Ni zama za kupunguza makazi kwenye maeneo hatarishi

22Oct 2017
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Ni zama za kupunguza makazi kwenye maeneo hatarishi

OKTOBA 13 ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa. Maadhimisho haya ni utekelezaji wa Azimio Na. 64/200 lililopitishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa Desemba 21, 2009.

Siku hii imechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kukuza utamaduni wa kupunguza maafa kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuzuia maafa, kujitayarisha kuyakabili na kupunguza madhara ya maafa yanapotokea.

Kwa miaka 25 iliyopita, Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Maafa imekuwa ni tukio kubwa la kujenga ufahamu kimataifa katika kutambua maendeleo yaliyofikiwa na kuhimiza jitihada zaidi za kujenga uthabiti dhidi ya majanga kwa jamii na taifa.

Katika kuadhimisha siku hii, Sekretarieti ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa ya Umoja wa Mataifa (United Nation Strategy for Disaster Reduction - UNISDR) hutoa kaulimbiu ya mwaka husika. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema:
“Makazi Salama: Punguza makazi katika maeneo hatarishi, punguza kuhama kutokana na Maafa”.

Siku hii ni fursa ya kutambua maendeleo yanayofanywa ili kupunguza madhara na hasara katika maisha, mfumo wa maisha na afya, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na rasilimali za mazingira ya watu, biashara, jamii na nchi.

Matokeo hayo ni lengo la Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Madhara ya Maafa uliopitishwa katika Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa juu ya Kupunguza Madhara ya Maafa nchini Japani mwezi Machi 2015.

Mfumo wa Sendai una malengo ya kimkakati ya kuhamasisha kazi muhimu ambayo inahitaji kufanyika na umeanzisha njia ya mwelekeo wa utekelezaji kamili.

Mwaka jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alifanya uzinduzi wa "Kampeni ya Malengo Saba ya Sendai" iliyojikita katika kuhamasisha utekelezaji wa malengo saba ya Mkakati wa Sendai katika kipindi cha miaka saba.

Lengo la mwaka huu linazingatia kuzuia, kulinda na kupunguza idadi ya watu wanaoathirika na majanga, ambalo ni lengo la pili (b). Lengo hili linahusu usalama wa watu wote, lakini hasa wale walio katika hatari zaidi ya kifo, kuumia, kuathirika kiafya, madhara ya mfumo wa maisha, kuhama makazi yao na ukosefu wa upatikanaji wa huduma za msingi kutokana na matukio ya maafa hasa kwa wanawake, watoto, watu wenye ulemavu na wazee.

Makundi haya ni muhimu kwa kuwa yana viwango tofauti vya uwezekano wa kuathirika na matukio ya maafa na hivyo yanahitaji kuzingatiwa kipekee katika mipango ya usimamizi wa madhara ya maafa.

Siku hii ya Kimataifa inamaanisha haya yote, lakini inazingatia kwanza umuhimu wa nyumba ya familia kama mahali rasmi na salama wakati wa maafa kwa lengo maalumu la kuzuia kuhama makazi. Nyumba ya familia mara nyingi ndipo mahali pa kazi kwa jamii za kipato cha chini. Kampeni pia itajumuisha viashiria vingine muhimu kwa lengo (b) ambavyo ni kujikinga dhidi ya kuumia, madhara ya kiafya na kupoteza mifumo ya maisha.

Kaulimbiu ya mwaka huu, imekuja kwa kuwa ni mwaka ambao watu milioni 24.2 walihama makazi yao kutokana na maafa duniani.

Siyo kila janga la asili husababisha madhara makubwa, bali pia mchanganyiko wa mambo ya mifumo ya asili, shughuli za maendeleo, kiutamaduni, kijamii na kisiasa huchangia maafa. Maafa yanayotokana na matukio yanayohusiana na hali ya hewa (mafuriko, dhoruba na vimbunga), yamechangia idadi kubwa ya vifo vya maafa kwa miaka mingi na kumekuwa na muendelezo wa kuongezeka.

Maafa ni miongoni mwa vyanzo vya umaskini na dhiki kwa watu wengi walio katika mazingira magumu hasa wanaoishi katika nchi zinazoendelea.

Kupunguza madhara yanayotokana na kuongezeka watu kuhamia mjini kwa kasi, umasikini, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kutapatikana kwa kuzuia kutokea au kuongezeka kwa matukio hayo.

Kampeni ya mwaka 2017 inahimiza kuongeza ufahamu kuhusu hatua za kuchukua ili kuboresha makazi, sera na utekelezaji wa masuala yanayoweza kupunguza uwezekano wa jamii kuathirika na hivyo kuchangia kuokoa uharibifu wa makazi na shughuli za kiuchumi kutokana na maafa.

Ni dhahiri kwamba kuchukua hatua katika suala hili kutaonyesha mafanikio endapo kutachangia matokeo chanya katika kuokoa maisha, kupunguza hasara za kiuchumi na kupunguza uharibifu kwa miundombinu muhimu ya huduma za jamii.

Pia kutaonyesha ushahidi wa kuwapo mikakati katika ngazi ya taifa na serikali za mitaa inayolenga usimamizi wa maafa hapa nchini.

[email protected]; Simu: 0744 466 571