Onyo hili lilete matokeo chanya matumizi sahihi ya antibaiotiki

24Nov 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Onyo hili lilete matokeo chanya matumizi sahihi ya antibaiotiki

ANTIBAIOTIKI ni dawa zitajwa kusababisha usugu katika mwili wa mtumiaji na hata wakati zinaweza kumletea madhara makubwa, ikiwamo kupoteza maisha iwapo atatumia bila maelekezo ya madaktari.

 

Kutokana na hali hiyo, serikali imekuwa ikitoa tahadhari mara kwa mara kwa kuitaka jamii kuacha mtindo wa matumizi holela ya antibiotiki, ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Tahadhari hiyo inatolewa kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya watu wamekuwa na kawaida ya kukimbilia katika maduka ya dawa na kununua na kuanza kutumia wanapojisikia vibaya. 

Utaratibu huo unakwenda kinyume, kwa kuwa inaelekezwa kuwa mtu anapojisikia kuumwa, aende kwa wataalamu wa afya apate ushauri utakaomwezesha kupata dawa sahihi za kumtibu.

Lakini bahati mbaya, miongoni mwa dawa ambazo watu wamekuwa wakinunua bila ushauri wa wataalamu wa afya ni antibaiotiki ambazo, jamii imekuwa ikishauri kutozitumia bila kupata ushauri wa madaktari. 

Inaelezwa kwamba, sababu kubwa ya bakteria kuwa sugu kwenye antibiotiki, ni matumizi makubwa kupita kiasi au matumizi yasiyo sahihi, kwamba mengi kwa dawa hizo si ya lazima. 

Ninadhaani kuwapo kwa dawa hizo kwenye maduka mengi, isiwe sababu ya watu kuamua kwenda kuzinunua tu bila kupata ushauri wa kitaalamu unaowawezesha kupata vipimo sahihi kabla ya kununua na kumeza au kunywa. 

Kwa kuwa inashauriwa kwamba matumizi ya antibaiotiki ni kwa ajili ya maambukizi ya bakteria tu na kwamba mtu asiitumie kwa changamoto zinazosababishwa na virusi kama mafua, koo kuwasha au kikohozi.

Hivyo, ni muhimu kuzingatia hilo na kuepuka pia matumizi ya dozi tofauti, kuvusha dozi au kutumia kwa muda mrefu zaidi, kwa kuwa kitendo hicho kinasababisha usugu wa dawa, hata kama mtu atajisikia vizuri baada ya siku chache, asiache kumeza dawa ulizopatiwa.Bahati mbaya imekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya watu kufanya hivyo, huku wengine wakaitumia dozi ya dawa walizoandikiwa wengine au dawa zilizobaki hapo awali, kwani pia ni kujisababishia usugu. 

Kwa kuwa matumizi holela ya antibiotiki, yanaifanya serikali kutoa maelekezo kila mara kwa kuwataka Watanzania kuwa makini, badala ya kujisikia kuumwa na kwenda kununua dawa, ni vyema kila mmoja kuchukua hatua.

Ni juzi tu serikali imetahadharisha matumizi mabaya ya dawa za antibaiotiki ambazo zinasababisha usugu wa vimelea dhidi ya dawa, ikionya hatari ya kutokea madhara makubwa hasa kifo kwa watumiaji.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu, anasema jijini Dar es Salaam kuwa takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 92 ya antibiotiki zinatumika nchini zimesababisha usugu kwa asilimia 59.8. 

Si mara ya kwanza kwa serikali kutoa onyo kwa Watanzania kuhusu matumizi holela na dawa hizo, kwani mwaka 2018, ilionya, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuchukua hatua zitakazomfanya awe salama dhidi ya antibiotiki. 

Mwaka huo wakati akizindua Mwongozo wa Matibabu nchini na orodha ya taifa ya matumizi ya sawa muhimu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akatahadharisha kuhusu matumizi ya antibiotiki. 

Kwamba, antibiotiki zitatumika katika ngazi ya hospitali za rufani za kanda, hospitali ya taifa na hospitali maalum, lakini zinauzwa latika maduka ya dawa, huku watu wakinunua na kutumia bila ushauri wa madaktari.

Kitendo cha baadhi ya watu kutumia bila ushauri wa madaktari, maana yake ni kujitafutia madhara kikiwamo kifo kama ambavyo wizara ya afya inatahadharisha umma wa Watanzania.

Top of Form

Bottom of Form

Top of Form

Bottom of Form