Ni muda wa kukimbia, siyo kutembea tena

13Apr 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni muda wa kukimbia, siyo kutembea tena

TANGU aanze kazi mara baada ya kula kiapo Novemba 5 mwaka jana, Rais John Magufuli, ameendelea kutimiza wajibu wake kama alivyoahidi kuwatumikia Watanzania bila woga wala kuwaona huruma wale ambao wanafanya mambo kinyume.

Mtindo wake huo wa kufanyakazi umeendelea kuwaweka ‘roho juu’ watendaji wa serikali wa ngazi mbalimbali hatua ambayo huenda ikasaidia kuwaamsha wale ambao walizoea kufanya kazi kwa mazoea.

Wapo ambao wamekuwa wakikosoa utendaji wa Rais Magufuli wakiwa na sababu zao mbalimbali, lakini binafsi ninadhani kwamba kinaachotakiwa kutazamwa hapa ni jinsi gani anavyorejesha nidhamu kwenye utumishi wa umma.

Ninasema hivyo kwa sababu siri kwamba baadhi ya watendaji walikuwa wanafanyakazi kwa mazoea na kufanya serikali kuonekana ya kawaida na ndiyo maana ilifikia wakati hata Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kuwaita mizigo.

Kwa hiyo kinachofanywa na Rais Magufuli sasa ni kuwafanya watendaji wa serikali yake kuachana na mazoea ya miaka ya nyuma na kutambua kuwa wako kwenye utawala mwingine ambao hautaki ubabaishaji.

Ili kuonyesha kuwa hataki ubabaishaji, juzi Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela na kuagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo, Abdul Dachi.

Sababu kubwa ya kutengua uteuzi huo ilitokana na mkuu huyo wa mkoa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu watumishi wa umma hewa kwamba hawapo mkoani kwake.

Imeelezwa kuwa Machi 20, mwaka huu, wakati wakuu wa mikoa wakiwasilisha ripoti ya watumishi hewa, Kilango alisema Shinyanga hakuna watumishi hewa na hivyo kusababisha Ikulu kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo kwa watumishi hewa 45.

Kazi ya kubaini watumishi hewa katika mkoa huo bado inaendelea na kwamba ingawa taarifa ya mkuu ya mkoa ilionyesha hakuna watumishi hewa, lakini tayari walikuwa wameshalipwa Sh. milioni 339.9.

Sijui mkuu wa mkoa alidanganywa hadi akatoa taarifa hiyo bila kutafakari kwa makini ili kujiridhisha! Lakini nadhani huu mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea ndiyo inaweza kuwa umesababisha hayo yote.

Ndiyo maana nikasema kuwa viongozi waache kufanya kazi kwa mazoea kwani mwisho wake wanaweza kuingizwa mkenge bila wao kujua na kujikuta kibarua kinaota nyasi.

Hata hivi karibuni wakati wa mchakato wa kumsaka Meya wa jiji la Dar es Salaam kulikuwa na 'figisufigisu', ambazo zilisababisha uchaguzi huo kuahirishwa mara kwa mara.

Ilifikia wakati baadhi ya watu kumpelekea msimamizi wa uchaguzi huo kupewa zuio feki ambalo lilisababisha vurugu katika ukumbi na kusababisha mwenyewe kuumizwa na baadhi ya wapigakura.

Hii inaonyesha ni jinsi gani watendaji wamekuwa na mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea, kwani alikuwa na nafasi na kulisoma kabla ya kutoa uamuzi na pengine vurugu zisingetokea kama angekuwa makini.

Sina maana kwamba RC Kilango alipewa taarifa feki na kuitolea maamuzi, bali nimetolea mfano huo mdogo wa uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es Salaam jinsi ambavyo msimamizi hakuwa makini hadi kukubaliana na uongo.

Hivyo ndivyo baadhi ya watendaji wa serikali walivyozoea kwa muda mrefu wakiamini kwamba hata ukitoa mkwara ni sawa na upepo wa kisiasa ambao hupita kisha mambo yakaendelea kama kawaida!

Wengi wao wamezoea siasa kiasi cha kuwaaminisha wananchi kwamba siasa ni uongo ndiyo wanasiasa wamekuwa hawaaminiki kwa sababu wanaeleweka kuwa ni waongo.

Rais Magufuli katika utawala wake ameonyesha kuwa hataki longolongo ofisini, kwa maana hiyo hata wale aliowateua wanapaswa kufanya kazi kwa mfumo huo ili kuendana na kasi yake.

Kikubwa ambacho wanatakiwa kutambua ni kwamba kila mtawala huwa anakuja na utaratibu wake wa kufanya kazi, hivyo wanaoteuliwa hawana budi kutambua hilo na kulifanyia kazi.

Kama hawajaona tofauti kati ya utawala wa Kikwete na Magufuli, basi watapata shida sana kwenda na kasi anayoitaka Rais Magufuli na mwishowe wataishia kumlaumu kwamba anaendesha nchi kidikteta.

Kwa mtazamo wangu ni kwamba nchi hii ilipofikia inatakiwa kupelekwa mchakamchaka ili irudi kwenye mstari na ndivyo Rais Magufuli anafanya ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakikosoa utaratibu huo.