Nini kosa JPM kujenga uwanja wa ndege, mbuga Chato?

14Sep 2020
Nkwazi Mhango
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Nini kosa JPM kujenga uwanja wa ndege, mbuga Chato?

KITENDO cha serikali kujenga uwanja wa ndege mkoani Geita kimewakera baadhi.

Mgombea fulani alisikika akilalamikia kuanzishwa mbuga ya wanyama mkoani Geita kiasi cha kuigeuza sera. Jamani, kama hamna cha kumpinga Rais John Magufuli heri mjinyamazie kuliko kujiaibisha.

Jamaa anasema hii ni aibu na Watanzania si wajinga. Kweli. Watanzania si wajinga. Ulizeni vigezo vilivyotumika kujenga uwanja husika. Je huyu hajui kuwa dhahabu inayopatikana sana Geita ni ya pili kwa kuchangia pato la taifa? Je, hajui kuwa wachimbaji wengi wa dhahabu huko licha ya kampuni kubwa kuliko zote ya GGM wako Geita? Je, hajui kuwa wachimbaji wengi ni matajiri wanaotaka usafiri haraka? Je, kama mkoa wenye kuzalisha dhahabu nyingi; hivi kosa ni kuwa na uwanja wa ndege wa kimataifa?

Chato ni ‘tactical’ kiusalama na ‘alternative’ kwa ndege zinapokuwa na dharura nchini na majirani. Geita ina vivutio vinavyohitaji usafiri wa haraka. Alitaka aanzishe uwanja wa mpira? Umuhimu wa Chato kwa dharura ni sawa na ule wa Anchorage Alaska kwa ndege za kimataifa. Walalamikaji hawajui: Chato-Burigi ni ya tatu kwa ukubwa baada ya Ruaha na Serengeti.

Je, walitaka hii mbuga iendelee kutumika kifisadi kama zilivyokuwa nyingine alizoanzisha hivi karibuni au makazi ya majangili na majambazi? Je, hawajui kuanzisha mbuga, zaidi ya kuongeza mapato kimkoa na nchi, huzalisha ajira mbali na usalama wa wanyama, mazingira na nchi kwa ujumla? Je, kosa la Magufuli ni kuzaliwa kwenye sehemu yenye Wanyama? Mbona wahusika hawalalamikii mbuga nyingine zilizoanzishwa sambamba na mbuga hii wala viwanja vya ndege vilivyojengwa sambamba na hiki kinachomnyima usingizi?

Kwanini wahusika wasifanye japo ‘homework’ kidogo wajiulize: Kwanini Geita inayoingiza mabilioni ya shilingi kiuchumi kitaifa isiwe na uwanja wa ndege, lakini Zanzibar ambayo pato inaloiingiza haliwezi kulingana na Geita iwe na uwanja wa ndege wa kimataifa?

Kwanini hawalalamikii Mbeya kuwa na uwanja wa kimataifa wa ndege wala Mwanza? Hata angepanua uwanja wa ndege wa Mwanza na kuacha kujenga wa Chato bado wangesema anapendelea Kanda ya Ziwa. Haya ndiyo mawazo ya watu wanaoshindwa kufikiri sawa sawa na kuhukumu mambo kama yalivyo baada ya kufanya hivyo kwa kusukumwa na hasira na kutaka umaarufu rahisi na kulipiza kisasi.

Wanaobeza juhudi za Magufuli wanapaswa kuwa na busara japo kidogo.

Niliwahi kusikia profesa mmoja mstaafu aking’aka eti watu wanasifia barabara, madaraja, ndege na reli.

Anataka wasifie umaskini uliofanya kuzidiwa na viinchi visivyo na rasilimali? Profesa huyu alisikika akimnukuu na akitaka kumtumia Marehemu Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere aliyesema kuwa maendeleo lazima yawe ya watu. Ama! Kwani hii miundombinu imejengwa isafirishe wanyama au majini? Hawa wanaopiga kelele watakuwa wa kwanza kuvitumia.

Wahenga wanaasa: Mnyonge mnyongeni: haki yake mpeni. Wapo waliosema kuwa hata makaburu walijenga miundombinu. Ni kweli.

Kwanini hawajiulizi: makaburu walimjengea nani kama siyo weupe tu wakifaidi vitu hivyo kwa jasho la Mswahili? Ajabu hao wanaomzodoa na kumlaani Magufuli kwa kujenga vitu ‘badala ya utu’ ni hao hao waliokuwa wakisafiri toka kwao kupitia Uganda na Kenya kwenda Dar es Salaam. Tumekuwa wepesi wa kusahau hivi kwa malengo ya kisiasa kiasi cha kujigeuza kwa makusudi wezi wa fadhila? Walitaka Magufuli ajenge nini zaidi ya miundombinu ili kufanya mageuzi ya uchumi wa kisasa?

Hao wakienda Ulaya wakapanda vipandwa wanavyolalamikia; wakija huku wanasema kwanini hatuwi kama Ulaya? Tukitaka kuwa kama Ulaya wanayoiabudia, wanaanza nongwa. Hii ni tabia ya kitoto.

Mtoto ukimpa mpira achezee akaupoteza anakulaumu. Ukimnyima ili asiupoteze anakulaumu.

Kimsingi, wanaompinga Magufuli watafute na kujenga hoja zenye mashiko badala ya uzushi na siasa za maji taka. Tuache siasa chafu. Watanzania si wajinga wala wasahaulifu hivyo wala si vipofu na viziwi.

Serikali iko mbioni kujenga hospitali za rufaa mikoani. Kesho utasikia Magufuli kajenga hospitali ya rufaa kwao.

Je, kwao hawaugui; si Watanzania sawa na wengine wanaohitaji huduma hii; kumzaa Magufuli inapoteza haki zinazopewa mikoa mingine? Ni ajabu kusikia wakisema eti Geita hakuna biashara ya kuhitaji ndege.

Mbona Arusha na Kilimanjaro kuna uwanja wa ndege wa kimataifa? Wazidi kutukana kuwa uwanja wa ndege wa Chato hauna kazi bali kutumika kumsafirisha Magufuli na mama yake.

Haya matusi ya nguoni yasiyopaswa kuvumiliwa. Pia si maneno ya kistaarabu. Nadhani tujadili hoja badala ya familia za wagombea kwani, wanafamilia si wagombea. 

Pia wanadai eti Nyerere hakujenga uwanja wa ndege kwao. Angejengaje wakati ule vipaumbele vilikuwa ni siasa za ukombozi Kusini mwa Afrika? Angejengaje wakati hata barabara zenyewe hazikuwa zimejengwa kutokana na jukumu la Tanzania kumpiga nduli Idi Amin? Hakika, hata Nyerere angekuwa hai leo, angemwambia Magufuli akachape kazi kama ambavyo mzee Ali Hassan Mwinyi, Marehemu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete walichagiza; si mara moja wala mbili.

Kumalizia, kuwasaidia wenzetu kufikiri kuwa kinachoendelea, si kwa faida ya Tanzania tu bali hata majirani zetu hasa nchi zisizokuwa na bandari kama vile Rwanda, Uganda, Zambia, Malawi na DRC.

Muhimu, kukubali na kuelewa: ndege zitazidi kununuliwa, barabara na madaraja kujengwa na mbuga mpya za wanyama kuanzishwa kwa faida ya Watanzania watake wasitake.

Binadamu tuna tatizo moja kubwa kimajaaliwa: kusahau tena kwa wengine haraka na kirahisi. Mpeni muda arekebishe Tanzania basi.