Ni vyema walimu wakajifunza kukabili majanga moto shuleni

30Jul 2021
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni vyema walimu wakajifunza kukabili majanga moto shuleni

MAJANGA ya moto yanapotokea katika shule za bweni, yanatakiwa kushughulikiwa mapema, ili usilete madhara na kuharibu mali.

Katika kupambana na majanga hayo, elimu inatakiwa itolewe kwa walimu ili waweze kukabiliana nayo pindi yanapotokea.

Elimu inapokuwapo, ni rahisi watu kujua jinsi ya kupambana na matukio hayo ya moto.

Kutokana na baadhi yetu kutokuwa na elimu ya masuala ya moto, inachangia hata moto unapotokea, wanakosa uwezo wa kuuzima.

Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Hadija Nasri, aliwataka wakuu wa shule za bweni zilizopo ndani ya wilaya yake, kuchukua tahadhari ya namna ya kukabiliana na majanga ya moto yanayoweza kutokea shuleni. 

Akizungumza katika kikao alichoitisha na  kujumuisha wakuu wa shule za bweni na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, mkuu huyo aliwasisitiza wakuu wa shule kuwa na dhamana na uwajibikaji wa kuzima moto katika viunga vyote vinavyozunguka shule, zikiwamo mabweni na mabwalo la chakula.

Ofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkuranga Inspekta Msaidizi, Fransisco Chunji, anawaomba walimu kuwashirikisha katika ujenzi wa mabweni na majengo ya shule.

Chunji anasema, inakuwa na msaada kuwashauri kuweka mifumo bora ya kung’amua moshi kabla madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na kutokea moto.

Mtazamo wake kitaalamu ni kwamba walimu hao kwa kushirikiana na kamati za shule, wanapaswa kujenga utaratibu wa kuzungumza na wanafunzi kila mara, kwa lengo la kupata taarifa za watoto wanaoweza kuwa chanzo cha majanga.

Anasema hiyo inatokana na utovu wa nidhamu au kutokuridhishwa na huduma zinazotolewa shuleni na hivyo kufanya hujuma kati ya wanafunzi wenyewe au wanafunzi na walimu, pia dhidi ya wananchi kutoka nje ya shule. 

Askari huyo anawataka walimu kuchukua tahadhari ikiwamo ukaguzi wa majengo, ambayo yamekaa muda mrefu yanayoonyesha hali ya uchakavu, yafanyiwe  ukarabati wa kuta penye nyufa na mifumo ya umeme.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde, aliyewakilishwa na Ofisa Elimu Wilaya, Benjamini Majoya, anawataka walimu kufanya mabaraza walau mara moja kwa muhula, ili kuwaruhusu wanafunzi kusema wanachokitaka katika madarasa na mabweni yao.

Anasema ni hatua itakayosaidia kupata picha ya changamoto na shida zinazowagusa na kupitia hayo, inawapatia taarifa za yanayowasibu, mfano hai kuwapo mwalimu anayechapa sana wanafunzi.

Ana msisitizo kwamba, dhana ya kutokujua jambo pekee, inaweza kusababisha wanafunzi kuchukia na kutafuta upenyo wa kuwasilisha hisia zao kwa kufanya uharibifu wa miundombinu, kwa kutumia njia za kuchoma moto au kuvunja vifaa vya kusomea

Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Ally Mbikilwa, anatoa ufafanuzi kwenye tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO19, akiwataka walimu kuchukua hatua kama miongozo na maelekezo ya afya yanavyotolewa na serikali, ili kuikinga jamii ya shule kwa ujumla.