Ni hatari hata waliokufa wanapokeketwa

07Feb 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Ni hatari hata waliokufa wanapokeketwa

Katika kongamano la kupinga ukeketeji kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu lililofanyika Singida mwishoni mwa wiki hii, imebainika kuwa baadhi ya mila hukeketa hata watu waliokufa.

Taarifa hii iliyotolewa kwenye kongamano hilo lililoshirikisha wadau kutoka mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji nchini, ilishitua washiriki wengi.
Washiriki hao walitoka katika mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Singida na Dodoma.
Kumbe kuna baadhi ya watu wanaoendelea kufanya ukatili wa kijinsia kwa kisingizio cha kuendeleza mila potofu!
Wadau walioshiriki kongamano hilo lililoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu (UNFPA), wadau walielezwa kuwa vitendo hivyo vya ukeketeji kwa kuwa haviruhusiwi, wazee wa kimila huwafanyia kwa siri watoto wachanga, wanawake wajawazito na wanawake wanaokwenda kujifungua ambao hawajafanyiwa ukeketaji.
Aidha, watu wanaondekeza mila hizo potofu hudiriki kukeketa maiti za wanawake ambao watagundulika hawakufanyiwa ukeketaji wakati wa uhai wao.
Washiriki katika kongamano hilo wakiwamo wakuu wa wilaya, wabunge, makatibu tawala, mahakimu, viongozi wa dini, makamanda wa polisi, asasi zisizo za kiserikali, wanafunzi, wakuu wa madawati ya kijinsia, mahakimu na waandishi wa habari, walielezwa jinsi mila hiyo inavyoathiri wanawake wengi nchini na kushindwa kushiriki ipasavyo kwenye shughuli za maendeleo.
Kwa mijibu wa takwimu zilizotolewa katika mkoa wa Singida kwa kipindi cha mwaka 2013-2015, ulikuwa unaongoza kwa matukio 9,386 ya ukeketaji katika wilaya za mkoa huo za Ikungi, Iramba, Mkalama, Manyoni na Singida.
Imedaiwa kuwa sababu za kuwafanyia wanawake ukeketaji ni kuondoa mikosi katika familia wanazotoka kama vile kuzaa watoto wasiiona au wenye magonjwa ya akili.
Aidha, imedaiwa kuwa watoto wa miaka mitano kwenda chini hufanyiwa ukeketaji.
Athari zinazoweza kumpata mwanamke aliyekeketwa ni kupogeza maisha kutokana na kupoteza damu nyingi wakati anapofanyiwa kitendo hicho, na hata kama atapona wakati wa kujifungua hupata maumivu makali sana kutokana na njia ya uzazi kushindwa kupanuka kwa sababu ya kovu alilolipata wakati alipokeketwa.
Vilevile mwanamke hukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa na pia anaweza kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na vifaa vinavyotumiwa na baadhi ya mangariba kutokuwa salama.
Changamoto kubwa inayojitokeza katika kukomesha tatizo hilo ni wanawake wenyewe kuwapeleka kwa siri watoto wao kufanyiwa ukeketaji na mangariba. Imeelezwa kuwa baadhi ya mangariba hutumia ukeketaji wa kutumia uzi kuwafunga watoto wa kike wachanga sehemu zao siri ili ikatike taratibu bila kijulikana na watu wengine. Aidha wengine hutumia magadi kuwasugua watoto hao sehemu zao za siri ili kukamilisha ukeketaji huo.
Hatahivyo, suala kubwa la kujiuliza pamoja na athari zote hizo kutokea kwa nini suala la ukeketaji linaendelea kutesa baadhi ya mikoa na wakati mwingine wanawake kukosa hata fursa za uongozi kwa sababu tu hakupitia mila hiyo ya kukeketwa?
Taasisi zisizo za kiserikali, wanaharakati wamejitahidi kutoa elimu kukomesha suala hili, lakini bado kuna watu wachache wanaokwamisha.
Baadhi ya wadau wameonyesha wasiwasi kuwa huenda serikali haijatilia mkazo suala hili kama yalivyo natatizo mengine.
Wamedai kuwa kama kungeundwa chombo maalumu
cha kupambana na suala hilo kama vile ilivyo kwa Tume ya Kupambana na Ukimwi (TACAIDS), pengine watu
wangeona umuhimu wa kupambana na tatizo hilo.
Watoto waliopata uelewa wa tatizo hili hukimbia nyumbani kwao mara tu wanapobaini wazazi wao kutaka kuwafanyia kitendo hicho. Wengi wa wazazi hao huwafanyia watoto wao wa kike tohara ili waweze kuolewa kwa madai kuwa bila kufanyiwa hivyo hawawezi kupata wachumba. Watoto hao hukatizwa masomo na kufifishwa ndoto zao za maendeleo.
Wengi wa watoto wanaokimbia hukosa makazi salama na kuishia kuishi kwa wasamaria wema au taasisi zinazojitolea kuwahifadhi.
Watoto hawa wanahitaji msaada mkubwa ili wakombolewe kwenye janga hili.
Viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, taasisi zisizo za kiserikali na wadau wengine ni jukumu letu kupambana na kutokomeza Mila hii potofu.
Kuna umuhimu pia wa kujenga vituo vya kuhifadhia wasichana wanaokumbwa na tatizo hili kwenye mikoa inayoendelea kuendekeza mila hiyo.
Umoja ni nguvu, tukipambana kwa pamoja tutashinda.

[email protected], simu: 0774466