Ni wakati wa kuundwa Baraza la Taifa la Vijana

15Apr 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni wakati wa kuundwa Baraza la Taifa la Vijana

VIJANA ni nguvu kazi la kila Taifa duniani. Hiyo inatokana na uwekezaji uliowekwa kati ka jamii ya vijana na kuwapo mazingira rafiki na inayojiwezesha.

Nchini Tanzania, vijana wanaelezwa kuunda asilimia 60 ya raia wake ambao ni wastani wa milioni 45, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.

Mazingira rafiki kwa vijana ni wajibu wa serikali na mamlaka zingine husika kuwaanda vijana hao, kuanzia wenye umri mdogo wakiwa katika shule za Chekechea, Msingi, Sekondari hadi vyuoni, ili wapate elimu bora.

Pengine hilo linaweza likaanza tangu ngazi ya elimu ya awali, kwa kuwajenga watoto tangu shule ya msingi, wakafahamu namna ya kujitegemea kupitia kuajiriwa na kujiajiri.

Elimu ya kumuandaa kijana kujitegemea, inaanzia shuleni na ndio maana, kuna mifumo mbalimbali ya elimu.

Hiyo inajumuisha mafunzo ya shuleni ambayo inapatikama kwa namna mbalimbali, kwa mfano shule za kutwa na bweni.

Walioko shuleni, wana fursa zaidi na kupata muda ambao wanatengewa au kufundishwa namna ya kujisimamia kimaisha na kutambua wajibu wao wa baadaye.

Kuwepo masomo tofauti kama vile Hisabati, Jiografia, Sayansi na Uraia zinatumika kumuandaa kijana kuhusu mbinu za kujikimu kimaisha masomoni na katika maisha.

Mathalan, vijana wanaojikita katika masuala ya mahesabu au sanaa tangu wakiwa masomoni, wanaandaliwa kumudu mengi kama vile biashara na ubunifu kwenye uigizaji, uchoraji, uimbaji na mengineyo yanayofanana nayo.

Pia kuna maeneo kama vile upatikanaji mitaji, mazingira rafiki yanayotegemea zaidi fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na kutoa mafunzo ya ujasiriamali na kuwapo mtaji.

Mazingira na miundombinu ya kufanikisha shughuli mbalimbali pamoja na kutolewa kwa mafunzo ya ujasiriamali ni changamoto.

Masharti magumu tunafahamu yapo katika taasisi nyingi za kifedha nchini, kwamba kabla ya kukopa fedha, ni lazima kuwapo dhamana ya kuulinda mkopo ambao unarejeshwa kwa riba maalumu inayowekwa.

Vijana wengi waliohitimu elimu ya ngazi ya elimu ya ufundi, kupitia katika taasisi zinazotambuliwa na serikal ni wengi sana na kila mwaka wanakadiriwa kufikia milioni moja, lakini wanaobahatika kupata ajira no 200,000 pekee, ambao ni sawa na asilimia 20 ya kundi hilo.

Katika kundi hilo, wapo wenye dhamira ya kuanzisha shughuli ya kuendesha shughuli zao binafsi, lakini changamoto inayowakabili ni mtaji mdogo.

Kuwapo Baraza la Taifa la Vijana linaloweza kukutana angalau mara tatu au mbili kwa mwaka, itasaidia kupangwa mikakati, ratiba na namna ya kutatua changamoto zao.

Vijana hao kutoka maeneo tofauti nchini, wanaweza kuwachagua wawakilishi katika kila mkoa na wilaya, wakaendesha mijadala ambayo itaibua muafaka wa hoja hiyo muhimu.

Kundi hilo litakapokutana na kutambuliwa kisheria, litakuwa na dhamana kubwa ya kutoa mchango mkubwa na kutetea maslahi ya vijana, hasa wanapopata fursa ya kutembelea bungeni kukutana na wadau mbalimbali wenye dhamana na ushawishi.

Wizara yenye dhamana na maisha ya vijana, inapaswa kusimamia kuanzishwa baraza hilo, ili changamoto za vijana zianze kutatuliwa, ikizingatiwa tayari serikali ilishasema inatenga fedha Sh. Milioni 50 kwa ajili ya kila kijiji nchini.