Ni wakati muafaka madalali, vyama vya msingi kujitafakari

24May 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni wakati muafaka madalali, vyama vya msingi kujitafakari

WIKI hii tumeona na kusikia kupitia vyombo vya habari, vikinena mengi, kuhusu kuongezeka bajeti katika Wizara ya Kilimo.

 Ongezeko hilo ni kutoka Sh. bilioni 170.2 hadi Sh. bilioni 253.85, ni neema kubwa katika sekta hiyo  ya kilimo.

 

Hapana shaka, ni kiashiria kwamba sekta hiyo inafanya vizuri na iko katika sehemu ya wachangiaji mafanikio ya kuongezeka pato la taifa, huku ikimuwezesha mkulima kunufaika kimapato kupitia sekta yake.

 

Inakuwa jambo jema lenye kutoa kila sababu ya  wakulima kunufaika na kile walichokilima, ili kiwaletee maendeleo.

 

Nianze kwa kuzungumzia uhalisia kwamba, hivi sasa mazao mengi yanapaswa kupelekwa sokoni kuuzwa na kumnufaisha moja kwa moja, tumekuwa tukimuona mkulima, ili aweze kuuza bidhaa zake, lazima dalali au vyama vya msingi kusimamia soko, ili mkulima afanye biashara.

 

Hata hivyo, kuna baadhi ya madalali na vyama vya ushirika, wamekuwa sio waaminifu na kusababisha wakulima kutonufaika na kupitia mazao ya wakulima hao.

 

Katika siku za karibuni katika semina ya Jinsia na Maendeleo zinazoandaliwa na asasi ya TGNP Mtandao. Baadhi ya washiriki walikuwa wakijadili mada inayozungumzia Bajeti katika Wizara ya Kilimo.

 

Katika semina hiyo, baadhi ya washiriki walichangia mada inayohusu Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya Mwaka 2018/2019 na mwaka 2019/2020.

 

Mjadala huo wa bajeti, uliibua mawazo tofauti ya washiriki, kutokana na kubaini fedha zinazotengwa katika Wizara ya kilimo. Baadhi ya washiriki walitoa maoni yao kupitia bajeti zinazotengwa.

 

Juliana Juma, anasema serikali inajitahidi kutoa pembejeo kwa wakulima, lengo ni kuwawezesha wakulima kupata mazao mengi, ili yawe mkombozi katika kuwainulia kipato.

 

Pamoja na serikali kutoa pembejeo wakulima kupata mazao mengi, changamoto inakuja katika upatikanaji masoko ya kuuza mazao hayo. Madalali wamekuwa wakiwatafuta wateja na kunufaika wao badala ya wakulima.

 

Mtoa maoni, Juma Amanzi, anasema madalali wanagawanyika katika makundi; waaminifu na wasio waaminifu. Pia, wapo wanaosimamia biashara za wakulima na wananufaika nazo, kwa namna wanazozijua.

 

Vivyo hivyo, kuna wanaojinufaisha kupitia mazao hayo ya wakulima, katika nyedo hizo za kidalali.

 

Ashura Juma, ana maoni kuwa, umefika wakati sasa wa wakulima kupewa elimu ya masoko, ili iwe mkombozi kwao kimapato.

 

Katika maoni yake, Ashura anasema kuwapo baadhi ya wakulima wanaolima matunda, lakini hawana masoko na kufanya matunda kuharibika kunayauiza. Kwani, iwapo wangekuwa na elimu ya usindikaji bidhaa hizo, zingeweza kuhifadhiwa kwa kipindi kirefu na kudumisha maufaa yake.

 

Hioyo ni sehemu ya hoja zilizoibuliwa na washiriki, katika semina, ombi ni kakapo sheria zitakazochukuliwa dhidi ya madalali, watakaoonekana kuhujumu mazao ya wakulima.

 

Mwingine mwenye maoni, Abdallah Hemed, anasema kuna vijiji ambavyo havina huduma za kibenki, lakini wakulima wake wanalima.

 

Hao ni kwamba, wanapopata matatizo, madalali hutumia matatizo hayo kuwapatia pesa kidogo, huku wakichukua mazao mengi kutoka kwa watu hao.

 

Nasema, kama mahali hapo kungekuwapo huduma za kibenki, wakulima wetu wangekuwa wanakopesheka. Lakini ndiyo hivyo, kutokuwapo huduma hizo, wanajikuta wakulima wakinyanyasika, huku mazao ni yao.

 

Huko vijijini, kinamama wanahangaika kulima, lakini wengi katika kundi hilo hawanufaiki na kilimo hicho. Kisa ni kwamba, wanahujumuwa kwa mazao yao kuanzia shambani hadi sokoni.

 

Niseme kinachotakiwa katika kuwanusuru kinamama wanufaike na kilimo chao, ni kwamba wawakilishi wao wawatafutie masoko ya uhakika, ikiwamo kuwachukulia hatua madali na vyama vya ushirika vyenye hujuma kwa mazao yao.