuu wa Gereza alipo na siyo wakili wake au mtu mwingine yeyote.

Halikadhalika , muswada huo, kwa mujibu wa utaratibu, kama ilivyo kwa miswada mingine, baada ya kupitishwa na Bunge ulisainiwa na rais hivyo wenyewe ni sheria rasmi na halali kuanzia hapo.

Ibara ya 97(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977; kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara.