Ni zamu ya wapigakura kuwachuja wagombea

24Jun 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ni zamu ya wapigakura kuwachuja wagombea

BAADHI ya wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wameshatangaza nia ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya vyama hivyo kuwataka wanachama wake wenye nia ya kutaka uongozi, kujitokeza ili kupimwa kama wanatosha kuviwakilisha kwenye uchaguzi huo.

Pamoja na milango ya baadhi ya vyama kufunguliwa, siyo vibaya wapigakura kujipa nafasi ya kuwachunguza na kuwapima watiania hao kama wanatosha, kwa lengo la kupata viongozi bora wa kuwaongoza.

Iwapo hawatafanya mchakato huo ‘wasiotosha’ hivyo kubaki kulalamika.

Ikumbukwe kwamba kila unapofanyika uchaguzi, watu wengi wanajitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, wakiwamo hata wale wasio na sifa ili mradi tu wapae uongozi.

Hivyo suala la kuwachunguza ni la muhimu kama ambavyo, Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA) inavyosisitiza, lengo likiwa ni kupata viongozi bora na siyo bora viongozi.

Binafsi ninaunga mkono ushauri huo wa CEGODETA, ambao unalenga kusaidia Tanzania kupata viongozi wanaofaa na wanaowatumikia wananchi.

Ni kweli, wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa na wasio na vyama, wanawajua watu ambao wanafaa kuwaongoza na wakati mwingine ni wale wanaoishi nao, hivyo njia nzuri ni kuanza kuwachunguza.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Thomas Ngawaiya, inatamani wapigakura wasijigawe kwa itikadi za vyama vya siasa na badala yake kumpendekeza yule wanayeamini anaweza kuwaongoza.

Jambo la kuzingatia liwe kutambua umuhimu wa watu wanaofaa kuongoza bila kujali mambo ya vyama, kwa vile maendeleo hayana chama ili mradi wanayemtaka ana uwezo wa kuongoza.

Anatambua kuwa ni lazima watia nia wapitie kwenye mchakato wa kura za maoni, katika vyama vyao, lakini wapigakura wana nafasi ya kuchunguza na kushawishi au kushauri ili kupata mgombea sahihi.

Kimsingi, ushauri huu ukizingatiwa, unaweza kusaidia kuleta maendeleo kwenye ngazi mbalimbali ikiwamo kata na majimbo, lakini ni vyema kuwe na angalizo katika jambo hili.

Angalizo ni kwamba ni muhimu kuzingatia jinsia kwenye uongozi, kwani katika jamii, bado kuna watu ambao wanawatenga wanawake wakiamini kuwa hawana uwezo wa kuongoza.

Dhana hiyo imeshapitwa na wakati, ni vyema sasa jamii ikabadilika na kutambua kuwa wanawake nao wana uwezo wa kuongoza kama walivyo wanaume, na inawezekana wapo wanaowazidi wanaume.

Kwa maana hiyo, mtiania awe mwanamke au mwanaume, wote wana haki ya kuchaguliwa na kuchagua, ili mradi wapigakura wamemchunguza na kuona mmoja wao anafaa, basi awe chaguo lao.

Suala la ubaguzi wa kijinsia lisipewe nafasi, kwa sababu linasababisha watu wenye sifa za kuongoza kukosa nafasi kutokana na jamii kuendekeza mila na desturi ambazo zimepitwa na wakati.

Uongozi ni wito, hivyo mtu akiwa kiongozi ni lazima ajijengee mazingira mazuri ya kuwa mfano wa kuigwa na watu wengine ili hata anapohitaji kuchaguliwa kwa mara nyingine, iwe rahisi kupata kura.

Ninaamini kwamba kwenye jamii, watu hao wapo wakiwamo wanaume na wanawake, na pia wapo pia wale, ambao hawajawahi kuongoza, lakini wameonyesha kuwa wakipewa nafasi wanaweza kuongoza.

Watu wa aina hii kama anavyosema Ngawaiya, wasiachwe, bali wapigakura wawafikirie pia, hivyo ikiwa imebaki miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu, ni vyema wapigakura nao wakajiwekea mbinu za kupata watu wanaofaa.

Wakati huu ambao michakato mbalimbali ikiendelea kufanyika kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo, wapigakura nao hawana budi kuwa na mchakato wao wa kimya kimya.

Uandikishaji wa watu, katika daftari la kudumu la wapigakura, utoaji wa elimu ya mpigakura ni miongoni mwa mambo ya muhimu katika uchaguzi huo, lakini wapigakura nao wawe wabunifu katika hili.

Kwa mujibu wa Ngawaiya katika siasa kuna mambo mengi yanafanyika ikiwamo watu wasio na sifa za kuongoza lakini nao hujitokeza kuwania uongozi.