Nidhamu ya bodaboda ikichekewa, tutalia sana

14Feb 2020
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Nidhamu ya bodaboda ikichekewa, tutalia sana

UKIPITA katika barabara zinazotumiwa na mabasi ya mwendokasi, utaona kila penye kivuko, kuna tangazo ambalo haziruhusu bodaboda kupita wakiwa wamebeba abiria.

Pamoja na kuandikwa kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza, bado madereva wa bodaboda wanapita wakiwa wamebeba abiria.

Hapo katika mustakabali wa usalama barabarani, inazua maswali nini sasa kifanyike? Iko wazi kinachotakiwa hapo ni hatua madhubuti. Zipi? Pale usafiri wa bodaboda unapopita katika maeneo hayo, mara moja kinachotakiwa ni mamlaka za dola kuchukua hatua zinazoleta marekebisho.

Panapaswa kuhakikishwa abiria waliopo wanashushwa, pia dereva wa bodaboda anatakiwa kushuka katika chombo chake, anakisukuma na baada ya hapo anaruhusiwa kupanda chombo kuendelea na safari yake.

Ninashuhudia pamoja na katazo hilo, bado watumiaji vyombo hivyo wanaendeleza tabia. Madereva wa bodaboda wamekuwa wakikiuka taratibu na kuamua kupita katika njia hizo, huku wakiwa wamepanda bodaboda zao. Niseme ni ukiukwaji mkubwa.

Walioamua kuweka utaratibu huo walikuwa na busara kubwa kuhusiana na usalama barabarani. Waliona mazingira ya kiashiria cha ajali inayoweza kuleta maafa kwao na umma kwa jumla, watu wakapata ulemavu wa namna mbalimbali.

Bodaboda mara nyingi zimekuwa zikikiuka sheria za usalama barabarani na kusababisha watu kupoteza maisha au kupoteza viungo.

Hiyo yote inatokana na madereva wa bodaboda kutokuwa makini na kazi wanazozifanya? Madereva haohao wanajua sheria inawataka wabebe abiria mmoja, lakini haohao wako mstari wa mbele kukiuka sheria, wanabeba abiria zaidi ya mmoja.

Pia, dereva wa bodaboda kawaida ya kubeba abiria zaidi ya mmoja na mara nyingi, hata uendeshaji wao si ulio salama hata kidogo. Kuna viashiria vingi.

Tukumbuke, hivi sasa katika barabara kama za jiji la Dar es Salaam, kuna magari ya mwendokasi zinapokutana na zuio la aina yoyote isiyo ya kawaida, ni wazi kuna ishara zaidi na kunapokuwapo zuio lolote, lazima jamii isifanye ukaidi. Ajali inaweza kutokea muda wowote.

Abiria nao mnaopanda bodaboda mkapita katika alama ya ‘zebra’ ni wajibu wenu kidereva mjiandae kushuka ili mkivuka upande wa pili, muendelee na safari zenu.

Pia, abiria kama hiyo sheria ya kushuka katika zebra za mwendokasi unaijua, ni muhimu usiipuuzie hata kidogo, kwa sababu walioweka wana maana kubwa katika usalama.

Tumekuwa tukishuhudia uendeshaji mbaya wa bodaboda unaofanywa na baadhi ya madereva wa vyombo hivyo. Imefika hatua, kwamba madereva hao wanaoendesha kwa kasi bila ya kujali chochote mbele yao na kuzua hatari, ikiwamo na maisha ya abiria wao, wachukue hatua.

Ni hao hao bodaboda wanapoona foleni kubwa, hawajali chochote na wanajichomeka katikati ya magari, bila ya kujali kinachoweza kutokea mahali hapo

Niwakumbushe abiria wezangu, iwapo mtaendelea kuwachekea bodaboda na kuwafumbia macho, mjue chochote kinaweza kuwapata na msilaumu pale mtakapopata ulemavu.