Ni kudai Katiba mpya na kujipanga 2025

14Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni kudai Katiba mpya na kujipanga 2025

MOJA ya mambo ambayo ni ya kwanza kwa wanasiasa na wanaharakati kuyaomba kwa Rais Samia Suluhu Hassan, mara tu alipoingia madarakani, ni kukamilisha mchakato wa kupata Katiba mpya.

Pamoja na madai hayo, ipo haja ya kuwakumbusha wanasiasa kwamba,  Katiba mpya ije lakini wajipange kiuchaguzi. Ni kwa sababu mwisho wa uchaguzi huwa ni mwanzo wa maandalizi ya mwingine, kwani miaka mitano si mingi katika kujipanga.

Sasa ni miezi tisa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka jana, huku CCM ikiibuka na ushindi kuanzia kwenye udiwani, ubunge hadi urais. Kwa kuwa kumalizika kwa uchaguzi, huwa mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine, ingependeza kama vyama vya siasa vingejipanga ili kushiriki vyema katika uchaguzi mkuu wa 2025.

Maandalizi hayo ni pamoja na kuongeza wanachama wapya, kwa kujikita zaidi kwenye mashina na matawi ambako ndiko wananchi waliko, ili kuondoa dhana iliyojengeka kuwa vyama vya upinzani ni vya msimu.

Katiba mpya ni muhimu, lakini vyama kujiimarisha kuanzia ngazi ya chini ni jambo muhimu zaidi, kuliko kusubiri kuibuka wakati wa uchaguzi tu bila kuwa na wanachama wa kutosha wa kuviunga mkono.

Vyama kusubiri uchaguzi ni sawa na kusindikiza lakini vikiwa na wanachama wa kutosha, inakuwa ni rahisi kufurukuta na hata kufanikiwa kupata viti vya udiwani na ubunge.

Hivyo, wakati vikidai katiba, visisahau kujipanga vizuri kuanzia ngazi ya chini, kwani kufanya mikutano ya ndani kama ambavyo serikali inaelekeza, badala ya kubaki kudai katiba muda wote wakati havina wanachama wa kutosha.

Kwa maana nyingine, joto la kudai katiba mpya lisivifanye vyama vya siasa kuishia hapo, bali vipige hatua zaidi kwa kuendelea kujipanga zaidi ikiwa ni pamoja na 'kuvuna' wanachama wapya.

Uchaguzi mkuu hufanyika kila baada ya miaka mitano, na maandalizi ya uchaguzi mwingine hutakiwa kuanza, vinginevyo vyama  vya upianzani vinaweza kuendelea kusindikiza chama tawala.

Ikumbukwe kwamba, tangu uchaguzi wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1995, baadhi ya vyama vilivyokuwa na nguvu wakati huo, vimeendelea kuyumba na vingine kushindwa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu.

Inawezekana sababu mojawapo ya kuwapo kwa hali hiyo ikawa inatokana na  kushindwa kujiimarisha kwenye ngazi ya chini ambako ndiko waliko watu  wengi wanaoweza kujiunga katika vyama hivyo au kuviunga mkono.

Mtindo wa kuendelea kuvizia na kujitokeza katika uchaguzi bila kujiandaa, hauwezi kuvisaidia vyama vya upinzani, badala yake viongozi wangebuni mbinu za kufanikisha kushiriki katika uchaguzi na kupata matokeo chanya.

Yale ambayo yalikikumba Chama cha TLP, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, yangefaa kuwa fundisho kwa vyama vingine vya upinzani kwa kufanya maandalizi mapema kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, chama hicho kilikosa mgombea urais na badala yake kiliunga mkono mgombea wa CCM, kikidai kwamba hakikuwa na mgombea mwenye uwezo wa kupambana na wa CCM.

Hatua ya chama hicho kukosa mgombea urais, ni wazi kwamba hakikuwa na maandalizi tangu kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka 2015 na kujikuta kikipeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi ya urais.

Lengo la chama cha siasa ni kushika dola kwa njia halali ambayo ni kupitia sanduku la kura, hivyo ili chama kifanikiwe katika hilo, ni muhimu kuzingatia kuwa mwisho wa uchaguzi, ni mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine.