Ni wakati sasa kilimo kiwe na asilimia 10 ya bajeti

15Oct 2019
Raphael Kibiriti
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni wakati sasa kilimo kiwe na asilimia 10 ya bajeti

WAKULIMA hasa wadogo nchini ni moja ya kundi linaloonekana kuwa na watetezi wengi.

Si watu binafsi, taasisi au mashirika tu, lakini majukwaa mbalimbali, kama vile Jukwaa la Asasi za Kilimo (ANSAF) na Shirika la Mapinduzi ya Kijani kwa nchi za Afrika (AGRA).

Haya yote yanalenga kuwasemea, kuwatetea na kuwapigania wakulima kutoka pande zote ili maisha yao yastawi kutokana na kazi hiyo muhimu wanayoifanya kwa maslahi ya taifa.

Lakini ukiachana na mashirika hayo yenye lengo la kuwa na sera, sheria na kanuni zinazomnufaisha mkulima, pia kuna kundi la wanasiasa.

Kundi ambalo linawajumuisha madiwani, wabunge, mawaziri na watendaji wengine wa serikali kama vile makatibu tarafa, wakuu wa wilaya na wa mikoa, bila kusahau viongozi wa kitaifa kwa maana ya rais na wasaidizi wake wakuu.

Kundi hili nalo limo miongoni mwa makundi yanayoonekana ‘kuwapigania’ wakulima.

Lakini pengine swali ni kwa nini wanafanya hivyo?

Kwa mashirika na asasi mbalimbali, wanafanya hivyo katika kutimiza malengo yao ya kuona wakulima wanastawi kimaisha.

Lakini kwa upande wa wanasiasa, Muungwana anaona wana sababu mbalimbali, lakini kubwa zaidi ni ile ya kutimiza malengo yao ya kisiasa vilevile.

Hii ni kwa sababu kilimo kinabaki kuwa sekta muhimu katika kuchagiza uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla wake.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, kilimo kinatoa ajira kwa takribani asilimia 75 ya Watanzania, huku kikichangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachozalishwa nchini.

Hivyo, hatua ya wanasiasa kuwatetea wakulima inaweza ikawa ni katika kukidhi malengo ya kisiasa, kwa msingi kuwa ndiyo sekta iliyoajiri sehemu kubwa ya Watanzania.

Kwamba asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima, wengi wao wakiwa wadogo wadogo, ni mtaji mkubwa kwa wanasiasa.

Ni kundi kubwa la wapigakura ambalo linaweza likamweka na kumtoa madarakani mwanasiasa yeyote yule na ndiyo maana haiwi ajabu kuona karibu kila mwanasiasa anajaribu kulionyesha kuwa bado analipigania.

Ni katika muktadha huo ndipo Muungwana anapoibuka kulonga, sana sana akielekeza mtazamo wake kwa wanasiasa hawa hawa ambao wawapo majukwaani ama kwenye kumbi zao za udiwani ama bungeni, hujipambanua kuwa watetezi wa kundi hili.

Tena wakati mwingine wakionyesha kuwa na hasira pale inapoonekana wakulima ‘wao’ wanapuuzwa.

Sasa Muungwana anawauliza wanasiasa hawa kuwa, kama wako tayari hata kukamata shilingi ya Waziri wawapo bungeni, ama kupiga kura ya kufukuza watendaji wa halmashauri za wilaya, miji, manispaa ama za jiji, iweje hadi leo hii, bado bajeti inayotengwa kwa ajili ya kilimo si kwa kiwango cha kuridhisha?

Tena wakati wao wakiwa ndio wahusika wa bajeti ya serikali?

Ikumbukwe kuwa Umoja wa Afrika kupitia NEPAD, waliasisi Programu ya Kuendeleza Kilimo mwaka 2003 (CAADP), kwenye mkutano uliofanyika jijini Maputo nchini Msumbiji.

Katika mkutano huo, viongozi hao walikubaliana kutenga asilimia 10 ya bajeti za nchi zao kwenye sekta ya kilimo na maendeleo vijijini.

Muungwana alitegemea basi wanasiasa waonyeshe kweli kuwa ni watetezi wa kundi hili kubwa la Watanzania, kwa kupigania bajeti ya kilimo ifikie hiyo asilimia 10 iliyokubaliwa kwa ajili ya kilimo.

Hivyo ni rai ya Muungwana kwa wanasiasa na watendaji wengine wa serikali kuwapigania wakulima na hasa wadogo wadogo kidhati, kwa kuhakikisha bajeti ya kilimo inakuwa ni asilimia 10 ya bajeti yote ya serikali.

Hilo likifanyika, wakulima wataondokana na mazonge yanayowakwamisha, kama yale ya tija ndogo katika uzalishaji, utegemezi wa mvua, huduma za ughani zisizoridhisha, miundombinu hafifu, ukosefu wa viwanda vya kusindika mazao, uzalishaji na teknolojia hafifu ya kilimo.

Hilo likifanyika wakulima hawatahangaikia masoko ya mazao yao kama ilivyo kadhia inayoendelea ya baadhi ya wakulima wa pamba kutolipwa fedha zao hadi sasa.