Nyosso anapotuonyesha tatizo la mabeki Bongo

22Feb 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Nyosso anapotuonyesha tatizo la mabeki Bongo

MARA baada ya mechi kati ya Simba dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sven Vendenbroeck, alionyesha kushangazwa na uwezo mkubwa wa beki mkongwe nchini, Juma Nyosso.

Alionekana kusuuzika mno na aina yake ya uchezaji na kuona kuwa hivi ndivyo beki anavyotakiwa kucheza baada ya kula sahani moja na John Bocco na kumpa wakati mgumu mno.

Sven, akauliza kama anaweza kumpata beki huyo kwenye kikosi chake cha Simba. Alishangaa aliposikia kuwa beki huyo alishawahi kuichezea Simba miaka kadhaa nyuma.

Kwa nini aliondoka? Hilo ni swali lingine. Kwa hali ilivyo ni kwamba wanachama na mashabiki wa Simba wasishangae kuona Nyosso akirejea tena Msimbazi kwa mara nyingine tena baada ya miaka mingi.

Nyosso alijiunga na Simba mwaka 2008, akitokea Ashanti FC na kukaa kwa miaka mitano, hadi 2013, alipohamia Coastal Union na baada ya hapo kwenda kuichezea Mbeya City, kabla ya kutua Kagera Sugar.

Bado anaonekana kuwa wamo. Pamoja na kwamba ni mchezaji wa muda mrefu, lakini bado ana nguvu, akitimiza majukumu yake yote ambayo beki anatakiwa kuyafanya.

Hata yale matatizo yake ya utovu wa nidhamu anaonekana kuwa amejirekebisha na badala yake amejikita zaidi kucheza soka.

Mwenyewe ametanabaisha kuwa hakuna straika anayemhofia Tanzania kama John Bocco na kudai ni mchezaji mwenye uwezo wa hali ya juu, nguvu, anayeweza kuwaadhibu wakati wowote ule mabeki wanapozubaa.

Tayari baadhi ya wachambuzi wa soka nchini wameshaanza kumpigia chapuo kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kitakachoenda kucheza michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, CHAN.

Itakumbukwa pia kuwa mara baada ya Fainali za Afrika (Afcon), mabeki wakongwe nchini, Kelvin Yondani na Erasto Nyoni walitaka kutangaza kujiuzulu kuichezea timu ya taifa.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwataka wasitishe mpango huo mara moja na kuwaomba waendelee kuichezea timu hiyo, si kwa manufaa yao tu, bali hata kwa taifa zima. Na hii ndiyo imefanya hadi leo wachezaji hao wawe kwenye kikosi cha timu ya taifa.

Makonda naye ni mwanasoka, aliona kabisa kama mabeki hawa wakijiuzulu, basi eneo la ulinzi kwenye kikosi cha Stars litakuwa matatizoni.

Ni kweli kabisa alikuwa sahihi. Kwa muda mrefu sasa nchini Tanzania kuna uhaba, au matatizo makubwa kwa wachezaji wa safu ya ulinzi hasa kwa wachezaji vijana.

Kile kizazi cha mabeki wenye nguvu, ambao pia wanatumia akili kimeanza kuondoka, na waliobaki ndiyo hawa kina Nyosso, Nyoni ,Yondani au Aggrey Morris wanaishia, badala yake sasa huko mbele ya safari tunaweza kuona mabeki wengi wakitoka nje ya nchi.

Mabeki wengi wa kisasa, hawana nguvu, badala yake wanaona kucheza ubabe ndiyo nguvu au rafu nyingi zisizo na maana, lakini pia hawana muendelezo wa uwezo wao, leo wanaweza kucheza vizuri, kesho matatizo, tofauti na mabeki hawa wakongwe niliowataja ambao wameanza kujulikana tangu katikati ya miaka ya 2000, hadi leo wapo dimbani.

Beki pekee kijana ambaye Tanzania inajivunia kwa sasa anayefuata nyayo za kaka zake hao, ni Bakari Mwamnyeto.

Ni kijana mwenye sifa zote zinazohitajika kuwa beki bora, akicheza kwa kiwango kikubwa akiwa na Coastal Union kwenye mechi zote, lakini hata timu ya taifa pia, amekuwa na kiwango kile kile kama cha kwenye timu yake.

Waliobaki ni wa kawaida tu, wengine wakiwa na viwango vya kupanda na kushuka na homa za vipindi.

Unapoona hadi kocha mgeni wa Simba, pamoja na timu yake kucheza mechi kadhaa za Ligi Kuu na FA, lakini akakunwa na beki mmoja tu, Nyosso ambaye ni mkongwe, huku pia mashabiki wa soka akiwamo Mkuu wa Mkoa, Makonda kuwataka Nyoni na Yondani waendelee kuichezea timu ya taifa, ujue kuna matatizo kwa mabeki wa kizazi cha sasa nchini.

Nilitegemea kwa sasa kuwapo kwa mabeki wengi bora wanaochipukia na kuwafanya kina Nyosso kufikiria kutundika daluga, lakini wapi. Sijui mabeki vijana wanaochipukia wa Kibongo wanakwama wapi?