Okwi sasa asimamie kauli yake Simba

22Jan 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Okwi sasa asimamie kauli yake Simba

HAKUNA ubishi kuwa Emmanuel Okwi raia wa Uganda ni mmoja wa wachezaji muhimu ndani ya kikosi cha Simba.

Lakini pia, mbali ya kuwa mchezaji muhimu, yeye pia ni miongoni mwa wachezaji 'kipenzi' wa mashabiki wa timu hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wake.

Kati ya kundi hilo la wachezaji muhimu na vipenzi kwa mashabiki, wapo pia Shiza Kichuya, Mdhamir Yassin, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Said Ndemla na Jonas Mkude, hiyo ni kutokana na kazi zao uwanjani.

Hata hivyo, linapokuja suala la Okwi, wana Simba wana mapenzi ya kipekee kwa mchezaji huyu ambaye Simba ni kama nyumbani kwake ama kwa wazazi wake.

Pamoja na mazuri yote ya Okwi uwanjani, mchezaji huyu amekuwa na kasoro moja kubwa ambayo kwa Wanasimba inawakwaza, ambayo ni utovu wa nidhamu.

Utovu wa nidhamu ninaousemea hapa sio wa kutukana wachezaji wenzake, makocha au marefa, hapana, ni kitendo sugu cha 'utoro' kwenye timu yake.

Kabla ya kurejea tena kwenye kikosi cha Simba msimu huu, miaka ya nyuma ambayo Okwi alikuwa akiitumikia timu hii, alikuwa na rekodi mbaya ya kuwa mtoro hasa anapopewa ruhusa ya kwenda nyumbani kwao Uganda, aidha kwa matatizo binafsi au hata kwa likizo fupi.

Okwi amekuwa msumbufu kwa suala zima la kurejea kwa wakati kazini kuitumikia timu yake, hivyo kusababisha mgongano ndani ya timu.

Hilo ni jambo ambalo huwakera mashabiki wa Simba, viongozi na hata wachezaji wenzake ambao wanajitoa kwa ajili ya timu bila kujali matatizo yao binafsi.

Wiki hii baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini vimemnukuu Okwi akiweka wazi kuwa kwa sasa atatulia kwenye timu na kuacha mambo yake ya kuondoka na kuchelewa kurudi kikosini.

Okwi amesema kuwa kwa sasa mambo yake kwao Uganda yamekaa sawa na hana sababu ya kuondoka tena, atatulia kwenye timu na kushirikiana na wachezaji wenzake kupambana na kuipa timu mafanikio msimu huu.

Hiyo ni kauli ambayo wana Simba wameifurahia kwa kuona sasa nyota wao huyo ambaye anaongoza kwenye orodha ya wafungaji msimu huu, ataweka akili na mawazo yake kwenye timu.

Binafsi, napenda kumwambia Okwi, asimamie kauli yake, akae akijua Wanasimba wanaumia na matendo yake hayo, na pia wanaimani kubwa naye.

Mashabiki wengi wa timu wanauchu ya kuona wanatwaa ubingwa msimu huu, kitu ambacho wamekuwa wakikisubiriwa kwa muda mrefu, hivyo wanataka kuona kila mchezaji anapambana uwanjani kwa ajili ya timu.