Ni hatari sana Simba SC, Yanga kwenda Manungu

22Jan 2022
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni hatari sana Simba SC, Yanga kwenda Manungu

KWA mara ya kwanza baada ya miaka 23, Mtibwa Sugar inaipokea Simba kwenye Uwanja wake wa Manungu, Turiani,mkoani Morogoro.

Inasadikiwa uwanja huo unaingiza watazamaji 1,000. Hata hivyo, Msemaji wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema lengo lao leo kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania bara ni kuingiza mashabiki 2,500.

Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeafiki mechi kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Simba kuchezwa kwenye uwanja huo.

Ni kweli uwanja umekidhi vigezo vyote vya kuchezea Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini nafikiri kwa mazingira na utamaduni wa soka la nchi hii, bado ulikuwa haukidhi vigezo vya kuzipokea timu zenye mashabiki wengi, si wa Simba tu, bali hata Yanga.

Katika mazingira ya nchi yetu na utamaduni wa Simba na Yanga ni timu ambazo zimebahatika kukusanya mashabiki kila kona ya nchi hii, tofauti na nchi za wenzetu Ulaya na hata nchi kadhaa Afrika, ambapo kila jimbo, mkoa eneo una timu zake, na mashabiki wake ni wa eneo husika.

Mfano huwezi kukuta mtu kutoka Kigoma akashabikia timu ya Dar es Salaam, lakini hii ni tofauti na nchi hii ya Tanzania. Huku ni Simba na Yanga.

Kama historia inavyojieleza, Simba haijaenda Manungu kiasi cha miaka 23 iliyopita, hiyo tosha itafanya kuwe na mashabiki wengi sana, hivyo kiusalama haitokuwa vizuri.

Ni kweli tumeambiwa usalama utakuwa mkubwa kwa mashabiki na mali zao, lakini ukweli unabaki pale pale Uwanja wa Manungu ni mdogo, hauwezi kuingia mashabiki watakaotoka Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na vitongoji vyake na hata mikoa jirani kama, Dodoma.

Tunaona mechi ambazo Simba au Yanga inacheza mikoani kwenye viwanja vikubwa kama Sheikh Amri Abeid, CC Mkwakwani, Ushirika, Ali Hassan Mwinyi, Sokoine na vingine vinajaa pomoni na kundi lingine la mashabiki linabakia nje ya uwanja, inakuwaje kwenye uwanja mdogo kama huo?

Hata kama Jeshi la Polisi na walinzi, wakikataza mashabiki wote waliotoka Dar es Salaam, Pwani na Morogoro mjini, na wakawaruhusu mashabiki wa Turiani tu kuingia, bado hautotosha.

Kinachotaka kufanyika hapo ni kuingia kiasi hicho cha watu tu, lakini inavyoonekana kabisa kazi itakayokuwapo ni kuwazuia watu waliokuwa nje kuingia uwanjani. Hiyo itakuwa ndiyo kazi kubwa namba moja ya Jeshi la Polisi na walinzi wengine kwenye mechi ya leo, achilia mbali ya pili ambayo ni kulinda ndani ya uwanja na mengineyo.

Nina uhakika mashabiki wengi kutoka Dar es Salaam, Pwani, vitongoji vya Morogoro na Dodoma watakuwepo uwanjani kila mmoja akitaka kujaribu kuingia kuangalia mechi hiyo, ndipo tatizo litakapoanza.

Mtu ametoka mbali kuja kuitazama Simba, unadhani atakubali kweli kuondoka kirahisi bila kuangalia mechi?

Kwenye mechi hizo pia hukusanya wanawake na watoto ambao nao baadhi watakuwa ndani ya uwanja na wengine nje, kitu ambacho ni hatari kama kuna baadhi watataka kulazimisha kuingia.

Hata kama watadhibitiwa kwa nguvu, lakini tayari kutakuwa na dosari ya baadhi ya watu kuumia.

Tumewahi kushuhudia maafa baada ya watu wakiwamo watoto hapa hapa nchini, kulazimisha kuingia uwanjani, si kwenye soka, bali kwenye masuala mengine ya kijamii, nadhani hatujajifunza kutokana na hilo.

Huko nje ya nchi tumewahi kushuhudia maafa kama hayo, baada ya mashabiki wa soka kulazimisha kutaka kuingia uwanjani.

Sisemi kama mechi itakuwa na vurugu, au lazima itokee leo, la hasha, lakini ukweli unabaki pale pale kuzichezesha Simba, au Yanga kwenye uwanja kama wa Manungu ni hatari.

Mtoto akicheza na wembe, hata kama haukumkata, lakini bado kuchezea kwake wembe ni jambo la hatari.

Nitoe wito tu kwa Bodi ya Ligi na TFF, hata baada ya mechi ya leo, iliangalie tena suala hili kwa jicho la tatu.

Hatuzitetei timu hizi ili zisicheze kwenye viwanja vya ugenini, lakini tunaangalia ukweli zinakuwa na mashabiki wengi, ambao pia baadhi yao wanakuwa na mambo mengi, ikiwamo mihemko kwa uwanja kama Manungu ni rahisi sana kuingia hata uwanjani wakati mechi inachezwa, au mara tu baada ya kumalizika.