Ni ngumu kudhibiti mashabiki viwanjani

22Jun 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni ngumu kudhibiti mashabiki viwanjani

HIVI majuzi serikali iliufungia Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuingiza mashabiki kutokana na kujaza idadi kubwa ya mashabiki, lakini pia kushindwa kufuata kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya juu ya udhibiti wa ugonjwa wa COVID-19 unaoletwa na virusi vya corona.

Hii ilikuwa ni baada ya mechi ya Jumatano iliyopita kati ya wenyeji JKT Tanzania dhidi ya Yanga iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara mashabiki walijazana kupita kiasi, baadhi wakiwa hawajavaa barakoa, lakini pia wakionekana wakikaa jirani na ile kanuni ya kuachiana mita moja haikuwapo.

Ingawa ugonjwa wa corona umepungua kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania, lakini bado upo, na serikali inahitaji kuudhibiti ili kutoleta maambukizi mengi mapya kwa wakati mmoja.

Ilionekana kwenye picha za televisheni, JKT Tanzania ilipopata bao la kwanza jinsi mashabiki wao, ambao kiuhalisia ni wa Simba, walikuwa wakishangilia kwa staili ya kulala upande mmoja, halafu wa pili (kulia na kushoto). Hali hii ilisababisha mashabiki kugusana na kuegemeana.

Hali kadhalika, Yanga nayo iliposawazisha bao, mashabiki wao walipagawa kwa furaha na kushangilia kwa staili ambayo haikutofautiana na ya wenzao.

Kusema kweli hali ilivyokuwa ilikuwa ni hatari kwa afya za mashabiki wa soka katika mchezo huo.

Hata hivyo, kwa maoni yangu nadhani adhabu ya kuifungia JKT Tanzania kucheza mbele ya mashabiki wao ni kubwa na mbali na kuiathiri timu hiyo, pia mashabiki na wadau wa soka watakosa burudani na michezo mbalimbali ya Ligi Kuu.

Ukiangalia umati ule, karibu asilimia 90 ulikuwa ni wa mashabiki wa klabu mbili kubwa nchini, Simba na Yanga.

Sidhani hata kama Uwanja wa Jamhuri usingefungiwa, ungejaza tena mashabiki wengi kama siku ile, ikizingatiwa tayari imeshamalizana na Simba mechi zote mbili.

Mimi nilidhani wa kuadhibiwa wangekuwa na wasimamizi wa uwanja huo ambao walijaza watu kupita kiasi kilichowekwa.

Kuna taarifa kuwa baada ya kuingia watu kiasi kilichowekwa, mashabiki walianza kuingia kwa njia za panya, yaani kulikuwa na tiketi za magendo ambazo zilisababisha watu kuwa wengi kiasi kile.

Halafu ukiangalia, ni kwamba umati ule haukutofatiana sana na ule wa Juni 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani, Shinyanga, wenyeji Mwadui walipocheza dhidi ya Yanga.

Mimi nadhani kama serikali imeruhusu mashabiki kuingia uwanjani, basi utaratibu uwe ni kwamba mashabiki wanaoingia wawe wamevaa barakoa, lakini pia kabla ya kuingia wanawe mikono na dawa, pia wasimamizi wawe makini kuwa na idadi maalum tu ya wanaingia na si vinginevyo.

Lakini tukisema watu wasikaribiane, kwenye mpira wa miguu ni ngumu sana.

Ikumbukwe soka ni mchezo wa hisia. Hata kama wakiruhusiwa watazamaji sita tu uwanjani, hutoona hata siku moja wamekaa mbalimbali. Ni lazima hao hao sita hata kama wamegawanyika, watatu wanashangilia timu moja na wengine nyingine, watakaa pamoja na kuanza kuzungumza, kutaniana, kujadili, kushangilia na makelele pia.

Umati wa mashabiki wa soka si umati waliokusanyika kwa ajili ya Injili.

Mashabiki wa soka siku zote wana mihemko, na wanataka wakae karibu karibu kwa ajili ya kuzodoana, wengine ambao ni timu moja watakaa ili kupeana moyo, kushangilia kwa pamoja na hata kusikitika kwa pamoja.

Hapa kuna mawili. Ni lazima tuamue ligi ichezwe bila mashabiki kama Ulaya, au kama tumeamua kama tulivyoamua, basi taratibu ziwe hizo nilizoziainisha na watu kunawa na kuvaa barakoa, lakini wakishaingia uwanjani na kukaa majukwaani, unaweza kuwadhibiti tu pale kabla mechi haijaanza, lakini ikianza wanakuwa si wale tena. Inakuwa ni ngumu sana kuwadhibiti wasikaribiane.