Ni nzuri Kibiti kufanyisha kazi wanaokiuka ya corona

21May 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni nzuri Kibiti kufanyisha kazi wanaokiuka ya corona

KATIKA kujikinga na maambukizo ya ugonjwa wa corona, utekelezaji katika kuipiga vita, kuna hatua za kujikinga. Jamii zimetakiwa kuzifuata, ili kuukwepa ugonjwa huo.

Muhimu na kinachohimizwa ni kuchukuliwa hatua mapema, kwamba ni jambo jema linalomsaidia mtu asiangukie katika tatizo.

Wataalamu kutoka sekta ya afya, wakiwamo viongozi wa ngazi za juu, pia wasanii, wamekuwa wakitoa elimu ya jinsi ya kujilinda kwa maambukizo hayo ya corona.

Mtu anatakiwa ajilinde dhidi ya maradhi hayo na kisha awalinde wengine.

Katika kujilinda mtu asipate, inaelezwa haja ya kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kuosha mikono kwa maji tiririka na kuvaa barakoa mara zote, ikiwamo kutumia vitakasa mikono.

Ni elimu inayotolewa kupitia kazi za wasanii na kauli za viongozi, kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Hiyo yote imo katika kuisaidia jamii isipate maambukizi ya ugonjwa huo.

Inaelezwa, ukweli ni kwamba iwapo jamii itazingatia elimu hiyo, haki hiyo itasaidia watu kutopata maambukizo ya ugonjwa huo.

Kama jamii haitatilia maanani maagizo yanayotolewa jinsi ya kujilinda na maambukizo ya corona hali hiyo itafanya watu kupata maambukizo.

Katika kupambana na maambukizo ya virusi vya ugonjwa wa corona, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, imetangaza hatua zitakazochukuliwa dhidi ya watu watakaokamatwa wakiwa wamekaa makundi vijiweni.

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gulam Musini Kifu, katika kikao cha Baraza la Madiwani kutokana na kuwapo ugonjwa wa corona, hivyo kila mtu anatakiwa kuchukua hatua.

Anasema, baadhi ya watu bado hukaa vijiweni, wanaendeleza mikusanyiko ambayo imekatazwa na serikali na kwa sababu za usalama kiafya, jambo ambalo si zuri.

"Kutokana na watu kutosikia makatazo ambayo serikali inatutangazia kila siku katika kujikinga na corona, sasa Kibiti nimeishamwambia OCD (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) wakiwakuta vijana vijiweni wawakamate, wawapeleke sokoni, ofisi ya mkurugenzi, kituo cha polisi na hospitali wakafanye usafi, ikifika jioni wawaachie waende makwao," anasema.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya, jambo la kuwafanyisha kazi za usafi wanaokaa vijiweni, itasaidia kupunguza mikusanyiko isiyo na faida.

Pia, anawataka madiwani pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kuwa wanatakiwa kuwahamasisha wananchi uvaaji wa barakoa.

"Mnapoenda kuhamasisha wananchi uvaaji wa barakoa, hakikisheni na nyie mnaenda mkiwa mmevaa,” anasema.