Ni lini sheria ya kutenganisha siasa, biashara itapatikana?

11May 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni lini sheria ya kutenganisha siasa, biashara itapatikana?

HIVI karibuni Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliwatangazia wabunge kuwa Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma inatarajia kupeleka muswada wa sheria bungeni ili kutenganisha biashara na uongozi.

Spika akawataka wabunge ambao wamezoea kusema ndiyo wajiandae kuisoma kwa umakini sheria na waelewe, kwa vile wengi wao wamekuwa wakichanganya na biashara ili kuweka mambo sawa.

Maana ya Spika ilikuwa ni kwamba wanaweza kupitisha sheria halafu wakaendelea na biashara na kujikuta wamejiweka pabaya, hivyo akawataka wawe makini.

Aliwatahadharisha wabunge ambao wamekuwa wakiunga mkono na kupitisha sheria mbalimbali kuwa makini kuhusu sheria hiyo na kwamba katika nchi zilizoendelea imekuwa ni kawaida mfanyabiashara anapokuwa mbunge anakabidhi biashara kwa mtu mwingine.

Nakumbuka suala hili la kutenganisha biashara na siasa halikuanza leo, kwani mwaka 2009 aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwahi kusema kuwa sheria hiyo ingepatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Lakini ajabu ni kwamba leo ni mwaka 2016 ndipo imeelezwa kuwa muswada huo utapelekwa bungeni ili ufanyiwe kazi na haijulikani kwenye utawala wa awamu ya nne ulishindwa nini?

Kuchanganya biashara na siasa ni mtego unaotakiwa kuteguliwa mapema kwa sababu wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakidaiwa kutafuta nafasi katika siasa ili kufanikisha biashara zao na siyo kutumikia umma.

Ninaamini kwamba kutenganisha biashara na siasa kutaweza kusaidia kuwadhibiti viongozi mbalimbali kurejesha angalau maadili ya viongozi wa umma kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Bila kutenganisha biashara na siasa, wananchi wataendelea kuwaona viongozi wao kama wasaliti na wanyonyaji wa rasilimali zao kwa kujilimbikizia mali nyingi ilhali maisha ya wananchi yakizidi kuwa magumu kadiri siku zinavyokwenda mbele.

Ninasema hivyo kwa sababu yapo matukio mengi tu ambayo yamekuwa yakiripotiwa sehemu mbalimbali nchini ya uharibifu wa mali za wawekezaji ambao wanasiasa unaofanywa na baadhi ya wananchi pale wanapobaini kuwa wameporwa ardhi.

Pamoja na hayo, bado inatakiwa ijulikane ni biashara gani ambayo kiongozi anazuiwa kuendelea kuifanya wakati wa utumishi wake kwa umma, ikizingatiwa kuwa viongozi wengi ambao ni pamoja na mawaziri ni wanahisa katika kampuni kubwa nchini.

Ni muhimu kujua ni biashara gani anazuiwa kiongozi asifanye. Kuna biashara ya makampuni makubwa, lakini pia kiongozi anaweza kufanya biashara ya duka nyumbani kwake.

Suala la kutenganisha siasa na biashara kama alivyosema Spika linatakiwa kujadiliwa kwa umakini na wabunge ambao baadhi wanahusika moja kwa moja na biashara zenye maslahi yanayogongana na nafasi zao kama viongozi.

Lakini cha msingi ni kwamba muswada huo ukifikishwa kwao ujadiliwe kwa mapama ili kulipatia uvumbuzi suala hilo
kwa manufaa ya umma na siyo watu wachache wanaonufaika na mtindo wa kufanya biashara na siasa.

Utawala Rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulijulikana kwa misingi inayozingatia usawa, kujali na kuwatumikia wanyonge, uadilifu na kuheshimu utu, misingi hiyo ndiyo iliyoendelea kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani.

Hata serikali ya Rais Magufuli imeliona hilo ndiyo maana sasa imeamua kupeleka muswada bungeni ili uwe sheria kwa ajili ya kuwadhibiti wale wanaoingia kwenye siasa ili kujitengenezea mambo yao.

Siyo siri kwamba dalili na vitendo vya waziwazi vya muelekeo wa kuibomoa misingi hii vimeanza kujitokeza vikiwamo vya rushwa, ufisadi, ubadhirifu, hivyo hatua zinazochukuliwa na serikali hii ili kuondoa uozo huo ni za kuunga mkono.