Ni ushindi kupindua usugu wa kifua kikuu kwa mapana

27Nov 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni ushindi kupindua usugu wa kifua kikuu kwa mapana

UGONJWA wa kifua kikuu umekuwa ukisababisha watu kupoteza maisha, hasa pale wanapochelewa kupata matibabu kwa wakati katika vituo vya afya.

Hivyo jamii imekuwa ikishauriwa kufika kwenye vituo vya afya kuchunguza afya zao na kama watabainika wana tatizo la kiafya, ni rahisi kwao kupatiwa matibabu, hata wakapona.

Mtu anapojulikana mapema ana tatizo fulani, ambalo linamsumbua, ni rahisi kufanikiwa kupata matibabu na kufikia hatua ya kupona anarejea maisha ya kawaida kabisa.

Hivyo, serikali imekuwa ikihamasisha jamii kujenga utamaduni wa kucheki afya zao. Lengo ni kuwasaidia wenye matatizo matibabu ya haraka na wakati.

Katika kuhakikisha inapambana na afya za wananchi kwa kuziweka sawa, serikali nchini kupitia mamlaka zake zinazosimamia afya imeazimia kutokomeza kifua kikuu kwa kuongeza ugunduzi wa wagonjwa wapya wa kifua kikuu na kuwaweka kwenye matibabu.

Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi, alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika jijini Dodoma.

“Uwezo wa nchi kugundua wagonjwa wapya na kuwaweka kwenye matibabu umeongezeka kutoka wagonjwa 62,908 (asilimia 33 mwaka 2015 na kwa sasa kufikia wagonjwa 82,166 (asilimia 59),” anasema Prof. Makubi.

Ni kutokana na hali hiyo, Prof. Makubi anasema kuna maisha ya wananchi takribani 300,000 wakiwamo watoto 45,000 wameponywa kwa kupatiwa dawa kwa wakati na kufuatiliwa kwa usahihi, kati ya mwaka 2015 na sasa.

Juhudi hizo pia zimeweza kupunguza idadi ya vifo vinavyosababishwa na kifua kikuu kwa asilimia hizo 33, kama Profesa Makubi anavyofafanua: “Mwaka 2015 kulikuwa na vifo 30,000 hivi sasa vimepungua hadi kufikia vifo 20,000.”

Mganga Mkuu anafafanua kwamba, kuna mafanikio katika hatua hiyo ya ongezeko la kasi ya ugunduzi wa wagonjwa wapya na mikakati mbalimbali iliyowekwa na wizara kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma.

Hapo kunatajwa kuwapo, maboresho ya huduma za ugunduzi wa ugonjwa wa TB na kutoa kipaumbele kwa makundi yaliyoathirika zaidi kama vile kaya zenye wagonjwa, wanaoishi kwenye kaya maskini, magerezani, wachimbaji wadogo na waathirika dawa za kulevya.

“Aidha tumewekeza katika ubunifu mbalimbali wa matumizi ya teknolojia mpya za ‘molekyula’ za kubaini TB kwa usahihi na kwa haraka” anasisitiza Prof. Makubi.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dk. Leonard Subi, ana jicho lake linalovutia kuhusu kifua kikuu kwamba, imefanya vizuri kufikia malengo waliyoyaweka unaomalizika mwaka huu.

“Malengo ambayo tulijiwekea ya kupunguza vifo vitokanavyo na kifua kikuu tumeweza kuyafikia, pamoja na kupunguza madhara yanayotokana na ugonjwa huo,” anajigamba Dk. Subi.

Anasema serikali imewza kuongeza vituo vya upimaji wa kifua kikuu sugu kutoka kituo kimoja mwaka 2015 hadi 145, hivyo kuongeza wigo wa huduma za matibabu ya ugonjwa huo.

Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa, Dk. Ntuli Kapologwe, anasema ofisi yake kwa kushirikiana wizara inayohusika na afya, katika kipindi cha miaka ijayo imejiwekea mikakati kadhaa.

Hiyo inajumuisha kuwawezesha watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya, ili wawe na ujuzi na uwezo wa kutambua na kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua kikuu.