Ongezeko la kodi kwenye taulo tuwasikie wadau

21Jun 2019
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ongezeko la kodi kwenye taulo tuwasikie wadau

BAADA ya kusikika kuwa kodi ya taulo za kike inaongezwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kuna wadau wametoa maoni yao kuhusiana na ongezeko hilo.

Taulo za kike ni mkombozi, pale mwanamke au mtoto wa kike aliyefikia umri wa kuanza kujisitiri, zinamwezesha kutumia na kuwa huru katika hali ya usafi.

Imeshabainika kwamba, kutokuwapo taulo hizo za kike katika baadhi ya shule, watoto wanapojichafua wanapata changamoto na kuamua kurudi nyumbani, mpaka hapo hali yake itakapokuwa salama.

Wapo watoto ambao wanakaa nyumbani hadi siku tano hawahudhurii masomo, kwasababu kubwa ni kutokuwapo uwezo wa kupata taulo hizo.

Taulo zimekuwa zikiuzwa gharama kubwa. Kutokana na ukweli, baadhi ya wazazi hawana uwezo wa kumudu gharama hizo, hawazipati.

Kuna baadhi ya wafadhili wamekuwa wakitoa elimu ya kutumia taulo hizo na kuwapatia watoto taulo, ili waweze kuzitumia kwa ajili ya kuendelea na masomo.

Mbali na wafadhili, pia baadhi ya shule kupitia mafungu yake ya mapato zimekuwa zikitenga fedha kwa ajili ya kununua taulo za kike, lengo ni kumwezesha bintipale anapoharibikiwa, aweze kujisitiri na kuendelea na masomo kama kawaida.

Pamoja na kutengwa pesa hizo, changamoto iliyopo ni uhaba wa taulo hizo. Mtoto anpoharibikiwa, anapewa taulo moja na anaweza kukaa nayo muda mrefu. Kiafya, hiyo haitakiwa mtu kukaa nayo kwa saa nyingi.

Hivi karibuni katika semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambazo hufanyika kila wiki, baadhi ya washiriki waliweza kuzungumzia kurudishwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika taulo za kike.

Washiriki walitoa maoni yao, kuendana na kila mmoja aliyekuwa anavyotathmini kwa maono na mazingira yake.

Mwajuma Ally, ni mama anayesema kuwa taulo hizo ni mkombozi kwa wanawake na watoto waliofikia umri wa kuanza kuzitumia.

Anasema ongezeko hilo, linaweza kuwafaa zaidi wanafunzi na kinamama, mama lishe na wengine ambao wanakaa muda mrefu wakihudumia wateja katika mihangaiko yao ya kila siku, kulingana na shughuli zao.

Anasema kama ongezeko likipitishwa, uwezekano wa kinamama kurudia miaka ya nyuma kujisitiri kwa tabu itarudiwa tena.

Amina Mwinyiheri anasema, serikali iliangalie hilo, kwamba kuna shule ambazo wanapata taulo kupitia wafadhili na hali hiyo imesaidia hata mahudhurio ya watoto katika masomo, kutokana na kupata taulo za kike.

Mama huyo anasema, kuwa bei ikiongezeka wafadhili waliojitolea katika shule nao huenda wanaweza kuacha na hali hiyo ikarudisha nyuma maendeleo ya watoto shuleni, hata afya zao.

Anasema hakuna anayepinga maendeleo, lakini katika suala la taulo, kuna kila sababu ya hitaji la kungaliwa upya.

Pia, Hamis Juma, anasema ongezeko la bei litawanufaisha wazalishaji, lakini litawaumiza watumiaji, huku Zuwena Hamis, akisema kuwa taulo zikiwa za bei kunwa, changamoto itatokea kwa walio na vipato vidogo.

Anasema wapo walio na watoto wenye matatizo ya akili wanapoharibikiwa hawataki kukaa na taulo muda mrefu na kila baada ya muda anataka abadilishwe na kwa siku anaweza kubadilisha hata mara 20.

Faustina John anasema, serikali ifanye jitihada za taulo za zifike vijijini, kutokana na maduka mengi kukosa baadhi na wanakijiji hawajui umuhimu wa taulo na bado wanatumia njia zisizo salama kujisitiri.