Ni hatari mtoto kujisaidia kwenye nguo -1

17Apr 2016
Jackson Paulo
Nipashe Jumapili
Afya
Ni hatari mtoto kujisaidia kwenye nguo -1

IWAPO mwanao ana tatizo la kujisaidia kwenye nguo licha ya kwamba ana umri ambao alitakiwa kutumia choo fahamu kuwa hilo si jambo jema kuna hitilafu zinazohitaji kushughulikiwa.

Hii ni kwasababu inaweza kuwa taabu kubwa kwako kama mzazi au mlenzi kwa vile wengi hudhani kuwa mtoto anayejisaidia kwenye nguo zake labda ana utovu wa nidhamu, mjinga au ni mvivu wa kutumia choo pale anapopaswa kufanya hivyo.

Ukweli ni kwamba, watoto wenye umri wa kuzidi miaka minne ambao wanajua kutumia choo, wanaojisaidia kwenye nguo zao wana tatizo lijulikanalo kitaalamu kama ‘encopresis’.

Hawa wana tatizo tumboni na huathiri mfumo wa kawaida wa kujisikia na kuhudhuria chooni na hushindwa kudhibiti kabisa haja kubwa hali inayowasababishia kujisaidia kwenye nguo.

Kwa kuwa kila mtoto anazaliwa na uwezo tofauti katika kuwa na ufahamu wa udhibiti wa haja kubwa, suala la matabibu halichukuliwa kwa uzito, hali ya mtoto kujisaidia kwenye nguo huonekana tatizo mpaka pale mtoto anapofikisha umri wa angalau miaka minne.

Encopresis ni tatizo linalowakumba takribani watoto kati ya asilimia moja hadi mbili ya watoto wenye umri chini ya miaka 10 na tatizo hili huwapata zaidi watoto wa kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa mara tatu hadi sita zaidi.

NINI CHANZO

Mara chache ‘encopresis’ husababishwa na hitilafu ya kimaumbile au ugonjwa ambao mtoto anazaliwa nao. Katika matukio mengi, husababishwa na tatizo la muda mrefu la kufunga choo (‘constipation’). Unapofunga choo, kinyesi huwa kigumu, kikavu na inakuwia vigumu kujisaidia. Kwahiyo watoto wengi wana tabia ya kubana choo au kujikaza kila wanapohisi dalili za haja kubwa,

Baadhi wanaogopa maumivu watakayoyapata wanapokwenda kujisaidia jambo ambalo huwaletea kwenda haja kwenye nguo watakapokuwa wakubwa.

KUFUNGA CHOO

Swali linalofuata ni hili kufunga choo kunasababishwa na nini? Watu wengi hudhani kuwa tatizo la kufunga choo ni kutokwenda haja kubwa pengine kwa siku nzima au zaidi. Hata hivyo kufunga choo maana yake siyo tu kutopata haja mara kwa mara lakini pia kupata choo kigumu wakati wa kujisaidia au kuhisi maumivu wakati wa kujisaidia.

Kila mtu ana ratiba ya pekee ya kwenda haja, hata hivyo watu wengi wenye afya njema hawapati haja kubwa kila siku. Mtoto mwenye tatizo la kufunga choo hupata haja kubwa kila baada ya siku tatu au zaidi.

Muhimu zaidi ni kwamba mtoto mwenye tatizo la kufunga choo hupata choo kingi na kigumu pia huambatana na maumivu wakati wa kujisaidia.

Kwa watoto walio wengi wenye tatizo la kujisaidia kwenye nguo, tatizo hili huwaanza kwa kupata choo kikubwa au kupata maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa. Hali hii hutokea muda mrefu kabla ya tatizo na mtoto hataweza kukumbuka lolote hata akiulizwa.

Baada ya muda mtoto husita kwenda haja kubwa na kujikaza kwa kubana haja kwa kuogopa maumivu.Hali hii ya kubana haja hukithiri na kuwa mazoea yaliyojijenga kwa mtoto muda mrefu baada ya tatizo la kufunga choo.

Kwa kadiri mabaki ya chakula au kinyesi yanavyozidi kujikusanya kwenye utumbo mpana wa mtoto, utumbo hutanuka taratibu hali inayoitwa kitaalamu megacolon.

Utumbo mpana kadiri unavyozidi kutanuka zaidi na zaidi, mtoto hukosa uwezo wa asili wa kujua ishara za kupata haja kubwa.Hatimaye, hutokea hali ya ulegevu katika sehemu ya chini ya utumbo mpana.

Baadaye choo ambacho kimeshatengenezeka kwa kiasi kidogo kwenye hatua za awali kutoka sehemu ya juu ya utumbo mpana huanza kuvuja pembeni mwa kinyesi kilichotengenezeka tayari kilichopo sehemu ya chini ya utumbo mpana au kwenye njia ya kupitishia choo na kutoka nje bila mtoto kuzuia.

Katika hatua za awali ni kiasi kidogo sana cha choo ndicho hutoka nje ambacho hubakiza alama kidogo katika nguo ya ndani ya mtoto. Kawaida baada ya hali hii mzazi hufikiri kuwa pengine mtoto hasafishwi kikamilifu baada ya kujisaidia au wengine hawajali sana hali hii.

Baada ya muda mrefu mtoto hushindwa kuzuia na kuanza kupitisha choo chote kwenye nguo za ndani. Mara nyingi mtoto hajui kama ameshajisaidia kwenye nguo.

Kwa kuwa kinyesi hiki hakikupita katika hali ya kawaida kwenye utumbo mpana (hakijawa kinyesi halisi), mara nyingi rangi yake ni nyeusi hunata na kina harufu mbaya kuliko choo kilichofuata mchakato wa kawaida.

Baada ya muda mtoto mwenye tatizo la kujisaidia huweza pia kupatwa na shida ya ukosefu wa mawasiliano ya misuli inayofanya kazi ya kusaidia harakati za tumbo wakati mtu akijisaidia.

Kwa hiyo idadi kubwa ya watoto, mshipa ambao upo mwisho wa sehemu ya kutolea haja kubwa na ambao husaidia kudhibiti haja hujikaza badala ya kulegea mtoto anapojaribu kujisaidia. Hali hii ya mvurugano wa mawasiliano ya misuli hujulikana kitaalamu kama anismus na huleta ugumu kwa mtoto kusukuma choo chote wakati akienda haja kubwa.

Itaendelea